24.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAALIM SEIF: VIONGOZI KUBALINI KUKOSOLEWA

Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka viongozi wa siasa, Serikali wanatakiwa kukubali kukosolewa pale wanapokosea na kujirekebisha.

Hayo aliyasema jana wakati akitoa salamu za mwaka mpya ambapo alisema kumezuka malumbano yasiyopendeza kati ya viongozi wa dini mbalimbali na Serikali ambayo haitaki kukosolewa.

Alisema viongozi wa dini kukosoa wanasiasa na Serikali si suala jipya kwani tawala zote zilizopita walikuwa wakitoa maoni yao na kusikilizwa.

Alisema kila mtu anatofautiana katika maono, huku akimtaka Rais Magufuli kusikiliza na kuvumilia na kama kuna kasoro ni wajibu pia wa viongozi wa siasa kujirekebisha kwani kuruhusu maoni ni jambo la msingi.

Alisema viongozi wanapaswa kusikiliza yale ambayo yanakosoa na si kusifia kwani kuna baadhi ya watu alidai wamekuwa wakijipendekeza kwa kusifia kwa sifa ambazo si za kwao.

“Utawala wa awamu ya tano kuna mazuri, na sisi wanasiasa tusione tabu kwa yale mazuri kusema mazuri na wao wasione tabu wakikosea kukosolewa wayachukue na kujirekebisha,’’

“Hata marehemu Samwel  Sitta alikuwa akisema kuwa mwanasiasa lazima awe na ngozi ngumu ya kukwepa mishale na kujirekebisha pale anapokosolewa,’’alisema Maalim Seif.

Katika suala la demokrasia alisema Tanzania kwa sasa imerudi nyuma kutokana na uhuru wa vyama vya siasa kubanwa .

Alisema hakuona sababu yeyote ya raisi kupiga marufuku mikutano ya hadhara kwa maana katika sheria ya vyama vingi moja ya haki za vyama ni kufanya mikutano ya hadhara na maandamano kwa utaratibu uliowekwa.

“Zamani ilikuwa tunatoa taarifa kwa mkuu wa wilaya ikaja Polisi , lakini si kupiga marufuku kwa kufanya hivyo  kumeathiri utendaji wa vyama, kwa maana wanachama wanakusikiliza endapo utakuwa unamwaga sera zako nzuri wakavutiwa nazo wanajiunga pia.

“Pia vyombo vya habari vimefinywa licha ya kwamba Tanzania ina vyombo vingi vya habari ila bado inafika pahala waandishi wana hofu ya kuripoti baadhi ya mambo , huku jambo la kushangaza ni la kupotea kwa waandishi ambapo  mpaka leo hajulikani alipo ili linaharibu utendaji mzuri uliofanywa,” alisema Maalim.

Alisema serikali haitakiwi kuogopa maoni ya wananchi serikali inatakiwa kupokea maoni ya wananchi na kutoa maoni yao ni jambo zuri kusikilizwa pia.

Alisema  watanzania wengi walikuwa na matumaini ya maisha bora kwa mwaka 2017 lakini hali imekwenda kinyume kutokana na maisha kuwa magumu.

Alisema hayo jana wakati anatoa salamu za mwaka mpya kwa watanzania ambao alisema kwa ujumla hali mbaya  si Tanzania Bara pekee bali hata Visiwani .

Alitolea mfano, hasa kwa wafanyabiashara wa mkoa wa  Dar es Salaam, ambao wengi wao wamefunga maduka na mabanda yao ya biashara.

Maalim Seif alisema ni jambo la kushangaza kuona Serikali inatangaza ukuaji wa uchumi kwa asilimia saba huku ukiwa hauendani na maisha halisi ya wananchi wake.

“Takwimu hizo hazimsaidii sana mwananchi kwa kua uchumi unakua kwenye makaratasi tu lakini si kwa wananchi ambao kwa sasa wanahali ngumu kimaisha,’’ alisema

Alizungumzia mapambano ya rushwa kwa serikali ya Tano kwamba imepungua kwa kiasi kikubwa  licha ya kwamba katika maeneo mengine rushwa bado zinaendelea.

“Hatusemi kwamba limemalizika lakini limepungua kwa sasa si rahisi watu kudai rushwa hovyo ingawa sehemu nyingine inaendelea katika hili serikali imeonyesha iko mstari wa mbele ukilinganisha na serikali za awamu  hii imeshughulikia hata  ambao tunawaita mapapa na sio vidagaa,’’ alisema Maalim

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles