Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro
WAKATI Maadhimisho ya Siku 16 ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia yakiendelea kote duniani, ndoa za utotoni katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro bado ni changamoto.
Akizungumza na Mtanzania Digital hizi katika kijiji cha Mondoros kata ya Soitsambu, Afisa Maendeleo ya Jamii Msaidizi Mwandamizi wa halmashari ya Ngorongoro, Mary Hulilo, amesema vitendo vya kikatili vinavyotikisa kwa sasa ni ndoa za utotoni.
“Hali ya ukatili wa kijinsia ipo tunajitahidi kupambana nayo kwa kushirikiana na wadau wengine.Kwa sasa hali inayotikisa sana ni ndoa za utotoni,tunajitahidi kuelimisha watoto wa kike juu ya wao kupata elimu.
“Tunajaribu kuzunguka katika jamii kuhamisha hilo na kuelimisha watoto wa kike kukataa ukatili huo endapo wazazi watawaambia wasiende shule na kuwalazimisha kuolewa,tuna wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao tunawasaidia kwenda shule kwa kushirikiana na mashirika,” amesema Mary.
Amesema kutokana na jamii hiyo ya kifugaji kutokuona umuhimu wa kusomesha watoto wa kike,wamekuwa wakishirikiana na wadau wengine wa maendeleo katika kuhamasisha juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
“Tunashirikiana na wadau wengine kutoa elimu kwa wanafunzi na tunawapa mbinu ambapo asilimia kubwa hukimbilia kwetu au kwa wadau wengine na tunawatafutia namna ya kuwapeleka shule.
Kuhusu ukeketaji alisema kutokana na elimu inayoendelea kutolewa katika jamii suala hilo limepungua kwa kiasi kikubwa.
“Hali ya ukeketaji imepungua kwa asilimia kubwa baada ya kutoa elimu na elimu hii tumeanza kutoa kwa watoto wa shule za msingi kuanzia darasa la pili na tumekuwa tukitoa elimu hii kwa sasa inapofika wakati wa kufungwa shule watoto wakienda likizo matendo hayo ndo hufanyika hivyo kabla ya kufunga shule tunapita kutoa elimu,”amesema.
Mmoja wa wadau wa maendeleo anayehusika kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia wilayani humo, Kooya Timan, amesema wamesimamia na kutoa elimu kwa jamii juu ya kupinga ukeketaji hali iliyosaidia kupunguza vitendo hivyo kwa kiasi kikubwa.
Kuhusu ndoa za utotoni amesema amekuwa akishirikiana na serikali kuhakikisha wanasaidia wanafunzi wa kike ambao wanataka kuozeshwa.
“Nimesimama katika kusaidia wasichana wanaotaka kuozeshwa na hadi sasa nimeshasaidia wasichana zaidi ya 20 ambao walitaka kuozeshwa na wazazi wao.
“Wakati mwingine tunatishiwa lakini nikiona vitisho nawasiliana na ofisi ya maendeleo ya jamii au ustawi wa jamii na tunasaidiana.
“Wilayani hapa kumeanzishwa mabaraza ya haki ya wanawake haya nayo yanasaidia kutoa elimu kwa jamii na kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na wasichana,”amesema.