Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilala jijini Dar es Salaam, ameishukuru Benki ya NMB kwa kulikumbuka kundi la wafanyabiashara wadogo nchini maarufu wamachinga na kuwasaidia kukua.
Alisema hayo jijini Dar es Salaam leo Machi 17, 2022 katika ofisi za makao makuu ya benki hiyo wakati akipokea kompyuta mpakato (Laptop) tano zilizotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA).
Aidha, baada ya kupokea vifaa hivyo Zungu alizikabidhi kwa viongozi wa SHIUMA kwa ajili ya matumizi ya kiofisi ikiwemo kuweka Kanzi Data, ili iwe rahisi kutambulika na kujua shughuli wanazofanya popote walipo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea na kukabidhi vifaa hivyo, Zungu alisema NMB ndio benki kipekee iliyoonyesha kwa vitendo kujali maisha ya wafanyabiashara wadogo, kwa kuwasaidia mitaji na pia kushiriki katika ukuaji wao.
“Naipongeza benki ya NMB kwa vifaa hivi, hii ni hatua kubwa na mnaonyesha wazi namna mnavyoungana na Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia Wamachinga. Sote tumeona namna Rais Samia alivyofanikiwa kuwaweka Wamachinga daraja la juu, nanyi mnatembelea eneo hilohilo.
“Mbali ya misaada hii pamoja na mikopo mnayowapa wafanyabiashara wadogo, naomba niwakumbushe kuwa mikopo si suluhu ya matatizo bali Wamachinga wanahitaji elimu ya ujasiriamali. Mara kwa mara huwa ninasema kundi la Wamachinga wakiwa milioni moja, kila mmoja akitoa Shilingi 300 kwa siku hiyo ni Sh Mil 300, kwa mwezi ni Sh Bilioni 9. Wanaweza kabisa kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi,” amesema Zungu.
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi NMB, Filbert Mponzi alisema vifaa hivyo ni mwendelezo wa makubaliano waliyoingia kati yao na SHIUMA, lengo ni kutengeneza Kanzi Data itakayowasaidia kujulikana kirahisi na kufikika.
“Tunataka Wamachinga wasajiliwe, wawe rahisi kufikika. Tunashukuru Mheshimiwa Naibu Spika Zungu aliliona hili akaamua kutushirikisha, leo hii tumekabidhi Kompyuta Mpakato tano zenye thamani ya Shilingi Milioni 7.5,” amesema Mponzi.
Alibainisha kuwa pamoja na makabidhiano ya vifaa hivyo, NMB imeendelea kushirikiana na kundi hilo la wafanyabiashara wadogo tangu mwaka 2000. Kwa wastani, benki ya NMB hutoa mikopo ya thamani ya Sh Bil 50 kila mwezi kwa kundi hilo la wafanyabiashara wadogo wakiwemo Wamachinga.
Kwa upande wake Katibu wa Wamachinga Kariakoo, Thabit Maloka aliyemwakilisha Mwenyekiti wa SHIUMA Taifa, alisema wamepata faraja kubwa kwa msaada huo kutoka NMB, wanaamini hayo ni matunda ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na ahadi aliyowapa kuwashika mkono.
“Hatujawahi kuthaminiwa kwa kiwango hiki, tumefarijika sana kwa msaada huu wa vitendea kazi kutoka NMB, kwa sasa Wamachinga tutajuana kwa majina, maeneo na aina ya biashara tunazofanya na hata itakuwa rahisi kupeana ushauri na misaada mingine,” amesema Maloka.
Amebainisha kuwa wanaamini huo ni mwanzo tu, kwani wanajua mazuri yanakuja. Ambapo aliuomba uongozi wa NMB kufikiria kuongeza msaada zaidi ikiwemo kufanya ukarabati wa majengo ya ofisi zao za Ilala jijini Dar es Salaam pamoja na kuwapa mafunzo ya ujasiriamali.
Kompyuta hizo tano zinakwenda kujenga mifumo ya mawasiliano, ufuatiliaji na tathmini katika shughuli za Wamachinga pamojaa na kuwasaidia Wamachinga kuwa na mfumo mzuri wa kufanya biashara zao.