NAIROBI, KENYA
VIONGOZI wa Chama cha ODM wameitaka Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kuacha kuwaandama wanahabari pamoja na viongozi wadogo badala yake imkabili kinara wa NASA, Raila Odinga.
Hata hivyo, wameonya kitendo chochote cha kumkamata Raila baada ya ‘kuapishwa’ kwake kama rais wa wananchi Jumanne iliyopita kitaifanya nchi iwake moto.
Viongozi hao, ambao walishutumu kukamatwa kwa mwanaharakati wa upinzani, Miguna Miguna, ambaye anajiita jenerali wa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM-K), walielezea kusikitishwa kwao kunyang’anywa walinzi, wakisema serikali itawajibika kwa lolote litakalowakuta.
Viongozi hao walikuwa wakizungumza katika mazishi ya mwanzilishi wa Kanisa la Kimataifa la Sauti ya Wokovu na Uponyaji (VOSH), Askofu Mkuu Silas Owiti (91) katika kijiji cha Tura, eneo la Nyando, Kaunti ya Kisumu.
Viongozi hao walikuwa ni pamoja na Naibu Gavana wa Kisumu, Mathews Owili, Seneta Fred Outa, Seneta Maalum Rose Nyamunga, wabunge Jared Okello (Nyando), Aduma Owuor (Nyakach) na Mbunge Mwanamke wa Kaunti ya Kisumu Rozah Buyu.
Walisema kuwa kwa sasa hakuna kati yao mwenye walinzi na Jubilee lazima iwajibike iwapo lolote litatokea kwao au kwa Odinga.
Outa alimtaka Rais Kenyatta kukubali kuwa Odinga ni rais wa wananchi.
“Waache kuwaandama waandishi wa habari na viongozi wadogo. Wakabiliane na Raila, ambaye ndiye aliyeapishwa,” alisema.
Wakati huo huo, Naibu Rais wa Kenya, William Ruto alimuonya Raila dhidi ya kuunda serikali nyingine na amemtaka aache kuwahadaa wafuasi wake kuwa bado wana nafasi ya kuiunda.
Badala yake Ruto aliwataka NASA kujiandaa kwa kinyang’anyiro cha mwaka 2022, akibashiri kwamba wapinzani watapoteza tena.
Aliwataka vinara wa muungano huo Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Moses Wetang’ula na Musalia Mudavadi kushirikiana na Serikali ya Jubilee kujenga Taifa, akisema wakati wa siasa umeisha.