Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Hanan’g, Dk. Mary Nagu (CCM), amesema hajawahi kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Hanan’g, Sarah Msafiri.
Dk. Nagu, alitoa ufafanuzi huo, baada ya gazeti hili katika toleo lake la Julai 19, mwaka huu kuandika habari za kukamatwa kwake kwa agizo la DC Msafiri, muda mfupi baada ya kuwapo vurugu katika kikao cha Kamati ya Siasa cha Wilaya.
‘Nimelazimika kuja ofisini kwenu kutoa ufafanuzi na kukanusha taarifa kwamba, nilikamatwa kwa agizo la mkuu wa wilaya.
“Nakumbuka siku hiyo, tulikuwa na kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya kulitokea kutoelewana kwa wajumbe juu ya kanuni zetu za vikao jambo ambalo kwa kweli likasababisha mkutano uvunjike,” alisema.
Nagu, mmoja wa wanasiasa wakongwe na aliyekuwa waziri mwandamizi mfululizo katika serikali za awamu ya tatu na nne, alisema alikwenda polisi ili kutoa maelezo ya kile kilichotokea ndani ya kikao hicho.
Wakati Nagu akitoa ufafanuzi huo, taarifa ambazo gazeti hili lilizipata siku ya tukio hilo zinaeleza kuwa mbunge huyo alikwenda polisi kwa maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya.
Uamuzi wa DC Msafiri ulitokana kuibuka kwa vurugu katika kikao hicho ambazo zilianza wakati wa kujadili ajenda ya uchaguzi.
Akizungumzia suala hilo siku ya tukio, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Massawe alikiri Dk. Nagu na wajumbe wenzake kuitwa na kuhojiwa katika kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano, kwa maelekezo ya Mkuu wa Wilaya.
Gazeti hili lilimkariri RPC Massawe akisema;
“Kweli wote wanashikiliwa kitu cha polisi Katesh kwa ajili ya kutoa maelezo yao, tunawahoji kujua tatizo ni nini, walikuwa wanajadili nini na nani aliyesababisha hali hiyo,” alisema.
UFAFANUZI WA DK. NAGU
Akitoa ufafanuzi wa tukio hilo, Dk. Nagu alikiri kushikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano.
“Baada ya zile vurugu kutokea tulipelekwa polisi Katesh, sikuwekwa ndani ndugu zangu…bali nilikaa ofisini kwa OCS kama dakika 20 hivi, halafu nikaondoka,” alisema.
Alisema yeye na wenzake walichukuliwa maelezo kwa nia ya kujua nini kilichotokea ndani ya kikao hicho.
MASHAMBA YA NAFCO
Kuhusu mashamba hayo, Dk. Nagu alisema hawajawahi kushiriki kwa namna yoyote ile katika suala la kuwagawia wananchi au wafanyabishara wa aina yoyote tofauti na ilivyodaiwa katika habari hiyo.
“Mimi sihusiki hata kidogo na suala la mashamba ya NAFCO na katika maisha yangu sijawahi kuhusika katika kugawa mashamba hayo kwa mtu yoyote au mfanyabishara wa nje ya Hanan’g.
“Ninapenda kuueleza umma mimi sijui lolote na hata katika kikao cha CCM ambacho pia na DC alikuwapo suala la mashamba halikuwa moja ya ajenda.
“Kwangu siku zote hujadili maendeleo ya wilaya yetu na si jambo lingine. Ila kwa kilichotokea ndani ya kikao Katibu au Mwenyekiti wa CCM ndiyo wanatakiwa kulisemea si mimi,” alisema Dk. Nagu.
Gazeti la MTANZANIA, linamuomba radhi Mbunge Nagu kutokana na upungufu au makosa ya kiuandishi yaliyojitokeza katika habari hiyo ambayo kwa namna moja au nyingine ilimsababishia usumbufu.
MHARIRI