25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ndesamburo amshtaki RC kwa Rais Kikwete

ndesa-nov25-2013Gama-Moshi----October25-2014Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro

MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo amemshtaki Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama kwa Rais Jakaya Kikwete kutokana na kile alichosema ni harufu ya rushwa katika kugawa kiwanja cha umma kinyume cha sheria.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na mbunge huyo ilisema, kiwanja hicho chenye hati namba 10660 ambacho ndipo zilipo ofisi za Kata ya Mawenzi ambacho zamani kilikuwa kikimilikiwa na The Registered Trustees of Mawenzi Sports Club kabla ya kutwaliwa na Serikali mwaka 2002.
Alisema katika kuhakikisha kiwanja hicho kinabaki mikononi mwa umma, walifuatilia jalada la kumbukumbu za wadhamini wa taasisi ya Mawenzi Sports Club iliyomilikishwa kiwanja hicho kwa amri ya Gama na kubaini udanganyifu mkubwa.
Alisema walivyofuatilia jalada la taasisi hiyo lililopo Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Registration Insolvency and Trusteeship Agency – Rita), walibaini kuwa Januari tano 2008, wadhamini wa taasisi hiyo waliotajwa kuwa ni Devchand Nathu Shah na Mohamedali Shariff walifanya kikao ambacho kilihusika kuhamisha udhamini wao kwa Amratlal N. Pattn na Hitesh H. Solani.
“Lakini tumebaini kuwa Devchand Nathu Shah, alifariki dunia mwaka 1979 wakati Mohamedali Shariff alifariki mwaka 1998. Tunajiuliza ilikuwaje wadhamini hao waliofariki mwaka 1979 na 1998 wakae tena kikao Januari 2008 wakati walishafariki dunia?
Kumbukumbu za Return of Trustees za miaka iliyofuata baada ya kufariki (2000-2008), zinaonekana kuwasilishwa Rita mwaka 2012 zikiwa na sahihi ya wadhamini hao ambao tayari walikuwa wameshafariki dunia tangu miaka ya 1979 na 1998,” inasema taarifa hiyo.
Alisema kutokana na hali hiyo, “tuhoji umakini wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama na wote waliomshauri hadi akafikia hatua ya kuandika dokezo Novemba 26, 2014 akimwagiza Katibu Tawala wake (RAS) akibariki mchakato mzima wa uporaji huo.
“Ni rai yetu kwa Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama kwa kushindwa kutumia vyombo vyake kulinda mali ya umma isiweze kuporwa na kikundi cha watu wachache kwa kutumia mgongo wa maamuzi ya Ofisi ya RC Gama,” ilisema tarifa hiyo.
Ndesamburo, alimuomba Rais kutumia mamlaka yake kubatilisha hati mpya ya umiliki wa kiwanja hicho, ambayo wamepewa Mawenzi Sports Club kutokana na kubainika kwa udanganyifu huo.

Aliitaka pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuanzisha uchunguzi rasmi wa watendaji wote wa Serikali waliotumia vibaya madaraka yao na kupotosha ukweli juu ya uhalali wa umiliki wa kiwanja hicho.
Alisema mpaka sasa tayari Rita, imeshachukua hatua ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi wake, Gilbert Bubelwa, kuwaandikia barua wadhamini hao wapya na kuwasimamisha kutekeleza majukumu yao.
Taarifa hiyo ilisema Rita walichukua hatua hiyo kupitia barua ya Aprili 10, 2015.
Alisema barua hiyo imenukuu kifungu cha sheria namba 17 (1) cha sheria ya wadhamini sura 318 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002 kinachotaka ili udhamini wa wadhamini ukubaliwe, lazima kuwepo kikao halali na kuwepo na uangalizi wa mamlaka za Serikali.
“Ukisoma masharti ya vifungu vya sheria hiyo na udanganyifu tunaoamini umefanyika katika kutunga kikao na kuwahusisha watu ambao ni marehemu, ni dhahiri hata miamala (transaction) zote zilizofanywa na wadhamini hao ni batili mbele ya uso wa sheria,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles