Na Mwandishi Wetu-Dodoma
SERIKALI imewataka wabunge kuielewa dhana ya ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji (Local Content) waweze kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi kushiriki kwa ukamilifu kwenye shughuli za uchumi na uwekezaji nchini.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama ambaye aliwataka wabunge hao kuhakikisha wanatumia nafasi zao kutoa elimu kwa wananchi.
“Mafunzo haya yanayotolewa kwenu yatasaidia kuleta mabadiliko chanya na jamii itashirikishwa kwa ukamilifu katika uwekezaji unaofanyika katika maeneo yao kupitia kwenu nyinyi wabunge,” alisema.
Alisema wakati umefika kwa Watanzania kuanza kunufaika kutokana na uwekezaji na hatimaye uchumi wa nchi kukua.
“Ni muhimu wananchi waliopo katika sehemu ambako viwanda au miradi inaanzishwa kushirikishwa katika hatua za awali za uwekezaji au utekelezaji wa miradi,” alisema Mhagama
Alisema mafunzo hayo kwa kamati mbalimbali za Bunge, pia yametoa nafasi kwa wabunge kutambua majukumu ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ambalo ndilo lenye dhamana ya kuratibu shughuli zote za uwezeshaji nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya NEEC, Dk. John Jingu, alisema uhusiano wa karibu kati ya wawekezaji na wananchi katika eneo la mradi unatakiwa kuimarishwa ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji wa miradi katika maeneo yao.
“Changamoto kubwa ni ujuzi wa wananchi wetu katika uwekezaji na ushiriki wao,” alisema Dk. Jingu na kuongeza kuwa Baraza limejipanga kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu ya namna bora ya kushiriki katika uwekezaji na kukuza uchumi wao.
Mbunge wa Muheza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu, alisema semina hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwao.
“Tuna kila sababu za kuwaelimisha wananchi wetu juu ya kuongeza thamani ya bidhaa waweze kuendana na matakwa ya wawekezaji,” alisema Balozi Adadi.
Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng’i Issa, alisema lengo kubwa la semina hiyo kwa wabunge ni kuwafahamisha majukumu ya baraza na pia mchango wao katika dhana hiyo ya ushiriki wa wananchi katika uwekezaji.
“Wabunge wanatoka katika halmashauri ambako miradi inafanyika, hivyo italeta wepesi kwao kusimamia utekelezaji wa dhana hii itakapoanza,” alisema Beng’i.
Wajumbe 152 wa kamati za Bunge walihudhuria semina hiyo iliyoratibiwa na NEEC na kudhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).