32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

NAPE NNAUYE, UMESAMEHEWA

KWAKO Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Jimbo la Mtama na Waziri wangu wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Salaam!

Nape, nilianza kukufahamu kwa mbali ulipokuwa kwenye Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).  Nakumbuka jina lako lilivuma wakati wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ulipopambana na Dk. Emmanuel Nchimbi.  Ulipambana, lakini kura hazikutosha.

Niliendelea kulisikia jina lako ulipotaka kugombea Uenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa mara nyingine.  Wakati huo, jina lako lilivuma sana kutokana na figisu figisu zilizokuwa zikiendelea ndani ya chama chako, ili kukuzuia usiwe mgombea wa nafasi hiyo.  Na waliokuwa hawakutaki walifanikiwa azma yao.  Hukuweza kugombea.

Nape, ulipogombana na wenzako ndani ya Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi, hatukujua mwelekeo wako ni upi.  Wakati wa harakati za uchaguzi mkuu, wala hata hukuwa upande wa Jakaya Kikwete alipokuwa akiomba ridhaa ya kuteuliwa na chama chenu kuwa mgombea Urais.  Ulimkataa na uliwafanyia kampeni wagombea wengine.  Aliposhinda, wengi tuliwaza hatima yako ya siasa itakuwa vipi.

Ulikuja kuibuka baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujiuzulu.  Wewe pamoja na akina Mwakyembe na Anna Kilango mlijipambanua kama watu waliokuwa wakipinga ufisadi na hapo ulisikika kweli kweli.  Baadaye, Rais Kikwete alikukumbuka na kukuteua kuwa Mkuu wa Wilaya.  Hatukukaa sawa, ukawa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi…na hapo ndipo dhambi zako zilipoanza.

Nape, yapo mengi uliyoyasema ambayo yaliwakwaza wapenda demokrasia wote nchini.  Sitaki kuyasema mengi leo hii, naomba nitaje machache tu.  Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ulisema maneno mengi sana ya kuudhi.  Kwanza, ulimnenea vibaya aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais kupitia Chadema, Edward Lowassa na kutamka kwamba mgombea huyo anadhani Ikulu ni wodi ya wagonjwa.  Kwa tuliosikia maneno yale, tulisikitika sana na kujiuliza endapo unaujua umri wa mtu uliyekuwa ukimsema.

Lingine ni lile la ‘bao la mkono’.  Sidhani kama yupo yeyote aliyesahau namna ulivyotamka wazi kwamba CCM lazima ishinde kwenye uchaguzi mkuu, hata iwe kwa bao la mkono.  Kauli ile ilitufanya tujiulize maswali mengi, kubwa likiwa kama matokeo tayari yamepangwa na ‘wenye nchi’ sisi tunakaa foleni ya kupiga kura ili iweje?

Ulitukera, ulitukwaza na ulitufanya tuseme mengi.  Ulipoteuliwa na Rais John Magufuli, tulishangaa na kujiuliza kama umelipwa fadhila kutokana na ‘bao la mkono’ na kama ulikuwa ukiistahili kweli nafasi hiyo.

Nape, naomba tu nikiri hadharani kwamba utendaji wako katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, sitakuja kuusahau.  Sikutarajia makubwa kutoka kwako, lakini ulipoishika wizara ile, nikashangaa kuona kwamba kumbe unaweza kuweka siasa pembeni na kuwa mtendaji mzuri. 

Mifano ipo mingi, kuanzia namna ulivyopambana kufanikisha Mbwana Samatta kuachiwa na timu yake huko Kongo ili kumruhusu kuichezea Genk na hata namna ulivyokuwa ukijitahidi kuwa karibu na wanahabari, kuwaomba ushauri na kujibu maswali magumu waliyokuwa wakikurushia.

Nakumbuka kuna wakati ulitangaza kuzifungia redio fulani kwa kutumia ile sheria kandamizi na tulipokuhoji, ulikiri kwamba sheria hiyo si nzuri, lakini unalazimika kuitumia kwa kuwa ipo.  Ulisema vilevile kwamba hatua zinaendelea kufanyika ili sheria ile ifutwe.  Nilikuheshimu.

Nape, wiki moja iliyopita niliposoma taarifa kutoka Ikulu kuhusu mabadiliko madogo kwenye Baraza la Mawaziri, niliumia.  Niliumia kutokana na jina lako kuondolewa katika Wizara ya Habari na niliumia zaidi kuona kwamba uliondolewa kutokana na kutetea uhuru wa habari.  Siku moja baadaye, nilikasirishwa zaidi na zaidi nilipoona umetolewa bastola baada ya kuomba kitambulisho cha aliyedai kuwa askari.  Iliniuma sana.

Nilisema siku ile, kwamba katika siasa unahitaji tukio moja tu la kukufanya ama uwe shujaa au zoba.  Naomba nitamke kwamba ujasiri ulioufanya wiki iliyopita, ghafla umekufanya uwe shujaa.  Ujasiri ulioufanya wiki iliyopita, umesababisha wengi wetu tusahau yale yote uliyoyafanya, yaliyotukera, yaliyotukasirisha, yaliyotufedhehesha.  Ujasiri ulioufanya wiki iliyopiita, umesababisha tukuite shujaa.

Nape Moses Nnauye, kwa sasa umetufanya tukuheshimu na tukulilie.  Sasa basi enenda zako na usitende dhambi tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles