24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Nani wa kuiokoa Bongo Muvi?

Elizabeth-Michael-Lulu

Na JOSEPH SHALUWA,

HALI ya soko la filamu nchini ni tete. Hakuna mwenye uthubutu wa kutamba tena hadharani kuwa eti sinema za Kibongo zinalipa (ingawa awali zilikuwa hazilipi sana).

Zinatolewa sababu nyingi; eti mastaa ni walewale, wachanga hawapati nafasi ya kutoka ndiyo maana soko limeshuka. Sababu dhaifu kabisa.

Nani alikuwa anamjua Rose Ndauka kabla ya filamu ya Swahiba? Nani angemjua Irene Uwoya kama asingecheza Diversion Of Love na baadaye Oprah? Je, kiwango cha Wema Sepetu kwenye A Point of No Return kimeshuka? Nani kasema?

Msanii Jenipher Kyaka ni zao la Mussa Banzi katika sinema ya Shumileta na nyingine nyingi, lakini leo ana kampuni yake ya filamu. Ni juhudi zake binafsi.

Ukweli ni kwamba ukiangalia kwa makini utagundua kuwa sinema za zamani zilikuwa zikitoka kwa kupishana na viwango vilikuwa juu. Mfano Filamu ya Shakira ya Ray iliyotoka mwaka 2008 inaweza kufananishwa na filamu gani iliyotoka ndani ya mwezi huu?Hakuna.

Huko nyuma Bongo Fleva walikuwa wanasubiri kwa Bongo Muvi, lakini sasa hivi ni kinyume chake. Ni rahisi kujua wimbo mpya wa Singeli uliotoka kuliko filamu mpya.

Wasanii waliokuwa waking’ara kama Dk. Cheni, Hemed Suleiman, Yusuph Mlela, Thea, Irene Uwoya, Johari, Frank Mwikongi, Aunt Ezekiel na wengineo wako wapi?

Leo hii wasanii walewale waliokimbia tamthiliya za runingani wamezirudia! Nakumbuka mwaka 2007, enzi tamthiliya za runingani zikianza kupoteza mvuto, wasanii wengi walikimbilia kwenye filamu.

Hoja zao kubwa zilikuwa tamthiliya hazilipi zaidi ya kuuza sura – kwamba filamu zinalipa zaidi. Walikuwa na hoja na kweli wengi waliachana na runinga na wengine wakaendelea kupiga kotekote.

Leo hii wasanii walewale wamerudi runingani tena. Hiyo ni dalili tosha kwamba soko la filamu limewashinda. Bahati mbaya kwao ni kwamba, badala ya kutafuta dawa, wameamua kukimbia.

Zipo tamthiliya kadhaa zinaruka kwenye vituo mbalimbali vya runinga, huku wasanii wengine wakubwa wakiendelea kurekodi tamthiliya zaidi kwa lengo la kuzipeleka kwenye vituo vya runinga.

ZAMARADI MKETEMA

Mtangazaji nyota wa Kipindi cha Take One cha Clouds TV, Zamaradi Mketema ni mdau mkubwa wa filamu nchini. Lengo la kuanzisha kipindi chake hicho ilikuwa ni kuwahoji wasanii wa filamu na alikuwa akifanya hivyo.

Lakini siku za hivi karibuni, kutokana na wasanii wetu kupoteza mvuto, anawahoji watu wote maarufu, tofauti na zamani wakati wasanii wa filamu wakiwa wanawika na kukubalika kila kona ya nchi.

Kwanini soko la filamu limedorora ghafla kiasi hiki? Ngoja tuone.

WASAMBAZAJI NI JIPU

Zipo sababu nyingi zinazosababisha kuipeleka Bongo Muvi ‘ICU’ lakini kubwa zaidi ni wasambazaji. Utaratibu na mikataba ya wasambazaji wa filamu siyo mzuri, na hili lilionekana mapema,  nilikuwa miongoni mwa wadau waliotilia shaka wasambazaji wetu  hasa wale wa kutoka nje ya nchi yetu.

Utaratibu wa kulipana kwa filamu siyo sahihi, lakini pia malipo na namna ya kulipana. Msambazaji anapanga bei yeye, anachagua filamu za kununua na wasanii wake anaowapenda na pia analipa kulingana na anavyoamua yeye.

Unapeleka sinema leo hii, utalipwa nusu (kama una jina) nusu nyingine wiki mbili baada ya sinema kuingia mtaani (hata kama ni baada ya mwaka mzima). Maana yake nini? Msanii anajilipa mwenyewe. Halafu bado mali ni ya msambazaji. Ni upuuzi.

Wasanii wasiojulikana ndiyo tatizo zaidi, wao hawalipwi mpaka itakapotoka, tena watalipwa kwa awamu. Figisu hii ikawafanya watayarishaji (ambao wengi ni wasanii wenyewe) kuamua kufanya kila kitu wenyewe.

Atatunga stori yeye, ataigiza, ataongoza na atakuwa meneja wa maeneo. Filamu bora itatokea wapi? Tayari soko limeshaharibiwa na wasambazaji.

Kutokana na wao kufikiria fedha tu bila kujali ubora, filamu mbovu zimeingia sokoni na kuharibu tasnia nzima.

Kama mtu amenunua filamu mara ya kwanza akaona mbovu, akajaribu na ya pili na tatu akakutana na pumba, huku kwenye kava kukiwa na mastaa, atakuwa na sababu gani ya kununua siku nyingine?

BADO WANA NAFASI

Wasanii mnatakiwa kuanza upya; pamoja na kwamba wasambazaji wameshaharibu kwa upande wa bei, lakini mnaweza kuanza kwa kutoa filamu bora. Rudisheni mgawanyo wa majukumu kama zamani.

Muongozaji abaki kwenye nafasi yake, msanii, mtu wa mapambo, maeneo nk. Ikiwa kila mmoja atasimama kwenye nafasi yake, sinema nzuri zitarudi na hapo utakuwa mwanzo wa kuhangaikia soko jingine la uhakika kuliko kuendelea kunyonywa na wasambazaji uchwara!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles