24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

BARCELONA wamechelewa maisha bila Messi

 BADI MCHOMOLO Na MITANDAO 

MAISHA ya timu ya Barcelona kwa asilimia kubwa yalikuwa yanamtegemea nahodha wao Lionel Messi. Amefanya makubwa akiwaongoza wachezaji wenzake ndani ya uwanja pamoja na kwenye vyumba vya kubadilishia nguo. 

Mafanikio ya Barcelona kwa zaidi ya miaka 10 yamechangiwa na mchezaji huyo kwa kuwa amekuwa akijitoa kwa kiasi kikubwa kuhakikisha timu inapata ushindi na inapata mataji na ndio maana ameweza kuwa kinara wa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa Ballon d’Or, akiwa amechukua mara sita na kuwa mchezaji wa kwanza kuchukua mara nyingi akifuatiwa na Cristiano Ronaldo aliyechukua mara tano. 

Messi ana umri wa miaka 33 sasa, kwenye soka ni umri ambao wachezaji wengi viwango vyao vinaanza kushuka kwenye suala la ushindani, lakini Messi ni mchezaji ambaye amebarikiwa kuwa na kipaji cha aina yake, akiwa na umri huo bado ni tishio duniani. 

Siku zote wachezaji ambao wanaangaliwa sana kwa ajili ya miaka mingi ijayo ni wale kuanzia miaka 19 hadi 30, hivyo Messi amepita katika vipindi hivyo na amefanya makubwa ambayo wachezaji wengine duniani hawajaweza kuyafanya. 

Mwaka 2017, wakati Messi anatimiza miaka 30, ulikuwa wakati sahihi wa uongozi wa timu hiyo kumuandaa Messi mwingine ambaye angeweza kuja kuvaa viatu vyake pale anapofikisha miaka 33. 

Wiki mbili zilizopita Messi alitangaza kuwa anataka kuondoka kwenye kikosi hicho wakati huu wa kiangazi, habari ambayo imetikisa dunia na imekuwa ikijadiliwa kila kukicha na vyombo mbalimbali vya habari. 

Kumekuwa na sababu nyingi ambazo zinamfanya mchezaji huyo kutangaza kutaka kuondoka, kati ya hizo ni mwenendo mbaya wa timu, usajili mbovu pamoja na uongozi mbovu. 

Kwenye sula la uongozi, Messi mapema mwaka huu alipishana kauli na aliyekuwa Mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo, Eric Abidal, baada ya kiongozi huyo kusema kuwa, wachezaji wakiongozwa na nahodha wao Lionel Messi hawajitumi uwanjani. 

Kauli hiyo ilimkasilisha sana Messi, ambapo aliamini kitendo cha kuwacha mastaa wengi wakiondoka kwenye kikosi hicho bila ya kusajili wachezaji wenye uwezo wa kwenye kuziba nafasi hizo. Wachezaji ambao waliondoka na walikuwa na mchango mkubwa kwa timu ni pamoja na Neymar, Philippe Coutinho, Xavi Hernandez, Andres Iniesta na wengine. 

Usajili ambao umefanywa na Barcelona kwa miaka ya hivi karibuni hauna faida kubwa kutokana na wachezaji hao kushindwa kuendana na matakwa ya kikosi kama vile Antoine Griezmann ambaye bado hajaonesha kile walichokuwa wanakikusudia. 

Hata hivyo, Barcelona walifanya usajili wa Ousmane Dembele akitokea Borussia Dortmund, lakini tangu ajiunge na kikosi hicho mwaka 2017, amekuwa akipata majeruhi ya mara kwa mara, hivyo mchango wake ni mdogo ndani ya matajiri hao.

Kutokana na hali hiyo, Messi ameona amekuwa akitumia nguvu nyingi kuipigania timu bila ya mafanikio, akatangaza kuwa anataka kuondoka, kauli ambayo inawaumiza mashabiki wa Barcelona huku wakiiangalia timu yao jinsi inavyotaka kuwa endapo ataondoka. 

Baada ya kauli hiyo mashabiki wa Barcelona walijitokeza kwa wingi kwenye viwanja vya Nou Camp na kukesha hapo kwa zaidi ya siku mbili wakishinikiza uongozi ujiuzulu kwa kushindwa kumpa furaha nahodha wao. 

Wengi wanaamini hakuna mchezaji ambaye ataweza kuufikia uwezo wa Messi kwa kipindi cha hivi karibuni, hivyo kuondoka kwake kunaweza kuifanya timu hiyo iwe ya kawaida pale itakapokutana na wapinzani wake. 

Thamani ya Barcelona itashuka kuondoka kwa mchezaji huyo, ushindani wa timu utapungua kwa kiasi kikubwa hata ule mchezo wa wapinzani Real Madrid dhidi ya Barcelona (El Clasico), utakuwa hauna mvuto kama ule ambao ulikuwepo wakati Messi na Ronaldo wanazitumikia timu hizo. 

Ronaldo wakati anakipiga Real Madrid, ushindani wa timu hizo ulikuwa mkubwa kupita maelezo, hapo ndipo kauli ya mtoto hatumwi dukani ilikuwa inatumika, lakini kuondoka kwa Ronaldo kujiunga na Juventus burudani ikaanza kupungua na sasa Messi anataka kuondoa ndio kabisa itakuwa ni bora kuangalia mchezo kati ya Liverpool dhidi ya Manchester City. 

Acha mashabiki wa Barcelona waendelee kuandamana kwenye viwanja vya Camp Nou kwa kuwa hakuna Messi mwingine ambaye atabaki kwenye viwanja hivyo na hakuna mchezaji mwingine ambaye atakuwa na uwezo wa kuipigania timu kwa sasa kama alivyokuwa anafanya yeye. 

 Hii ni kutokana kwamba, viongozi wa Barcelona walishindwa kuwaandaa akina Messi wengine ambao kwa sasa wangekuwa wanafurahia kusikia Messi anaondoka ili wao waweze kuvaa viatu vyake, lakini labda Griezmann ndio mchezaji ambaye moyoni anafurahia Messi kuondoka, lakini usoni anaonekana kuchukia. 

Hii ni kwa sababu, wengi waliamini ujio wa Griezmann ndani ya Barcelona kunakwenda kumrahisishia kazi Messi, lakini bado alishindwa kufanya hivyo na kujikuta akimezwa na kivuli cha staa huyo raia wa nchini Argentina ambaye alimfanya hata Neymar kuondoka kwa ajili ya kwenda kutafuta ufalme nje ye Barcelona. 

Hata hivyo, Barcelona haijazoea kununua sana wachezaji wa bai mbaya sokoni, mara nyingi wamekuwa wakitumia wachezaji kutoka timu yao ya vijana na sasa wanao ambaye anafanya vizuri Ansu Fati, anaweza kuja kuwa bora hapo baadae kutokana na kile anachokifanya sasa, lakini pengo la Messi litakuwa ngumu kuzibwa kama ataondoka wakati huu wa kiangazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles