Na TAUSI SALUM
-DODOMA
SERIKALI imeahidi kuleta ndege nyingine mbili za C Series ifikapo Novemba mwaka huu na Boeing nyingine Januari 2020, ikiwa na lengo la kutimiza ndoto yake ya kuhakikisha inafufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Ndege hizo zitakazowasili zitakuwa ni mwendelezo wa ndege zilizofika nchini awamu ya kwanza aina ya Bomberdiar na hivi karibuni kushuhudia kuwasili kwa ndege nyingine Boeing 878 Dreamliner.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, alisema manufaa ya ndege hizo yameanza kuonekana na zinasaidia wananchi wengi kusafiri na kufanya biashara zao kwa haraka.
“Tangu tulete ndege hizi abiria wa ATCL waliongezeka hadi kufikia 107.207 katika mwaka 2016/17 wakati mwaka 2015/16 walikuwa 49,173 ikiwa ni ongezeko la asilimia 118,” alisema Dk. Abbasi.
Akizungumzia gawio la mashirika ya umma kwa serikali, alisema yemekuwapo maneno ya kupotosha kutoka kwa wanasiasa kuhusiana na gawio la Sh bilioni 700 lililotolewa hivi karibuni kwa Serikali na mashirika hayo kuwa sio sahihi, jambo ambalo ni uongo.