NA JESSCA NANGAWE
DILI la kiungo mahiri wa Simba, Said Ndemla, kwenda kucheza soka la kulipwa Sweden limefikia hatua nzuri, ambapo anatarajia kusafiri nchini humo wiki ijayo.
Tayari klabu ya Simba imempa baraka zote kiungo huyo kwaajili ya kwenda kujaribu bahati yake katika klabu ya AFC Eskilistuna, inayomhitaji.
Akizungumza na MTANZANIA, meneja wa mchezaji huyo, Jamal Kisongo, alisema wapo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha taratibu zitakazomruhusu mchezaji wake kuingia Sweden.
“Suala la Ndemla lipo kwenye hatua za mwisho, kinachosubiriwa ni hati yake ya kusafiria ambayo wakati wowote itatoka, tunaamini siku yoyote kuanzia Jumatatu anaweza kuondoka,” alisema Kisongo.
Ndemla alikuwa anahitajika katika klabu hiyo tangu mwishoni mwa msimu uliopita, lakini uongozi wa Simba uliweka ngumu baada ya kudai bado ulikuwa unahitaji mchango wake katika kikosi cha Msimbazi.
Endapo kiungo huyo atafuzu majaribio yake, ataungana na Mtanzania mwingine, Thomas Ulimwengu, aliyejiunga na timu hiyo mapema Januari, mwaka huu.