Na HERIETH FAUSTINE,
NANASI ni moja kati ya matunda yanayopendwa zaidi  kutokana na ladha yake tamu, ambayo inatokana na sukari iliyoko ndani yake. Ladha hiyo hulifanya  kuwa moja kati ya matunda yanayotumika zaidi kwa kutengenezea juisi.
Ni tunda lisilopatikana mara kwa mara kutokana na kuwa la msimu. Wataalamu wa tiba wanasema kuwa tunda hili lina virutubisho mbalimbali ambavyo huwezesha mfumo wa usagaji chakula tumboni kufanya kazi yake ipasavyo.
Pindi mfumo huu unapowezeshwa kufanya kazi yake vizuri, mtu huweza kupata choo laini na kwa wakati kama inavyotakiwa. Hivyo basi, wenye kula tunda hili kwa wingi hawawezi kusumbuliwa na tatizo la ukosefu wa choo.
Nanasi pia linaaminika kuwa miongoni mwa matunda yenye chanzo kizuri cha vitamin C ambayo kazi yake mwilini ni kuupa mwili kinga dhidi ya wavamizi (free radicals), ambao wakiingia mwilini, kazi yao ni kuharibu chembechembe hai za mwili.
Wavamizi hao wanapoweka makazi mwilini, huziba mishipa ya damu na hivyo kusababisha magonjwa ya moyo, saratani ya tumbo na mengine mengi.
Kwa kuongezea, vitamini C inaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili, hivyo kuifanya kuwa kinga ya magonjwa madogo madogo kama vile mafua, kikohozi na homa.
Mbali ya kuwa ni chanzo kizuri cha vitamin C, nanasi pia ni chanzo kizuri cha madini aina ya ‘manganese’ ambayo yanaaminika kuwa na uwezo wa kuboresha ufanisi wa vimeng’enyo mbalimbali vya mwili, vikiwamo vya kuzalisha nishati na kinga ya mwili.
Halikadhalika tunda hili lina kiwango cha kutosha cha vitamin B1 (thiamin).
Licha ya karoti kuwa tunda linalosifika kwa kuwa na uwezo wa kuimarisha nuru ya macho,nanasi pia lina uwezo mkubwa wa kuimarisha nuru ya macho na kuyafanya yaone vizuri hasa nyakati za usiku.
Katika faida kubwa zinazoelezwa na wataalamu mbalimbali duniani, ni uwezo wa tunda hili katika kutunza ama kuboresha uwezo wa ubongo wa mbele ambao unatumika kutunza kumbukumbu.
Ulaji wa nanasi hadi mwisho humpa mlaji faida nyingi ikiwamo kusaidia wagonjwa wenye upungufu wa damu unaoweza kujitokeza kwa sababu kadhaa ikiwamo homa za malaria,typhoid, minyoo na aina nyingine za magonjwa.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa ulaji wa tunda hili na matunda mengine kwa kiasi cha milo mitatu kwa siku tatu, huondoa hatari ya kupungua kwa nuru ya macho asilimia 36 kwa watu wazima.
Hivyo, inapaswa kila ulapo chakula ni muhimu kula tunda lolote ili liweze kusaidia usagaji wa chakula mwilini.