24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBOSASA KUANZISHA WILAYA MPYA ZA  POLISI

Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, ametaka zianzishwe wilaya mpya za  polisi za Ukonga na Kawe   kukabiliana na matukio ya uhalifu ikiwamo ubakaji na uvunjaji.

Alikuwa akizungumza katika mkutano uliohusisha kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Ilala   katika Kata ya Zingiziwa Ukonga jana.

Kamanda Mambosasa alielezea kusikitishwa na kuendelea kwa matukio uhalifu katika Wilaya ya Polisi Ukonga licha ya kuwapo vituo vya polisi.

Alisema  umekuwapo ubabaishaji mkubwa kwa baadhi ya askari na wakuu wa vituo katika eneo hilo ikiwamo kuomba rushwa ili kuwapa watu dhamana wananchi.

“Nimeanza kuandika andiko tupate OCD hapa kwa sababu wananchi wanatembea umbali  mrefu, hata Wilaya ya Kawe pia tunataka tuipasue ili tupate wilaya mpya ya  polisi ya Mbweni, kuanzishwa kwa wilaya hii mtapata askari zaidi ya 100.

“Lengo ni kuweka mambo vizuri wananchi watukimbilie siyo watukimbie kwa hiyo nanyi wananchi tupeni taarifa tuzifanyie kazi. Tunataka Jeshi la Polisi litatue changamoto za wananchi na si kutengeneza changamoto,” alisema Mambosasa.

Alimwagiza Mkuu wa Kituo cha Kikuu cha Polisi Chanika kumpatia majina ya askari waliotumwa kushughulikia taarifa za mmoja wa wananchi aliyetoa taarifa ya mtu anayeuza gongo na kushindwa kuchukua hatua.

Katika ziara hiyo, Mambosasa alifuatana  na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sofia Mjema, kwenda eneo hilo kutatua kero hizo zinazowakabili wananchi.

Akitoa takwimu za uhalifu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Ilala, Salum Hamduni, alisema kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu yalikuwapo matukio 1,131 ikilinganishwa na matukio 1,674 mwaka jana.

Alisema katika kipindi hicho kulikuwa na matukio 89 ya ubakaji ikilinganishwa na matukio 78 mwaka jana, ulawiti matukio 20 kutoka 16 mwaka uliopita huku matukio ya dawa za kulevya yakipungua kutoka 10 hadi sita.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sofia Mjema, alisema kamati yake itaandaa utaratibu wa kuwataja wahalifu wote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles