* Makontena 11,884 yaliyopaswa kulipiwa kodi ya Sh bilioni 47 yalipitishwa kinyemela na kampuni saba za wafanyabiashara vigogo
* Magari zaidi ya 2000 yalipitishwa bila kulipiwa kodi ya bilioni moja kwa mwaka jana tu
*Mawakala wa Forodha 280 watuhumiwa kuhusika kukwepa kodi mpya nchini
Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imewakamata watumishi wake 15 ambao wanadaiwa kuhusika na ukusanyaji wa malipo ya tozo ‘wharfage’ na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 47. 418 kwa kutoa kinyemela makontena 11, 884 kwenye Bandari Kavu (ICD) saba.
Pamoja na uamuzi huo pia hivi sasa, mamlaka hiyo imeingia katika msako wa kuwakamata mawakala ambao bado hawajalipa kodi na kufikia Januari 10, mwakani wawe wamefikishwa polisi ili waweze kulipa fedha wanazodaiwa kwa mujibu wa sheria.
Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na mamlaka hiyo ilieleza kuwa watumishi hao pia wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 1.072 za malipo ya tozo ‘wharfage’ kwa magari 2,019 katika CFS sita.
Taarifa ilisema, baada ya kubaini hali hiyo Desemba 28, mwaka huu Bandari iliwafikisha polisi watumishi hao ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Watumishi hao ambao wametajwa katika taarifa hiyo ni Nathan Edward, John Elisante, Aron Lusingu, Aman Kazumari, John Mushi, Valentino Sangawe, Leticia Massawe, Christina Temu, Merina Chawala, Happygod Naftai, Adnan Ally.
Wengine ni Masoud Seleman, Bonasweet Kinaima, Benadeta Sangawe pamoja na Zainab Bwijo.
Bandari Kavu na tozo
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ICD zilizotajwa kuhusika na ukwepaji wa tozo hizo ni MOFEG ambayo ilikuwa na makontena 61 na kutakiwa kulipa tozo ya Sh milioni 513, DICD iliyokuwa na makontena 491 ambayo walitakiwa kulipa tozo ya Sh bilioni 3.888.
“JEFAG iliyokuwa na makontena 1,450 ilitakiwa kulipa tozo ya Sh bilioni 7.943, Azam ilikuwa na makontena 295 na kutakiwa kulipa tozo ya Sh bilioni 1.541 wakati PMM ilikuwa na makontena 779 na kutakiwa kulipa tozo ya Sh bilioni 4.510.
“…AMI ilikuwa na makontena 4,384 na kutakiwa kulipa tozo ya Sh bilioni 14.395 na TRH ambayo ilikuwa na makontena 4,424 na kutakiwa kulipa tozo ya Sh bilioni 14.625,” ilieleza taarifa hiyo
Magari 2019
Kwa upande wa CFS, jumla ya magari 309 yalitolewa katika CFS ya TALL ambayo yalitakiwa kulipiwa tozo ya Sh milioni 242.481, CHICASA ilikua na magari 65 ambayo yalitakiwa kulipiwa tozo ya Sh milioni 16.370, FARION ilikuwa na magari 18 ilitakiwa kulipa tozo ya Sh milioni 46,390,385.00 na SILVER iliyokuwa na magari 97 ambayo ilitakiwa kulipa tozo ya Sh milioni 168.904.
“MASS ambayo ilikuwa na magari 171 walitakiwa kulipia tozo ya Sh milioni 32. 807 na HESU iliyokutwa na magari 1,359 ikitakiwa kulipiwa tozo ya Sh milioni 565.533 ambapo jumla ya magari 2019 yalitakiwa kulipiwa Sh bilioni 1.072,” ilieleza taarifa hiyo
Kiama kwa makampuni
Kutokana na hali ya ukwepaji kodi, TPA imezitaka kampuni 280 ambazo zinahusika na kutolewa kwa makontena na magari bila malipo kuhakikisha zinawasilisha malipo husika.
Bandari ilitoa orodha ya majina ya kampuni hizo katika baadhi ya magazeti ya juzi ambapo zilitakiwa kuwasilisha nyaraka zao za kuanzia Julai mwaka jana hadi Aprili mwaka huu katika ofisi ya Meneja Biashara na Masoko kwa ajili ya uhakiki wa malipo waliyolipa kwa TPA.
“Mamlaka haitamvumilia mfanyakazi yeyote wa TPA awe mkubwa au mdogo ambaye atabainika anajihusisha na upotevu wa mapato ya bandari.
“Mawakala wote wa forodha ambao wataendelea kushirikiana na wafanyakazi wa bandari kutoa mizigo bila ya kulipa tozo ya wharfage serikali itawafutia leseni za kufanya biashara,” ilieleza.
Desemba 7, mwaka huu, TPA ilibaini upotevu wa makontena 2,431 yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye Bandari Kavu (ICD) nne za Azam, DICD, JEFAG na PMM bila ya kulipiwa tozo ya ‘wharfage’ ya kiasi cha Sh bilioni 1.912 na kusababisha watumishi 12 wa TPA wakiwamo wanane kufikishwa mahakamani.
“Ili kuhakikisha kuwa malipo ya wharfage ambayo hayakulipwa na mawakala wa forodha yanalipwa waliohusika walipewa notisi ya siku saba ili walipe fedha wanzodaiwa. Ndani ya siku saba za notisi Mawakala saba waliweza kulipa jumla ya Shilingi milioni 80.216.
“…baada ya muda waliopewa kwisha wale mawakala ambao walikuwa hajajalipa TPA ilisitisha kufanya nao biashara hadi walipe na pia walianza kukamatwa na kufikishwa polisi ambapo hadi Desemba 28, mwaka huu walilipa kiasi walichokuwa wanadaiwa ambapo jumla ya Shilingi milioni 820.473 zililipwa,” ilisema Bandari
Kutokana na hatua hizo jumla ya Sh milioni 900.690 zililipwa hadi kufikia Desemba 28, mwaka huu na zoezi la kuwakamata mawakala ambao bado hawajalipa linaendelea ambapo lengo hadi ifikapo Januari 10 mwakani wawe wamekamatwa na kufikishwa polisi ili walipe fedha zote wanazodaiwa.
Mbarawa atua TPA
Wakati huo huo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, jana alifanya ziara ya kushtukiza bandarini ili kuangalia utendaji wa kazi wa watumishi wa mamlaka hiyo.
Akiwa bandarini hapo, Profesa Mbarawa alisema watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na uharaka wenye tija ili kukidhi matarajio ya wananchi katika wizara hiyo.
“Tuwe tayari kubadilika, tufanye kazi kwa maslahi ya nchi, hivyo basi acheni kufanya kazi kwa maslahi binafsi, tambueni Serikali na wananchi wanahitaji huduma bora zitakazokuza uchumi wa taifa kutoka katika bandari zenu,” alisema Prof. Mbarawa.
Namna TPA ilivyoumizwa
Vigogo na watu wakubwa wenye ushawishi serikalini wakishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitajwa katika orodha aliyokabidhiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kama wahusika wakuu wa kupitisha kinyemela makontena takribani 2,780 na kukwepa kodi inayokadiriwa kuzidi Sh bilioni 600.
Kauli hiyo ilitolewa na mmoja wa maofisa wa TPA ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuhofia usalama wake.
Alisema katika ripoti aliyokabidhiwa Waziri Mkuu, Majaliwa imeeleza pia jinsi ‘wakubwa’ hao walivyofanikisha kupitisha makontena hayo kwa kutumia kampuni zao za mifukoni na vimemo.
Alisema tayari majina ya vigogo hao yamekabidhiwa kwa mtendaji huyo wa Serikali ambaye tangu ateuliwe kuwa waziri mkuu amefanya ziara ya kushtukiza mara mbili katika mamlaka hiyo na kuibua ufisadi huo.
Novemba 27, mwaka huu Waziri Mkuu Majaliwa, alisema taarifa za ukaguzi zilizopo zinaonyesha kuanzia Machi hadi Septemba mwaka 2014, makontena zaidi ya 300 yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne (ICDs) ambazo ni Jefang, DICD, PMM na Azam.
Alimuagiza Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga, kuhakikisha ndani ya kipindi cha wiki moja anabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka ‘billing system’, badala yake uwekwe mfumo wa malipo wa kielektroniki uitwao e-payment.
Miongoni mwa mifumo aliyoiangalia ni ya upokeaji na utoaji mizigo pamoja na utozaji wa malipo na aliikagua baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila kulipiwa ushuru.