Na JOHANES RESPICHIUS
-DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), amehoji sababu za vyama vya siasa kuendelea kupokea wanachama wa vyama vingine, badala ya kushughulika na Watanzania wasio na vyama.
Akizungumza jana katika mahojiano yaliyorushwa mbashara na Kituo cha Televisheni cha Azam, Nape alisema siku zote amekuwa na msimamo tofauti na wanachama wanaovihama vyama vyao kwa maelezo kuwa unawajenga wanaohama, si vyama.
“Kama tunataka kujenga vyama viwe vya kitaasisi ni lazima kuhamahama lisiwe suala la kawaida. Yaani mtu mpaka anahama watu waseme kweli huyu alistahili kuhama ndiyo maana kwa CCM hutumia gharama kubwa kujenga wanachama wapya kuanzia ngazi ya chini chipukizi.
“Lengo tu ni kuwajenga kiitikadi na nikupe mfano tulikuwa katika maadhimisho ya CCM vijana wa chipukizi wanakuja wanataka wapangwa ili wafanye maonyesho bure na walipokataliwa mtu analia, huko ndiko kujenga itikadi,” alisema Nape.
Alisema Watanzania wapo zaidi ya milioni 50 wenye uwezo wa kujiunga na vyama kikatiba wanaweza kuwa zaidi ya 30 milioni, waliopo kwenye vyama wanaweza wasifike milioni 10.
“Kwa nini tunakwenda kuhangaika na wanachama wa vyama vingine badala ya kushughulika na Watanzania wasio na vyama? Tushughulike kuwashawishi hawa,” alisema.
Nape ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Itikadi na Unezi wa CCM, alisema wakati mfumo wa vyama vingi ulipoaanza CCM ilikuwa na utaratibu licha kutojua uliishia wapi.
“Kwamba mtu akihama lazima akae miaka mitano ya kumwangalia halafu baadae ndio unapewa fursa ya kufanya jambo fulani.
“Katika hali ya kawaida hamahama hii ndiyo inaua vyama, leo hii mgogoro wa Chama cha Wananchi CUF ni kwasababu kuna wakubwa walihama kutoka CCM wakaparamia vyama vya upinzani hivyo namna ya ‘kumanage’ siasa zao.
“Hata CCM ikiendelea kupokea wakishafika huku kwa sababu wapo watu ndani wameteseka miaka mingi halafu mtu ambaye jana alikuwa hawaamini hata tone aliwatukana sana na kuwavuruga anakuja anaambiwa akae pale wewe uliyehangaika unaambiwa kaa kule.
“Tunapoelekea hali hii italeta mgogoro katika vyama vyote na hakuna chama kitabaki salama kama hii hamahama bila taratibu za msingi ikiendelea na ni katika mambo ambayo yameleta aibu kwenye demokrasia yetu,” alisema Nape.
Alisema kuwa hali hiyo haiwezi kuleta tija na kuvitaka vyama vijifunze kuacha kunyang’anyana wanachama badala yake watengeneze watanzania ambao hawana vyama kuwa wanachama wao.
Kuhusu uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 uliofanya Novemba 26 mwaka jana, Nape pamoja na kusema kuwa upinzani haukuwa na hoja madhubuti za kuiangusha CCM alikiri kuwapo kwa vitendo vya matumizi ya nguvu ambavyo wote wanapaswa kuvipinga.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya muda ya uongozi CUF anayetambuliwa na upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, Julius Mtatiro, alisema katika uchaguzi mdogo Serikali ilitumia nguvu kubwa ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kuingia kwenye vituo vya kupiga kura kwa baadhi ya mawaka la uchaguzi upande wa upinzani.
“Dhambi ni dhambu haijalishi imefanyika Ulaya au Afrika, uchaguzi wa kata 43 haukuwa uchaguzi kwasababu unaweza kuhujumu mpizani wako kwa kutumia akili lakini kwa sasa hivi haipo hiyo zamani CCM walikuwa wanaibia kura bila kujua wakati huu imekuwa lazima washinde ili kuonyesha awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli inakubalika sana.
“Tulifanya tathimini kwa zile kata ambazo CCM walijaribu kuiba kura wakashindwa matokeo yake wakaamua kutangaza kwamba zimechukuliwa na wagombea wa chama hicho ni jumla ya kata 12 hicho ndicho kinatufanya kuamini kwamba hakuna uwanja sawa wa upinzani kupambana na chama tawala,” alisema Mtatiro.
Naye mwanahabari mkongwe, Dk. Gideon Shoo waliungana na Nape kukosoa vitendo vya wanachama kuvihama vyama vyao.
Kwa mtazamo wao, hamahama ya wanasiasa ni miongoni mwa kasoro zilizojitokeza mwaka 2017.