NA CHRISTOPHER MSEKENA
INAAMINIKA kila mwanadamu ana jambo linalomnyima usingizi kutokana na vita anayopigana ili kulitimiza kwa kulitoa katika fikra na kuliweka kwenye uhalisia. Hivyo ndivyo watu wote wenye mafanikio wameweza kutimiza ndoto zao.
Walifanikiwa baada ya kupigana vita ya maneno kwa kukatishwa tamaa, kupitia changamoto mbalimbali ambazo zilitoka kwa watu wao wa karibu, marafiki na wengine ambao waliamini hakuna mtu anayeweza kufanikiwa kupitia jambo hilo.
Nimeanza kwa utangulizi huo ili nipate nafasi ya kuchangia japo kwa uchache suala ambalo limejitokeza hivi karibuni katika sekta ya burudani hivi karibuni baada ya moja ya nyota wake kuweka wazi ndoto yake.
Miongoni mwa mijadala iliyogonga vichwa vya habari za burudani wiki hii, ni uamuzi wa memba wa kundi la Weusi, Nikk wa Pili, kuweka hadharani ndoto yake ya kuja kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nikk wa Pili, amewagawa watu katika makundi mawili yenye mitazamo tofauti dhidi ya ndoto yake. Kuna la watu waliomuunga mkono na kumtia moyo kuwa anaweza kuifikia ndoto hiyo lakini pia kuna wengine waliopinga.
Rapa huyo amejikuta katika vita iliyoanzishwa na watu wa rika lake ambao wamepinga maono yake waziwazi kiasi kwamba ilionyesha namna gani jamii yetu ina watu wenye husda kiasi cha mtu kuchukia ndoto ya mtu mwingine bila sababu.
Binafsi naamini Nikk wa Pili, amejipambanua vyema na kuona mpaka muda utakapofika atakuwa ametosha kuvaa viatu vya kuwa rais wa Tanzania, ni ndoto nzuri ambayo ikipitia michakato ya kuvunjwa vunjwa basi inaweza kutimia bila shaka.
Hivyo basi inawezekana kabisa rapa huyo kuwa rais kwa sababu ndoto ni mchakato, si kitu cha mara moja, kinahitaji maandalizi ya fikra, subira na kujifunza kila uchwao kwa watu waliofanikiwa kupitia ndoto inayofanana na yako.
Nimependa jinsi wasanii wa Tanzania, wanavyoamua kuvuka mipaka ya fikra zilizozoeleka, ndiyo maana ndoto ya Nikk wa Pili licha ya kuwa bado haijatimia imekuwa gumzo na kuzua mjadala.