26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Nato yaikalia kooni Urusi kwa kumpa sumu mpinzani wa Putin

 BRUSLESS, UBELGIJI

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami (NATO), Jenerali Jens Stoltenberg amesema kuna ushahidi usio na shaka kwamba mpinzani wa Urusi, Alexey Navalny amepewa sumu inayofahamika kama Novichok ambayo inaathiri neva. 

Tukio hilo ambalo limeibua mjadala mkubwa kati ya mataifa ya Magharibi na Urusi jana Nato imeielekeza nchi hiyo kushirikiana katika uchunguzi utakaoongozwa na taasisi ya kuzuia silaha za kemikali (OPCW).

“Matumizi yeyote ya silaha za kemikali ni yanaonyesha kutoheshimu maisha ya binadamu, na hayakubaliki,” Stoltenberg aliwaambia waandishi wa habari.

Awali Ujerumani ambako mwanasiasa wa upinzani nchini Urusi, Alexei Navalny anatibiwa ilisema kuna ushahidi ulio dhahiri kuwa alipewa sumu ya Novichok.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alisema mwanasiasa huyo alinusurika kuuawa na dunia itatafuta majibu kutoka kwa Urusi.

Navalny alisafirishwa Ujerumani baada ya kuanza kuugua akiwa ndani ya ndege huko Siberia mwezi uliopita na hadi sasa bado amepoteza fahamu.

Timu yake inasema alitiliwa simu kwa maagizo ya Rais Vladimir Putin. Hata hivyo Urusi imekanusha madai hayo.

Msemaji wa Urusi aliitaka Ujerumani kuishirikisha taarifa zake zote huku Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Maria Zakharova akilalamika kwamba madai ya Novichok hayakuambatinishwa na ushahidi wowote. “Ukweli uko wapi, ni mchakato gani uliotumika, yaani hata mtoe taarifa?” alisema.

Sumu inayoathiri neva ya Novichok ilitumiwa kwa aliyekuwa jasusi wa Urusi Sergei Skripal na binti yake wakiwa Uingereza mwaka 2018. Ingawa wao walinusurika, mwanamke mwingireza alifariki baadae akiwa hospitalini. 

Uingereza ilishutumu jeshi la Uingereza kwa kutekeleza shambulio hilo.

Jina Novichok maana yake ni “mgeni” kwa lugha ya Kirusi.

Ni jina linalotumiwa kurejelea kemikali za sumu ambazo hushambulia mfumo wa neva mwilini.

Kemikali hizo ziliundwa na Muungano wa Usovieti miaka ya 1970 na 1980.

Zilifahamika kama silaha za kemikali za kizazi cha nne na zilistawishwa chini ya mpango wa silaha za Muungano wa Usovieti uliofahamika kama “Foliant”.

Mwaka 1999, maofisa wa ulinzi kutoka Marekani walisafiri hadi Uzbekistan kusaidia kuvunja na kusafisha moja ya eneo kubwa zaidi lililotumiwa kufanyia majaribio silaha za kemikali na Muungano wa Usovieti.

Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa ngazi za juu ambaye alitorokea Marekani, maofisa wa Usovieti walitumia kiwanda kilichokuwa eneo hilo kuunda na kufanyia majaribio sampuli za kemikali ya Novichok. 

Kemikali hii iliundwa mahsusi kutoweza kugunduliwa na wakaguzi wa silaha na sumu katika mataifa mengine.

Madaktari walimtibu Alexei Navalny kwa siku tatu pekee kabla ya kuhamishwa hadi hospitali ya Charité mjini Berlin nchini Ujerumani.

Sumu hiyo pia inaelezwa kuwa ni yenye nguvu kuliko sumu nyingine

Moja ya kemikali hizi zinazofahamika kama Novichok – A-230 – inadaiwa kuwa na nguvu mara 5-8 zaidi ya sumu nyingine hatari kwa jina VX.

“Hii ni sumu hatari na changamano kushinda sumu aina ya sarin au VX na pia huwa vigumu zaidi kuitambua,” anasema Prof Gary Stephens, mtaalamu wa kemikali katika Chuo Kikuu cha Reading.

Sumu ya VX ndiyo iliyotumiwa kumuua ndugu wa kambo wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un mwaka jana, kwa mujibu wa Marekani.

Aina mbalimbali za kemikali hii ya A-230 zimekuwa zikitengenezwa, na aina moja inadaiwa kuidhinishwa na jeshi la Urusi itumike kama silaha ya kemikali.

Ingawa baadhi ya aina za sumu hii ya Novichok huwa majimaji, kuna aina nyingine ambazo ni yabisi (ngumu au isiyokuwa majimaji).

Ni kemikali ambayo pia inaweza kugeuzwa kuwa poda laini.

Baadhi ya sumu hizi pia hudaiwa kutumiwa kama silaha za ngazi mbili.

Hii ina maana kwamba sumu hii huhifadhiwa mara nyingi kama kemikali aina mbili ambazo zikiwa kando kando si hatari.

Zinapochanganywa, huingiliana na kutengeneza sumu.

Hii huifanya rahisi sana kwa viungo vya kemikali hii kusafirishwa kwani huwa sumu tu zikichanganywa.

“Moja ya sababu ambayo hufanya sumu hizi kuandaliwa ni kwa sababu viungo vyenyewe havijapigwa marufuku,” anasema Prof Stephens.

“Hii ina maana kwamba kemikali hizi ambazo huchanganywa huwa rahisi sana kusafirishwa bila kuwa hatari kwa anayezisafirisha.”

Sumu hiyo pia inaweza kuathiri mtu haraka sana

Mtu anapovuta sumu ya Novichok, au hata ikigusa ngozi yake, basi huanza kumuathiri upesi.

Dalili zake zinaweza kuanza kujionesha katika kipindi cha muda mfupi hivi, sekunde 30 hadi dakika mbili.

Hata hivyo, sumu hii ikiwa kama poda huchukua muda zaidi kuanza kuathiri mtu.

Dalili kali zinaweza kuanza kujionesha saa 18 baada ya mtu kukumbana na sumu hiyo.

Sekunde 30 tu zinatosha kwa dalili za sumu kuanza kujionesha

Sumu aina ya Novichok huwa na madhara sawa na ya sumu nyingine zenye kushambuliwa mfumo wa neva.

Hii ina maana kwamba huwa zinafanya kazi kwa kuzuia ujumbe au mawasiliano kati ya mfumo wa neva na misuli, na pia kusambaratisha shughuli nyingi muhimu za mifumo mwilini.

Dalili zake ni pamoja na macho kuwa na rangi nyeupe, huku mboni za macho zikiminyika, viungo kunyong’onyea, na mtu kuonekana kupumbaa. 

Wakati mwingine, mtu hupoteza fahamu, kushindwa na kupumua na kufa.

Sumu hizi kimsingi hufanya moyo kupunguza mapigo yake na kubana njia zinazotumiwa na mwili kupumua na mwishowe mtu kufariki kutokana na mtu kukosa hewa ya kutosha.

Baadhi ya aina za sumu hii ya Novichok zimeundwa mahsusi kuhakikisha dawa za kawaida za kupoza nguvu ya sumu haziwezi kufanikiwa.

Iwapo mtu amepewa sumu , anapaswa kuvuliwa mavazi yake na ngozi yake kuoshwa vyema kwa maji na sabuni.

 Macho yanafaa pia kuoshwa vyema kwa maji na apewe hewa ya oksijeni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles