Na MWANDISHI WETU-DAR E S SALAAM
Wataalamu kutoka Baraza la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC), kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wamechukua sampuli zaidi ya kumi ya maji kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kubaini kama maji hayo yana kemikali zenye madhara kwa viumbe hai.
Sampuli ya maji hayo yanayodhaniwa kuwa na kemikali yanayotiririka kutoka katika Mgodi wa Acacia North Mara mpaka kwenye makazi ya watu.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli, alilolitoa hivi karibuni alipokuwa ziarani Mkoani Mara.
Akizungumza jana Wilayani Tarime, wakati zoezi hilo hilo likiendelea, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Dk.Vedast Makota, alisema wameanza kutekeleza agizo hilo kwa kuchukua sampuli katika maeneo yote ili kubaini kama zina madhara kwa viumbe hai au la.
“ NEMC kwa kushirikiana na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali watafika kila mahala ikiwemo kupitia vibali vyote vya awali ili kubaini kama utolewaji wa vibali hivyo ulikidhi vigezo vinavyotakiwa na kuona kama wamiliki wa mgodi huo wanazingatia masharti yaliyoagizwa katika vibali hivyo,” alisema Dk. Makota
Alisema utafiti wao utaenda sanjari ya uchukuaji sampuli mbalimbali yakiwemo maji, mimea na mchanga ambapo watahakikisha wanashirikiana na jamii inayozunguka mgodi huo ili kufanikisha zoezi zima kuona kama kuna viashiria vinavyoshukiwa kuwa na chembe chembe zenye kemikali.
“Tupo katika hatua za awali za utekelezaji wa agizo hilo ambapo wataalumu wametembelea maeneo ya mto Tigite, ambao kwa kiasi kikubwa maji yake ndiyo yanatumika sana wakazi wa eneo hilo kwa shughuli mbalimbali za kijamii,” alisema.
Alisema wameshatembelea mabwawa mbalimbali yanayotumika kuhifadhia tope sumu zinazotokana na shughuli za mgodi huo ikiwemo wataalamu kutoka kwa mkemia mkuu wa serikali kuchukua sampuli mbalimbali ambazo zitapelekwa maabara kwaajili ya kufanyiwa vipimo vya kitaalamu.
“Baada ya kukamilisha zoezi la utafiti na uchukuaji sampuli hizo na kubaini ukiukwaji wa sheria za mazingira ni wazi kuwa NEMC haitosita kuchukua hatua kali za kisheria kwa mmiliki ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema Dk. Makota.
Naye Meneja wa Kanda Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Venkya Masambu alisema kwa kutambua uharibifu mkubwa unajitokeza katika maeneo ya migodini ofisi yake kwa kushirikiana na NEMC waliamua kuchukua sampuli hizo upya ambazo watazipekela katika maabara ya
serikali yenye wataalamu waliobobea.
“Endapo sampuli zitakayopelekwa kwa mkemia mkuu zitabainika kuwa na madhara kwa binaadamu hawatasita kutoa ushauri kwa wamiliki wa mgodi ili kuona namna gani ya kutatua dosari zinazoweza kujitokeza,” alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa Uendeshaji Idara ya Uchenjuaji Dhahabu wa Acacia North Mara, Patice Kabazimu alisema wamewapokea wataalamu hao na kwamba watahakikisha wanawapatia ushirikiano wa kutosha kufanikisha kazi yao.
“Kiukweli sisi kama Acacia tunatambua umuhimu wa zoezi linalofanywa na wataalam hawa ili kuleta ustawi na maendeleo kwa jamii yetu,” alisema
Ujio wa wataalamu kutoka NEMC na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imepokewa kwa shangwe na mwananchi wakiwemo viongozi wa vijiiji na vitongoji ili waone uhalisisa wa kile wanachokiita kuwa ni maji yenye kemikali.
Kwanza kabisa nimshukuru sana MH. Rais wa jumhuri ya muungano wa Tanzania kwa kututembelea sisi wananchi wa tarime,lakini pia kubaini tatizo LA maji ya MTO tigite kutililisha maji ya sumu yatokanayo na kemikali za mgoni; wito WANGU kwa ofisi ya mkemia mkuu wa kanda,na ofisi ya mazingira wafanye kazi yao kwa waledi na kuzingatia maadili ya taaluma yao-wasije wakapokea rushwa na kupotosha ukweli wa tatizo hili kama ilivyotokea wakati ule na sisi wananchi tunaimani na serikali ya awamu tano,hivyo sisi waathirika wa tatizo hili tutarajie majibu chanya; asante gazeti la mwananchi kwa kupaza sauti kwa hili