25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

NEMC: Chupa za plastiki zimeathiri fukwe

Na Mwandishi wetu -Dar-es-salamm

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesema kuwa limebaini kukithiri kwa chupa za plastiki katika fukww mbalimbali nchini.

Kutokana na hali hiyo, NEMC imeitaka jamii kujenga utamaduni wa kusafisha fukwe nchini ili kulinda mazingira wakati wote.

Hayo yalisemwa jana wakati wafanyakazi wa NEMC kwa kushirikana na asasi za kiraia walipofanya usafi katika fukwe ya Andy-Mbezi B ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.

Asasi hizo za kiraia zilizoshirikiana bega kwa bega katika zoezi zima la kusafisha fukwe ni pamoja na Nipe fagio, Aspect na Green Waste Pro.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kufanya usafi katika fukwe hiyo,  Kaimu Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki, Benjamin Mchwampaka, alisema ni muhimu wananchi wakajenga mazoea ya kusafisha fukwe kwani ni eneo linalojumuisha jamii mzima.

“Fukwe hii ya Andy imekuwa na uchafu mwingi kutokana na kutofanyiwa usafi kwa muda mrefu hiyo kwa kufanya zoezi hili kutahamasisha wakazi wa maeneo haya kujitoa katika kufanya usafi mara kwa mara ili kufanya mazingira ya fukwe kuwa salama,” alisema Mchwampaka.

Alisema katika kufanya usafi, wamebaini chupa za plastiki ambazo hazirejerezwi zinazofungashiwa vinywaji mbalimbali ndio zimekithiri katika maeneo mengi ya fukwe na kusababisha mazingira kutokuwa salama kutokana na kukithiri kwa uchafu.

“Tumefanya kuchambua taka katika makundi mbalimbali ili kutupa urahisi wa kubaini aina za taka, hususani chupa za rangi na kufuatilia mzalishaji ili tusaidiane nae katika kutafuta suluhu ya kufanya urejereshaji wa chupa hizo ili kuondoa tatizo hilo,” alisema Mchwampaka.

Alisema tayari kuna vijana wamejiajiri kukusanya chupa nyeupe na kujipatia kipato kwa kurudisha kwa mzalishaji kwa ajili ya kuzirejereza, hivyo njia hii iliyoondoa chupa za maji kuzagaa mitaani, ndiyo itakayotumika kuondoa chupa za rangi.

“Kwa asilimia kubwa taka za plastiki ni janga kutokana na ukweli kwamba kwenye mazingira zinapoingia ardhini zinaweza kukaa muda mrefu bila kuoza na pia kama vinaingia baharini zinakwenda kuharibu ikolojia na kupelekea viumbe wa baharini kupotea,” alisema.

Mchwampaka alisema Serikali imepiga hatua kubwa katika kulinda mazingira kwa kukataza matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo ilikuwa ikiendelea kuharibu taswira ya nchi kimazingira na kusababisha maeneo mengi kuathirika.

“Kaulimbiu kwa sasa katika kuyalinda mazingira ni “Tuungane kuweka mazingira yetu safi na salama tusibadili vifungashio kuwa vibebeo,” alisema na kuongezea kuwa elimu kwa umma bado inaendelea kutolewa katika kuwajengea uelewa wananchi juu ya tofauti ya vifungashio na vibebeo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles