29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

NANI KUINGIA ROBO FAINALI UEFA WIKI HII?

NA BADI MCHOMOLO


TIMU nne wiki hii zinatarajia kuingia hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Ulaya baada miamba nane kuoneshana uwezo.

Wiki iliyopita tuliona historia mpya katika michuano hiyo ya hatua ya 16 bora, huku Barcelona wakionesha maajabu kwenye uwanja wa Camp Nou kwa kuichapa PSG kutoka nchini Ufaransa mabao 6-1 na kufuzu hatua ya robo fainali.

Wachache ambao waliipa Barcelona nafasi ya kufuzu kwa kuwa walikuwa na deni la mabao 5-0 ili kuweza kusonga mbele baada ya mchezo wa kwanza kupoteza kwa mabao 4-0.

Wiki hiyo timu nne ambazo zilifuzu kuingia robo fainali ni Barcelona, Real Madrid, Bayern Munich na Borussia Dortmund.

Wiki hii timu ambazo zinawania kufuzu nafasi hiyo ni pamoja na Leicester City, Sevilla, Juventus, Porto, Monaco, Man City, Atletico Madrid na Bayer Leverkusen, nani kati yao kuingia robo fainali?

Leicester City vs Sevilla

Tangu klabu ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Leicester City imfukuze kocha wao, Claudio Ranieri, Februari 23 mwaka huu, imekuwa ikifanya vizuri michezo yake huku ikiwa na kocha msaidizi, Craig Shakespeare, ambaye amechukua nafasi ya Ranieri kwa muda.

Ranieri alifukuzwa kazi ikiwa ni siku moja mara baada ya kikosi chake kuchezea kichapo cha mabao 2-1 katika mchezo wa hatua ya 16 bora katika michuano ya klabu bingwa Ulaya dhidi ya Sevilla, ambapo marudiano ya mchezo huo yatapigwa kesho.

Leicester City japokuwa walipoteza mchezo wa awali, lakini wana nafasi kubwa ya kuingia robo fainali, wanachokihitaji Leicester ni ushindi wa bao 1-0, ili kusonga mbele kwa bao la ugenini.

Lakini mchezo huo utakuwa mgumu sana kutokana na ubora wa Sevilla, hawatakubali kirahisi kuupoteza mchezo huo, na wao watahakikisha wanapata ushindi wa haina yoyote au sare ya aina yoyote.

Katika Ligi ya nchini Hispania, Sevilla inaonekana kufanya vizuri huku ikishika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi, wakati huo Barcelona na Real Madrid wakiwa nafasi mbili za juu. Kwa upande wa England, Leicester City inashika nafasi ya 15 kabla ya michezo ya mwishoni mwa wiki iliyopita.

Juventus vs Porto

Mchezo wa awali ambao ulipigwa kwenye uwanja wa Porto nchini Ureno, wenyeji hao walikubali kufungwa mabao 2-0, hivyo mchezo wa kesho wana kazi kubwa ya kurudisha mabao hayo na kuongeza moja ili kusonga mbele.

Kama walishindwa kufanya hivyo kwenye uwanja wa nyumbani, basi itakuwa ngumu kwenye uwanja wa ugenini, japokuwa soka ni mchezo wa makosa.

Barcelona waliweza kufanya hivyo kwa kuwa walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani, lakini kama ingekuwa ugenini, ni wazi Barcelona wangeshindwa kusonga mbele.

Juventus, ambao ni vinara wa Ligi Kuu nchini Italia, kazi yao ni ndogo sana kesho kuhakikisha wanasonga mbele, wanachokihitaji ni kutafuta sare au ushindi, kwa kuwa wana akiba ya mabao mawili ambayo yanaweza kuwatia kiburi.

Monaco vs Man City

Huu ni mchezo mwingine ambao utakuwa na mvuto wa aina yake kesho kutwa. Timu hizo zilioneshana ubabe kwenye mchezo wa awali ambapo Man City walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Etihad na kuichapa Monaco mabao 5-3.

Ilikuwa ni idadi kubwa ya mabao kwa klabu hizo, hivyo wiki hii tunatarajia kuona tena ushindani mkubwa kwa washambuliaji.

Man City wanapewa nafasi kubwa ya kusonga hatua ya robo fainali kama wataweza kutumia vizuri nafasi ambazo watazitengeneza, huku walinzi nao wakipambana kutoruhusu bao.

Kazi kubwa ya Monaco katika mchezo huo ni kuhakikisha wanashinda mabao 2-0, ili kusonga mbele, wakati huo Man City wakihitaji sare au ushindi na kama kufungwa basi iwe bao moja bado watakuwa na nafasi ya kusonga mbele kutokana na idadi kubwa ya mabao waliyoshinda nyumbani.

Katika Ligi ya Ufaransa, Monaco ni vinara wa ligi hiyo wakiwaburuza Nice na PSG, ambao wanashika nafasi za pili na tatu, lakini Man City nchini England wakishika nafasi ya tatu kabla ya michezo ya mwishoni mwa wiki iliyopita.

Atletico Madrid vs Bayer 04

Kwa nchini Hispania, Atletico Madrid ni miongoni mwa klabu ambazo zinaogopwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwa na wachezaji wenye uwezo na kocha mwenye mipango mingine uwanjani.

Timu hiyo imepewa nafasi ya kusonga mbele hatua ya robo fainali kutokana na akiba ya mabao waliyoyapata kwenye mchezo wa awali dhidi ya wapinzani wao kutoka nchini Ujerumani, Bayer 04.

Mchezo wa awali ambao ulipigwa nchini Ujerumani, wenyeji Bayer 04 walikubali kufungwa mabao 4-2 mbele ya mashabiki wao.

Ili Bayer iweze kusonga hatua ya robo fainali inahitaji mchezo wa kesho kutwa ugenini ishinde mabao 3-0, lakini kama walishindwa kwenye uwanja wa nyumbani hata ugenini ni rahisi kushindwa.

Kwa upande wa Atletico, wanahitaji ushindi wa aina yoyote, sare na hata wakifungwa bao moja bado nafasi ni ya kwao hatua inayofuata.

Soka ni mchezo wa makosa, lakini kwa idadi kubwa ya mabao ya Atletico, ikiwa pamoja na lile la ugenini ina uhakika wa kuingia robo fainali, lakini chochote kinaweza kutokea na kuishangaza dunia kama ilivyofanya Barcelona kwa PSG.

Tunatarajia kuona ushindani wa hali ya juu wiki hii kwa kuwa kila timu inahitaji kuingia hatua hiyo ya nane bora, nani atafuzu? Majibu yatapatikana wiki hii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles