25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

NEC YATUPA PINGAMIZI ZA WAGOMBEA

tume-ya-taifa-ya-uchaguzi

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetupilia mbali rufaa za pingamizi za wagombea wa ubunge na udiwani katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Januari 22, 2017.

Taarifa iliyosambazwa jana kwa vyombo vya habari na Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Hamid M. Hamid, ilieleza kuwa, rufaa hizo zilikataliwa kutokana na kutokuwa na mashiko kisheria.

Alisema kati ya rufaa hizo, moja ilikuwa ya kupinga uteuzi wa mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Razak Khatib, katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani – Zanzibar, iliyokatwa na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Juma Ali Juma, ambaye alipinga uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi kumsimamisha mgombea huyo.

“Rufaa hiyo ilikuwa na sababu mbili ambazo ni:- (i) Hakurudisha fomu za uteuzi kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria na (ii) Hakudhaminiwa na chama cha siasa kugombea ubunge,” alisema Jaji Hamid.

Alisema katika kikao kilichofanyika jana, Tume ilipitia rufaa hiyo na kuona sababu zilizotolewa na mkata rufaa hazina nguvu kisheria, kwa kuwa, mgombea wa CUF alirudisha fomu za uteuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu.

“Fomu zake za uteuzi zimesainiwa na kugongwa muhuri wa Katibu wa Wilaya ya Magharibi B. Kwa mantiki hiyo, Tume imekubaliana na uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dimani – Zanzibar. Hivyo, mgombea wa CUF amekidhi vigezo na uteuzi wake ni halali, aendelee na kampeni za kugombea nafasi ya ubunge wa Jimbo hilo,” alisema Jaji Hamid.

Jaji Hamid alisema pia NEC ilipokea rufaa tatu kutoka Kata ya Kijichi – Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, Kata ya Misugusugu – Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani na Kata ya Ihumwa – Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Mkoa wa Dodoma.

Alisema katika Kata ya Misugusugu, rufaa ilikuwa ya mgombea wa Chadema, Gasper Ndakidemi dhidi ya mgombea wa CCM, Bogasi Ramadhani, huku Kata ya Kijichi, rufaa ikiwa ya mgombea wa CUF, Khadija Shamas, dhidi ya mgombea wa Chadema, Fredrick Rugaimukamu.

Jaji Hamid alisema katika Kata ya Ihumwa rufaa ilikuwa ya mgombea wa Chadema, Magawa Juma, dhidi ya maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi.

“Rufaa ya mgombea wa Chadema, Ndakidemi katika Kata ya Misugusugu na ya mgombea wa CUF, Khadija katika Kata ya Kijichi, hazina mashiko ya kisheria na zimekataliwa. Hivyo, Tume inakubaliana na uamuzi wa wasimamzi wa uchaguzi wa Halmashauri hizo na wagombea waendelee na kampeni kwa mujibu wa ratiba,” alisema Jaji Hamid.

Akielezea rufaa ya mgombea wa Chadema kutoka Kata ya Ihumwa, Jaji Hamid alisema Tume ilipokea barua ya msimamizi wa uchaguzi Manispaa ya Dodoma, ikiwa imeambatanishwa na barua ya mgombea huyo ya kuiondoa rufaa yake na kwamba anakubaliana na maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi ambayo yalimuengua.

“Leo (jana) Tume ilipokea barua za kujitoa kugombea za wagombea wa Chadema na ACT – Wazalendo katika Kata ya Ihumwa. Kwa maana hiyo, rufaa iliyokuwa imekatwa na mgombea wa Chadema imeondolewa kwa kuwa mkata rufaa ameiondoa na amejitoa kabla haijasikilizwa,” alisema Jaji Hamid.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles