BARCELONA, HISPANIA
UONGOZI wa klabu ya Barcelona umefikia makubaliano na mshambuliaji wa timu hiyo, Neymar ya kumuongezea mkataba mpya ambao utamfanya akae Nou Camp hadi 2021.
Julai mwaka huu klabu hiyo iliweka wazi kuwa ina mpango wa kutaka kumwongezea mkataba mchezaji huyo wa miaka mitano, lakini walishindwa kufanya hivyo kwa wakati huo kutokana na mchezaji huyo kujiunga na timu ya taifa kwa ajili ya michuano ya Olimpiki.
Kupitia mtandao wa klabu hiyo, umeweka wazi kuwa tayari uongozi na mchezaji huyo umefikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya Oktoka 21 mwaka huu ambapo itakuwa kesho kutwa Ijumaa.
Mchezaji huyo ambaye amekuwa na mchango mkubwa ndani ya klabu ya Barcelona pamoja na timu ya taifa ya Brazil, alikuwa anawindwa na mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini Ufaransa, PSG, ambao walikuwa tayari kuweka mezani kitita cha Euro milioni 193, huku wakidai kuwa walikuwa tayari kumpa mshahara wa Euro 650,000 kwa wiki.
Baada ya usajili huo ambao utafanyika Ijumaa, mchezaji huyo atakuwa anachukua kitita cha Euro milioni 16 kwa mwaka, wakati usajili wake utakuwa wa Euro milioni 200 kwa mwaka wa kwanza, Euro milioni 222 kwa mwaka wa pili na Euro milioni 250 kwa miaka mitatu ya mwisho.
Hata hivyo, klabu hiyo tayari imemalizana na nyota wake Javier Mascherano ambapo wamempa mkataba mpya utakaomfanya akae ndani ya klabu hiyo hadi 2019.
Beki huyo wa timu ya taifa ya Argentina mwenye umri wa miaka 32, alikubali kusaini mkataba na klabu hiyo tangu Julai mwaka huu, lakini mpango huo umekamilika tangu Jumatatu baada ya kukutana na rais wa klabu hiyo, Josep Maria Bartomeu.
Mchezaji huyo alihusishwa kutaka kujiunga na klabu ya Juventus katika kipindi cha majira ya joto kuungana na Dany Alves ambaye amejiunga na timu hiyo.
Mascherano hadi sasa ameitumikia klabu hiyo na kucheza michezo jumla 290 tangu ajiunge na klabu hiyo akitokea Liverpool miaka sita iliyopita na kufanikiwa kutwaa mataji 17 kwa kipindi chote hicho.