24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

BOBI WINE AZUA GUMZO AFRIKA MASHARIKI, DUNIA

Na BADI MCHOMOLO


IMEKUWA wiki ya vilio na huzini nchini Uganda hasa kwa mashabiki wa staa wa muziki nchini humo, Robert Kyagulanyi, maarufu kwa jina la Bobi Wine, kukamatwa na kusota ndani hadi sasa.

Msanii huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kyadondo Mashariki nchini Uganda, alikamatwa na wiki iliyopita mara baada ya dereva wake kuuawa kwa kupigwa risasi.

Tukio hilo la kuuawa kwa dereva huyo lilitokea katika eneo la Arua, kwenye kampeni za uchaguzo mdogo baada ya mbunge wa jimbo hilo, Ibrahim Abiriga kuuawa, hivyo Bobi Wine na viongozi wengine kadhaa walikuwa kwenye jimbo hilo kwa ajili ya kumuunga mkono mgombea huru Kassiano Wadri.

Inadaiwa kampeni hizo zilikwenda sawa kwa kipindi chote kabla ya polisi kuanza kukabiliana na wafuasi wa Wadri ambao waliripotiwa kukabiliana na wale wa mgombea wa NRM Tiperu Nusura.

Vurugu hizo zilisababisha msanii huyo kukamatwa na polisi jambo ambalo lilionekana kupingwa na idadi kubwa ya wananchi, wakidai kuwa msanii huyo hakuwa na hatia.

Waandamanaji zaidi ya 103 walikamatwa na polisi  wakipinga msanii huyo kukamatwa, lakini vikosi vya jeshi la polisi vilizima maandamano hayo.

Hata hivyo kukamatwa kwake kulisababisha vurugu kubwa hadi moja kati ya magari ya Rais Yoweri Museveni kuvunjwa kioo cha nyuma likiwa katika msafara wake.

Juzi msanii huyo alifikishwa katika mahakama ya kijeshi na kufutiwa shitaka la umiliki haramu wa silaha, lakini muda mchache baadaye alikamatwa na kushtakiwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mkuu kwa mashtaki mpya ya uhaini.

Mahakama ilisema kuwa Bobi Wine anaweza kuwa huru iwapo hakuna mashtaka mengine yatakayowasilishwa dhidi yake. Wakati huo Wine alionekana akilia na kupangusa machozi wakati hukumu hiyo ikisomwa.

Alitoka nje ya mahakama akiwa anatembea kwa magongo na kuonekana kuwa na maumivu makali, kitu ambacho kiliwahuzunisha wengi waliojitokeza mahakamani hapo.

BIBI WINE NI NANI?

Ni msanii wa muziki wa Afrobeats, alizaliwa Februari 12, 1982 katika Wilaya ya Mpigi, lakini kwa sasa wilaya hiyo inajulikana kwa jina la Gomba, ila alikulia Kamwookya, Kaskazini mwa Jiji la Kampala.

Alianza kujulikana moja kwa moja kwenye tasnia hiyo ya burudani miaka ya 2000. Aliwahi kusema kuwa, lengo la kuingia kwenye muziki ni kutaka kuelimisha na kuburudisha jamii.

Moja ya kazi zake ambazo zilionekana kuelimisha jamii ni pamoja na ‘Kadingo’ ambayo ilikuwa inahusiana na masuala ya usafi wa mwili.

ELIMU

Msanii huyo alipata elimu ya muziki na uchekeshaji kwa ngazi ya shahada katika Chuo Kikuu cha Makerere.  Februari 2018 alimaliza Stashahada ya Sheria katika Chuo cha Law Development Centre (Chuo cha Maendeleo ya Sheria) kilichopo Kampala.

MUZIKI/FILAMU

Alianza muziki miaka ya 2000, wimbo wake wa kwanza kuuachia unajulikana kwa jina la ‘Akagoma’ kabla ya kuachia ‘Funtula’ na Sunda ambao alimshirikisha Ziggy D. Nyimbo hizo zilimfanya msanii huyo kujulikana kwenye ramani ya muziki.

Bobi Wine alikuwa Rais wa Fire Base Crew, lakini baada ya kundi hilo kuvunjika, alianzisha kundi lingine ‘Ghetto Republic of Uganja’ na aliendelea kuwa rais.

Kwa upande wa filamu, Wine aliwahi kufanya filamu ambayo inajulikana kwa jina la Binayuganda iliyotoka mwaka 2010, pia alishirikishwa kwenye filamu zingine kama vile Cleopatra Koheirwe, Yogera na zingine nyingi.

Mbali na muziki na filamu, msanii huyo mwaka 2008, chama cha ngumi nchini humo kilimpa leseni kwa ajili ya kushiriki mashindano baada ya kufuzu.

SIASA

April 2017, msanii huyo alitangaza kuingia kwenye siasa akidai kuwa anataka kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Kyadondo Mashariki. Alifanya kampeni yake nyumba hadi nyumba kwa ajili ya kuwashawishi watu wamjue, kitendo hicho cha kutembea nyumba kwa nyumba kilimfanya kuwa maarufu zaidi ndani na nje ya Uganda.

Alichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mdogo baada ya kusimama kama mgombea huru mwaka jana.  Aliwashinda wagombea kutoka Chama Tawala cha National Resistance Movement (NRM) na chama kikuu cha upinzani Democratic Change (FDC).

Hata hivyo katika kipindi kifupi cha uongozi wake, msanii huyo alitajwa kuwa mmoja kati ya viongozi ambao wamekuwa wakileta changamoto kwa Rais Museveni. Lakini mwenyewe alidai kuwa, aliwania nafasi hiyo kwa ajili ya kutaka kuwaunganisha raia kuwa kitu kimoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles