KOCHA wa klabu ya Valencia, Gary Neville, amedai kwamba timu yake ilikuwa haina uwezo wa kuwafunga wapinzani wao, Barcelona, katika michuano ya Kombe la Copa del Rey hatua ya nusu fainali ya pili.
Katika mchezo huo, timu hizo zilitoka sare ya 1-1, wakati mchezo wa awali ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Camp Nou, Barcelona ilifanikiwa kushinda mabao 7-0.
“Tuliingia uwanjani huku tukijua kwamba lazima tupoteze mchezo huo kwa kuwa mchezo wa awali tuliupoteza kwa kufungwa mabao mengi, hivyo ilikuwa ni kazi ngumu ya kuweza kurudisha mabao hayo.
“Barcelona ni klabu kubwa, ina wachezaji wenye uwezo, hivyo akili yetu ilikuwa inaangalia mchezo wa Ligi Kuu nchini Hispania dhidi ya Espanyol mwishoni mwa wiki hii na si mchezo huo.
“Baada ya kufungwa mabao 7-0 katika mchezo wa awali, niliweka wazi kwamba nguvu zetu zinaelekea kwenye mchezo wa Ligi Kuu na si Copa del Ray tena, kwa kuwa ilikuwa ngumu kuifunga klabu hiyo ya Barcelona,” alisema Neville.
Kwa hatua hiyo, Barcelona imefanikiwa kutinga hatua ya fainali kutokana na ushindi huo dhidi ya Valencia wa mabao 8-1.
Hata hivyo, kocha wa Barcelona, Luis Enrique, alikishusha dimbani kikosi chake bila wachezaji wake nyota kama vile, Lionel Messi, Luis Suarez, Neymar, Gerrard Pique, Dani Alves na wengine wengi.