24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

NDUGAI ATOBOA SIRI YA MAALIM SEIF

Na EVANS MAGEGE -DAR ES SALAAM

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ametoboa siri ya kutofanya kazi na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kwani hatambuliwi na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Amesema licha ya kiongozi huyo, pia hawezi kufanya kazi na wabunge waliofukuzwa na chama hicho kwani utaratibu ulifuatwa na sasa ofisi yake inajiandaa kuwaapisha wabunge wapya Septemba 5, bungeni mjini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam jana, Ndugai alisema kuwa msimamo huo ni suala la utaratibu kwa sababu mwenye kumbukumbu za vyama vya siasa na viongozi wake halali ni Msajili wa Vyama vya Siasa.

Alisema ikiwa atasema kuwa hamfahamu mtu na yeye lazima asimfahamu kwani ndiyo utaratibu wa kazi unavyotaka.

“Kwa hiyo linapotokea jambo kwenye chama ambacho kina mvutano, kazi yangu ni kumuuliza huyo mweka hazina wa vyama vya siasa kwa maana hiyo niliyoieleza, kwamba kuna huyu, aah huyu simfahamu, basi na mimi nakuwa simfahamu. Akisema namfahamu basi na mimi nakuwa namfahamu.

“Lazima twende kwa utaratibu, ni sawa na taasisi fulani ambayo inatakiwa iandikishwe BRELA, mnanielewa?  Ikatuandikia Bunge jambo fulani, lazima tuiulize BRELA bwana unamjua huyu, akisema hatumjui, maana yake na mimi simjui. Sasa siwezi kuzuka nikawa nawatambua watu ambao hawatambuliwi na BRELA, kwa maana hiyo ya makampuni na kadhalika na msingi huo siwezi kuwatambua watu ambao hawatambuliwi na msajili.

“Kwa sababu huko ndiko vyama vinakopeleke Katiba zao, huko ndiko vyama vinakopeleka mabadiko ya kumbukumbu zao za mikutano ya mabadiliko yoyote yale,” alisema Ndugai.

Aliendelea kufafanua kwamba tangu Machi mwaka huu, alipata barua kutoka kwa Msajili iliyomweleza kwamba amepata taarifa rasmi kuwa Maalim Seif hayupo ofisini, kwa msingi huo majukumu ya chama hicho yatatekelezwa na Naibu Katibu Mkuu wake hadi hapo itakapoelezwa vinginevyo.

“Kwa hiyo huo ndio msimamo wa tangu Machi kwa mujibu wa barua niliyokuwa nimeandikiwa kama rekodi ya kufanyiwa kazi, sasa ninapoletewa barua na mtu huyo baadaye ungekuwa wewe ungefanyaje wakati umekwishaharifiwa kwamba huyo mtu hayupo ofisini? Sasa swali la kwanza ni kumuuliza huyo mtu ameisharudi ofisini? Akikwambia hapana, sasa barua naandikia wapi, Kongwa?

“Kwa hiyo inakuwa ngumu kidogo. Ni tatizo la kwao, hamuwezi kumlaumu Spika au mtu mwingine. Ni usafi wa kufanya ndani kwao wenyewe, wakifanya usafi wao sisi wala hatuna tatizo. CUF ikisema inakutambua wewe sisi tutapinga? Hili ni la kwao na wanajua zaidi wao kuliko sisi, tuwaachie wao wenyewe wenye jukumu la kusafisha nyumba yao,” alisema Ndugai.

 

VIINUA MGONGO

Katika hatua nyingine, alifafanua kuhusu viinua mgogo vya wabunge wa Viti Maalumu wa CUF waliovuliwa ubunge, akisema kuwa kwa mbunge mwenye stahili zake atapata na asiye na sitahili atakosa. Pia kama ana madeni yatamfuata alipo.

“Hili linabidi kukaa chini na kuona ni nini mtu anastahili na nini mtu hastahili. Inategemeana, yapo mambo mengi sana, maana kuna wengine wana mikopo, unaweza kusema anastahili kumbe inajifyeka humo kwa humo na kadhalika,  kwa hiyo ni ngumu kusemea hicho kwa sasa hizi, lakini kama ana stahili zake atapata na kama hastahili atakosa na kama ana madeni anaondoka nayo,” alisema Ndugai.

 

RIPOTI YA LUGUMI

Akizungumza kuhusu ripoti ya Lugumi, alisema bungeni kuna ripoti nyingi, hivyo angepata muda wa kutosha angeizungumzia zaidi.

Hata hivyo, alidokeza kwa ufupi kwamba kamati ilikuwa ni ya kufuatilia utekelezaji wa mkataba wa uwekaji wa vifaa vya polisi kwenye vituo kadhaa.

Alisema kamati hiyo kazi yake kuu ilikuwa ni kukagua na kuainisha ni maeneo gani hayajakamilika na kwa nini hayajakamilika alafu Serikali ikapewa kazi ya kuhakikisha inakamilisha zoezi hilo ili hoja hiyo iweze kufungwa.

“Kwa kawaida baada ya muda fulani lazima apite tena ‘Auditor General’ katika mwaka mwingine wa fedha, aangalie kama yale yaliyodaiwa yamekamilika.

“Kwa hiyo katika ripoti ya ‘Auditor General’, hii ambayo imewekwa bungeni, huenda akawa amesema sasa jambo lile ameridhika nalo, hivyo yeye anaweza akafuta hoja sio Bunge, kama hajaridhika Bunge tunaendelea kufuatilia kuibana Serikali kuhakikisha kwamba hoja ile inafungwa,” alisema.

 

KAMATI ZA TANZANITE, ALMASI

Akizungumzia ufanisi wa kamati za madini ya almasi na tanzanite, Spika Ndugai alisema alikuwa hayupo nchini kwa siku kadhaa, hivyo leo anatarajia kwenda Dodoma na akifika  ataomba apewe mrejesho wa shughuli za kamati hizo.

Hata hivyo, alidokeza kwamba kwa taarifa alizonazo kwa sasa, kamati hizo ziliendelea kufanya kazi vizuri ingawa aliongeza kuwa wiki ijayo mapema atatoa taarifa ya nini kitafuata.

 

MALIPO KWA WABUNGE

Akijibu madai ya ucheleweshaji wa malipo ya wabunge na fedha za Mfuko wa Jimbo, Spika Ndugai alisema ni mapema kulisemea suala hilo.

Aliwataka waandishi wa habari kuvuta subira hadi atakapofika Dodoma na baada ya wiki moja anaweza kulitolea taarifa ya kina jambo hilo.

“Niseme tu hapa kwamba hivi sasa kamati mbili za Bunge zimeishaanza shughuli, Kamati ya Bajeti ipo hapa Dar es Salaam na imeishaanza kufanya kazi zake na Kamati ya Ukimwi nayo imeishaanza kazi zake, pia kamati mbili maalumu nazo zinaendelea na kazi zake.

“Lakini Jumatatu kamati zote za Bunge zitakuwa zipo kazini, nyingi kati ya hizo ziko Dodoma na pia Kamati ya Hesabu za Serikali inaanza kesho (leo). Sasa kama ingekuwa ni kweli sina pesa nisingeweza kuitisha kamati zote hizo,” alisema.

Awali Ndugai alikutana na ujumbe wa Spika wa Chama cha Wabunge wa Afrika, Cipriano Casama, ambaye aaikuja mahususi kuikaribisha Tanzania kujiunga na chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles