22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 11, 2024

Contact us: [email protected]

NAMNA TUNAVYOWEZA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO MPYA ZA MALEZI -2

Wanawake wengi hivi sasa wanatumia muda mwingi kutafuta kipato na kuwa mbali na familia zao.
Wanawake wengi hivi sasa wanatumia muda mwingi kutafuta
kipato na kuwa mbali na familia zao.

Na Christian Bwaya,

KATIKA makala iliyopita tuliona kuwa jamii yetu inapitia mabadiliko makubwa yanayoathiri mfumo uliozoeleka wa malezi. Tulitambua hatua kubwa tuliyopiga kama jamii katika kuhakikisha kuwa akina mama wanakuwa na fursa sawa na wanaume katika soko la ajira.

Hata hivyo, tulidokeza pia kuwa mafanikio hayo ya kujivunia yamekuja na gharama zake. Ingawa ni kweli kuwa jukumu la malezi ni la wazazi wote lakini mama ndiye amekuwa na wajibu mkubwa zaidi. Kwa mfano, jamii ilimtarajia mama kubaki nyumbani aelekeze nguvu zote kwenye malezi ya watoto.

Mwanamume tofauti na mwanamke, hakutarajiwa kutumia muda mwingi nyumbani. Ilifahamika kuwa kwake mwanamume, jukumu kubwa ni kuhakikisha familia inapata kipato cha kutosha kuendesha maisha. Kwa hiyo, kwa kawaida mwanamume alitumia muda mwingi nje ya familia akijua mama yupo nyumbani.

Familia tandao

Hata hivyo, katika baadhi ya makabila ilitokea mwanamke akawa na majukumu ya kufanya kazi zaidi kuliko hata mwanamume. Ingawa mwanamke kwa kawaida hakuwa na ajira rasmi, alitarajiwa kujituma katika shughuli zinazoingiza kipato cha familia. Uwepo wa familia tandao katika mazingira kama haya, ulimwondolea mama hofu ya nani angebaki nyumbani na mwanawe.

Wakati mama akisafiri kwenda kuuza mazao mjini kwa mfano, nyumbani walibaki ndugu waliomwangalia mtoto. Mama hakuwa na wasiwasi na usalama wa mtoto kwa sababu alijua amemwacha mtoto wa baba mkubwa, binamu au shangazi waliomjali mtoto wake kama ndugu.

Haya mawili yalifanya suala la malezi kuwa jambo lisilo na changamoto kubwa. Kwamba baba akiwa kazini, mama alikuwepo nyumbani. Ikitokea mama naye anawajibika kufanya kazi nje na nyumbani ilikuwepo familia tandao kuhakikisha mtoto analelewa ipasavyo.

Hata hivyo, ukaribu wa familia tandao unaendelea kufifia. Imeanza kuwa nadra kuishi na watoto wa ndugu, akina mama nao wameweza kuingia rasmi katika ajira zinazowalazimu kuwa mbali na nyumbani.

Ulazima wa mlezi asiye mama

Katika mazingira ya namna hii, wazazi wanakuwa na changamoto ya kufikiri namna bora ya kuhakikisha mtoto anapata malezi yanayostahili bila kuathiri kazi ya wazazi nje ya familia. Kwa haraka zinakuwepo namna mbili.

Moja, kumtumia mtu mwingine mbali na mama atakayekuwa na jukumu la kumuangalia mtoto. Mtu huyo anaweza kuwa mama asiye ndugu aliyekubaliana na wazazi kukaa na mtoto wakati wa mchana; kuajiri msichana atakayeishi na familia kwa lengo la kumwangalia mtoto; au kupata msaada wa dada mwenye undugu na baba au mama atakayeweza kukaa nyumbani na mtoto.

Mifano hiyo ni ya huduma zisizo rasmi kwa malezi ya mtoto kutokana na ukweli kuwa hazitolewi na watu wenye ujuzi wa malezi na makuzi ya mtoto. Ndizo, hata hivyo zinazotumiwa na wazazi wengi shauri ya unafuu wake.

Pili, ni utaratibu wa kutumia vituo vinavyotoa huduma rasmi ya uangalizi wa watoto kwa makundi. Kwa utaratibu huu mama humkabidhi mwanawe kwa mlezi aghalabu mwenye utaalamu wa makuzi kuanzia asubuhi na humfuata mtoto baada ya saa za kazi.

Malezi ya vituoni yako namna mbalimbali. Kuna ya uangalizi wa mtoto kituoni bila matarajio ya elimu rasmi (day care); shule za awali za kutwa ambapo mtoto hupatiwa malezi na elimu (nursery) na shule za awali na msingi za kulala. Zote hizi tunaweza kuziita huduma rasmi za malezi ya mtoto zitolewazo kwenye vituo vinavyotambuliwa kisheria.

Itaendelea.

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles