26.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 8, 2022

Contact us: [email protected]

Ruby: Nitafunika zaidi nikisimama mwenyewe

Hellen George 'Ruby'
Hellen George ‘Ruby’

Na JOHANES RESPICHIUS

STAA wa muziki wa Bongo Fleva aliyeibuliwa na kibao ‘Na Yule’, Hellen George ‘Ruby’ ameibuka na kueleza mengi kuhusiana na muziki wake baada ya kimya cha muda mrefu.

Msanii huyo ambaye amepitia katika Jumba la Vipaji Tanzania (Tanzania House of Talent) ‘THT’, amekuwa gumzo baada ya kuachana na uongozi uliokuwa ukimsimamia na kugeukia kufanya kazi zake kama msanii binafsi.

Mbali hilo, hivi sasa amekuwa katika majibizano kwenye mitandao ya kijamii na mtangazaji wa Kipindi cha Ala za Roho cha Radio Clouds FM cha jijini Dar es Salaam, Loveness Malinzi ‘Diva’ na hivyo kuzidi kuwaacha mashabiki katika hali ya sintofahamu.

Ruby ambaye vibao vyake Sijutii, Forever na Suu alioshirikishwa na Yamoto Band vinamng’arisha, amefunguka kwa mara ya kwanza tangu alipoachana na uongozi wake na kudai kuwa anaamini atafanya vizuri zaidi akijisimamia mwenyewe.

Hapa chini Paparazi wa Swaggaz anakuletea sehemu ya mahojiano hayo, ambapo Ruby anaeleza yanayoendelea katika staili yake mpya ya maisha ya kimuziki.

Swaggaz: Kwanini tangu uachane na uongozi wako wa awali kumekuwa na malumbano katika mitandao ya kijamii  kati yako na Diva?

Ruby: Kwanza kwa jambo linalohusu uliokuwa uongozi wangu siwezi kulizungumzia kabisa kwa sasa. Lakini kwa faida ya mashabiki wangu, ni kwamba wategemee mazuri zaidi. Najisikia huru na naamini nitafanya vizuri zaidi nikijisimamia.

Kuhusu Diva, bora tu niachane naye maana sioni vitu vya kumuongelea kama anavyofanya yeye. Zaidi namuonea huruma tu, namsikitikia na ninamwombea kwa  Mungu amrudishie akili zake. Nahisi ana ugonjwa wa kusahau, jambo ambalo ni baya sana kulingana na umri wake.

Swaggaz: Umesikika kwenye wimbo wa Suu wa Yamoto Band, lakini kwenye video yake hujaonekana kushirikiana nao, badala yake sehemu yako amecheza msichana mwingine. Nini kilitokea?

Ruby: Ukweli ni kwamba sikukataa kufanya video hiyo… tatizo ni mapatano hayakuwa mazuri, walishindwa kutimiza kile nilichokuwa nakihitaji.

Swaggaz: Kuna tetesi kwamba kilichosababisha uachane na uongozi wako ni kutaka kuwa chini ya mwanamuziki Jide, ikoje hiyo?

Ruby: Siyo kweli na sijawahi kuongea jambo hilo sehemu yoyote wala kumtafuta Jide kuhusiana na suala hilo.

Swaggaz: Kwahiyo hutegemei kufanya naye kazi?

Ruby: Nategemea lakini kwa sasa bado, kulingana na mambo yanayoendelea miongoni mwa watu lakini kuhusu mimi kukutana na  Jide  ni ndoto yangu ya muda mrefu kwakweli.

Swaggaz: Changamoto gani kubwa ambazo umepitia katika safari yako ya sanaa?

Ruby: Jambo kubwa ambalo lilikuwa likinipa huzuni ni watu kunikashfu, kunichukulia poa na kutengenezewa chuki bila sababu. Watu hatufanani. Siyo kila nilichonacho mimi mwenzangu anacho, vipo vitu vingi sana ninavyo lakini Beyonce hana. Hivyo hivyo anavyo vingine ambavyo sina,   kibongobongo ni vigumu kuelewa ndiyo maana wasanii tunawekeana chuki.

Swaggaz: Jambo gani la huzuni na la furaha yaliyowahi kukutokea maishani mwako kiasi huwezi kusahau?

Ruby: Nilihuzunika sana niliposikia watu wakisema mimi nakataa kufanya video na wasanii wenzangu, kitu ambacho siyo cha kweli. Ukweli ni kwamba wengi wanaotaka hivyo wanashindwa kufikia makubaliano.

Jambo la furaha ambalo siwezi kulisahau ni pale nilipokubaliwa na mama yangu kuanza kufanya muziki wa Bongo Fleva na kuachana na nyimbo za Injili. Ilikuwa siku nzuri sana kwangu.

Swaggaz: Kwa ufupi nini kilisababisha ukaamua kuachana na nyimbo za Injili na  kuingia kwenye Bongo Fleva?

Ruby: Muziki wa Bongo Fleva na Injili ni vitu viwili tofauti kabisa kwani kwa upande wa Injili ni kama kuhubiri lakini Bongo Fleva uko kibiashara zaidi, hivyo niliingia huku kwa sababu ya biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,682FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles