Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
VIONGOZI wa nchi mbalimbali za Afrika jana walijitokeza kuaga mwili wa aliyekua katibu mtendaji wa kamati ya ukombozi kusini Afrika, Brigedia Jenerali Hashim Mbita katika Hosipitali ya jeshi ya Lugalo, Dar es salaam.
Mbali na nchi hizo, Rais Jakaya Kikwete aliongoza kuaga mwili wa marehemu Mbita akifuatana na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na viongozi waandamizi wa jeshi na vyama vya siasa.
Mwili wa Mbita uliagwa jana na marais wa nchi mbalimbali za Afrika zikiwamo Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia, Malawi, Msumbiji na nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Mbita alizikwa jana katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Viongozi waliopata nafasi ya kumzungumzia marehemu, walisema atakumbukwa na kutokana na msimamo wake wa kuhakikisha nchi za Afrika zinapata uhuru na kuondoka kwenye mikono ya wakoloni.
Mwakilishi wa Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, alisema Mbita aliweza kushirikiana na aliyekuwa kiongozi wa Chama cha African National Congress(ANC), Oliver Tambo kuhakikisha nchi hiyo inakuwa uhuru.
“Mbita alishirikiana na Oliver Tambo ili kuhakikisha Afrika Kusini inapata uhuru, jambo ambalo lilisaidia kuondoka kwenye mikono ya ubaguzi wa rangi na kuwa huru,” alisema.
Naye mwakilishi kutoka Namibia, Nentumbo Nandy, alisema Mbita alikuwa mstari wa mbele kutetea masilahi ya nchi za Afrika ikiwamo kuondoa utawala wa kikoloni.
Naye Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Msumbiji (Frelimo), Yemi Joseph, alisema katika uhai wake, Mbita alishirikiana na viongozi wa chama hicho kuandaa mafunzo ya kijeshi huko Nachingwea, jambo ambalo lilisaidia nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1975.
Aliongeza kutokana na hali hiyo nchi za Afrika zitaendelea kuenzi mchango wake kupitia mradi wa Hashim Mbita uliozinduliwa Agosti mwaka jana nchini Zimbabwe.
Akisoma risala ya Katibu Mkuu wa SADC, Dk. Stergomena Tax alisema nchi hizo zitaendelea kuenzi harakati za kiongozi huyo ili ziweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, alisema msiba huo ni mkubwa kwa sababu taifa limempoteza mpigania haki na maendeleo kwa nchi za Afrika.
Alisema mchango wa Mbita uliweza kuleta ukombozi kwa nchi nyingi za Afrika, jambo ambalo limezisaidia kupata uhuru.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alisema safari ya ukombozi kwa nchi za Afrika ilianza wakati wa uhai wa Mbita.
Akisoma wasifu wa marehemu, Brigedia Jenerali Dominic Mrope alisema Mbita alizaliwa Novemba 2 mwaka 1933 katika Kijiji cha Songoro mkoani Tabora na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Government Town mwaka 1946 hadi 1949.
Alijiunga na sekondari ya Government mwaka 1950 hadi alipohitimu kidato cha sita mwaka 1957.
Januari 1960 hadi Aprili 1960 alijiunga na Chuo cha East African School of Co-operatives huko Kabete nchini Kenya na kupata ujuzi wa mkaguzi wa ushirika.
Baadaye alijiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Novemba Mosi mwaka 1968 na kutunukiwa Kamisheni Aprili 1969.
MBITA NA UANDISHI
Kinana alisema mwaka 1960 Mbita alichaguliwa kuwa Ofisa Habari wa Mkoa wa Dar es Salaam na mwaka 1962 hadi 1965 alikuwa Ofisa Habari Mwandamizi wa mkoa huo huo.
Alisema mwaka 1965 hadi 1967 alichaguliwa na Rais Julius Nyerere kuwa Msemaji wa Ikulu na mwaka 1967 hadi mwaka 1968 alikuwa Katibu Mwenezi wa Chama cha TANU Mkoa wa Dar es Salaam.
Brigedia Jenerali Hashimu Mbita, ambaye alifariki juzi katika Hospitali ya Jeshi Lugalo alikokuwa amelazwa kwa matatizo ya moyo, alistaafu utumishi jeshini mwaka 1992 akiwa ametumikia kwa miaka 24 na miezi miwili.