27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

NAMNA YA KUKABILIANA NA HOFU MAISHANI

Na CHRISTIAN BWAYA


NILIPOFIWA na mama yangu miaka kadhaa iliyopita mtazamo wangu wa maisha ulibadilika. Mama hakuwa mgonjwa. Hatukumwuuguza, kifo chake kilitokea ghafla katika wakati ambao familia tulimhitaji. Ombwe la kumkosa mama nililinitengenezea hofu kubwa. Nikawa na maswali mengi yasiyo na majibu: Kwanini Mungu aliamua kumchukua mama yangu katika kipindi ambacho anajua fika ninamhitaji zaidi? Nikajiuliza tena na tena maisha yatakuwaje bila mama?

Tangu nilipopata taarifa za msiba nilianza kukitazama kifo kwa mtazamo tofauti. Nilianza kuwa na wasiwasi nisiouelewa. Ingawa awali nilifahamu kuna kufa kwa kila binadamu na wakati mwingine niliwafariji wenzangu waliokuwa wameondokewa na wapendwa wao, sikuwahi kufikiri kuna siku ingetokea kwangu. Baada ya kuondokewa na mama yangu ufahamu wangu ulianza kukichukulia kifo kwa uzito tofauti. Nilianza kuelewa maana ya kifo na hofu ilinisumbua.

Kwa kipindi cha karibu mwaka mzima baadae, haikuwa inapita siku sijafikiri kuhusu mama. Ingawa hakuna aliyejua kwa hakika kuwa ninawaza nini lakini nilikuwa na mahangaiko ya ndani kwa ndani. Kuna wakati nilijinyima baadhi ya mambo kwa sababu tu ya wasiwasi wa kutokumtendea haki mama. Nakumbuka siku chache kabla ya kifo chake tulikuwa tumezungumza kwamba angehudhuria mahafali yangu. Tuliweka mipango sawa. Tukio la Mungu kumchukua ghafla lilinijaza hofu na kuniondelea msisimko wa kuhitimu. Sikuwa na nguvu wala motisha ya kuendelea na mpango huo.

Hofu ni mkusanyiko wa wasiwasi unaotokana na hisia za kutokutimia kwa makusudio yetu. Unaweza kuwa na matarajio ya kufanya jambo fulani vizuri lakini mazingira yanapobadilika na kuongeza uwezekano wa matarajio hayo kutotimia, unajawa hofu.  Ukiruhusu hali hii ikutawale unaweza kujikuta unajitengenezea mazingira ya kuwa na sonona. Kwa kawaida, hofu hutuondolea ujasiri na hivyo kukutatisha tamaa. Ukishakata tamaa unakosa matumaini ya maisha.

Kwangu hofu ilitokana na kifo cha mpendwa wangu. Kwako inaweza kuwa hofu ya kupoteza kazi. Inawezekana unaenda kazini lakini ndani yako unajua kabisa huna amani. Muda wote kuna mawazo yanakunyemelea yakikukumbusha kuwa si muda mrefu utafutwa kazi. Huna sababu ya msingi lakini hujui kwanini unawaza kuna mtu atakufuta kazi saa yoyote. Unaweza kuitwa na bosi wako kuulizwa kitu cha kawaida kuhusu utendaji wako, lakini kwa sababu tayari una mawazo kuwa yanatafutwa mazingira uondolewe kazini, hata lugha yako inaweza kuwa na matatizo. Utajibu maswali kwa kujitetea, ukijihami, ukilalamika, ukishutumu na tabia nyingine hasi ambazo kweli zinaweza kumfanya bosi wako ahisi una kasoro. Hapa tunaona, wakati mwingine hofu inaweza kutokana na kutojiamini.

Pia hofu inaweza kutokana na mambo kutokwenda kama ulivyotarajia. Umeanzisha biashara na inakwenda vizuri lakini huna amani kabisa. Kichwani ni kama umeweka mkanda unakuimbia kuwa saa yoyote mambo yataanza kwenda mrama. Unapokutana na changamoto fulani fulani ambazo na wafanyabiashara wenzako wanakutana nazo, unajikumbusha, “Si unaona? Kama nilivyokuwa nafikiri. Biashara inajifia hii.” Kumbe ni mawazo yako tu yanakusumbua na yanakufanya utafute ushahidi kuwa unachokiwaza ni kweli.

Unaweza kuwa mwanafunzi unajiandaa na mtihani lakini hupati usingizi kwa sababu kila wakati fikra zako zinakukumbusha kuwa huwezi kufanya vizuri. Ni kama kuna mtu anakuzomea kichwani kwako kuwa huwezi kufanya chochote. Na kwa vile hofu ina nguvu, unaweza kujaribu kusoma, unashangaa kweli haviendi. Unatumia nguvu nyingi kusoma mambo unayoyasahau hata kabla hujayatumia. Tafiti zinasema hofu ya kushindwa mtihani inachangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kushindwa kufanya vizuri mtihani yao. Wazo kwamba wanajiandaa kushindwa mtihani hujenga taswira halisi vichwani mwao inayowanyonya nguvu za kujiandaa ipasavyo.

Wakati mwingine ni mambo uliyowahi kukutana nayo katika maisha. Nina rafiki yangu aliyewahi kunusurika ajali mbaya iliyochukua uhai wa watu aliokuwa nao kwenye gari moja. Bwana huyu hadi leo hatamani kusafiri nje ya mji wake. Kila anapokumbuka yaliyowahi kumtokea, anaomba udhuru asisafiri. Unaweza kupata shida kumwelewa lakini hofu ya namna hii ni kitu halisi kwake. Sasa ni rahisi kumshauri “Acha woga kaka. Mungu alishakunusuru na ajali. Jitahidi kusahau.” Huelewi anachopitia. Ndio maana katika unasihi tunasisitiza kutokukurupuka kutoa ushauri kienyeji kwa sababu hatuelewi hali halisi za wenzetu tunaotaka kuwashauri.

Namfahamu kijana mmoja anayeogopa kuoa. Umri umeenda na haonekani kuwa na mawazo ya kutafuta mwenzi wa maisha. Ukimkumbusha aoe anasitisha uhusiano na wewe. Unaweza kufikiri ana matatizo fulani ya kiafya lakini ukifanikiwa kuelewa unaweza kuhitimisha kuwa, “Ningepitia aliyoyapitia huyu jamaa huenda na mimi ningekuwa na msimamo kama wake.” Tunakuwa wepesi kuwahukumu wenzetu kwa sababu wakati mwingine hatuwaelewi.

Kwa ujumla hofu ipo. Kila mtu ana kiwango chake. Wasiolewa wanaogopa umri unaenda na hawajaolewa, waliooa wanaogopa miaka inaenda na hawajabarikiwa mtoto. Wenye watoto wanaoogopa watakuwaje wakiwa watu wazima. Swali ni je, tunawezaje kukabiliana na hofu? Usikose makala ijayo panapo majaaliwa.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Kwa unasihi wasiliana naye kwa 0754 870 815.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles