Na Faraja Masinde, Mbeya
Wazazi na Walezi nchini wametakiwa kubadilika na kuwalea watoto katika misingi itakayowasaidia kufanyakazi na kujitegemea ili kuepukana na mambo yasiyofaa yanayowasababisha kutumbukia kwenye maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI.
Wito huo umetolewa leo jijini Mbeya Novemba 29, 2021 na Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI nchini (NACOPOHA), Leticia Mourice, wakati wa Mdahalo wa Viongozi wa Dini na Vijana kuhusu UKIMWI.
Amesema kuyumba kwa malezi bora kutoka kwa wazizi na walezi ndiyo imekuwa sababu ya vijana wengi kukosa mwelekeo na matokeo yake kuwa mzigo kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla.
“Pamoja na kazi kubwa ambayo imekuwa ikifanywa na serikali katika kukabiliana na Virusi Vya UKIMWI, lakini bado takwimu zinaonyesha kuwa changamoto ni kubwa upande wa vijana hususan wa kike.
“Katika hili naomba nitoe wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha kuwa wanatilia mkazo suala hili la malezi, tubadilike tuwalee vijana wetum katika misingi ya kufanya kazi ili waweze kuepukana na mambo ya ovyo ysiyokuwa ya lazima kwa namna moja ama nyingine.
“Kwani tukifanya uzembe tukakubali kuwalea kilelemama utakuwa mzigo kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla,” amesema Leticia.
Tahadhari kwa Wasichana.
Aidha, katikia hatua nyuingine, Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wasichana nchini juu ya kujiepusha na vishawishi kutoka kwa wanaume ambao wamekuwa wakiwalaghaina kisha kuwakiimbia huku wakiwa tayari wamewaachia maambukizi ya VVU.
“Pamoja na kupambana lakini naomba niwambie vijana wangu kwamba kama mnavyofahamu takiwmu za maambukizi ziko juu hasa kwa vijana wa kike, hii ina maananisha kwamba mnafanya ngono isiyo salama, nataka niwaambie vijana wangu wa kike, nikweli kabisa tunatambua kuwa kufanya mapenzi ni haki ya msingi lakini inategemea ni lini, wapi na nani, hivyo naomba niwaambie vijana wangu wa kike, hawa wanaume hawa siyo… siyo kabisa siyo… wanaume hawa ni wataalamu sana wa kuchana mistari (kulaghai) katika habari ya mahaba.
“Wanajua mpaka kunena kwa lugha… kwa hiyo mimi naomba niwaambie vijana wangu msiwape kabisa ushirikiano na wala nafasi ya kujieleza, wao ni wataalumu sana tena ukijichanganya ukasema ‘nina soma kidato cha tatu’, atakwambia ‘mama somo gumu pale ni Hesabu mimi linasafiri kwenye mishipa ya damu nitakufundisha’, lakini mafundisho yake utabaki na ningali ningeli.
“Kwa hiyo mabinti naomba msimame katika roho na kweli ili muweze kutimiza ndoto zenu, na ninyi vijana wa kiume hebu badilikeni, hii habari ya kujifanya mnajua kuchana mistari hadi kwa mama watu wazima tuliokula chumvi mpaka sukari muache.
“Nasema muache sababu najua mnakwenda huko kwa ajili ya kutafuta unafuu wa maisha na mkisha wapata wamama hao wenye umri mkubwa wakakununulia jinsi, wakakupeleka saluni unasema umefika Jerusalem…hujafika ni mahangaiko naomba msimame katika kweli na mbadilike haya mambo yapo tu,” amesema Leticia.
Wito kwa Viongozi wa Dini.
Akizungumza kuhusu Viongozi wa dini, Leticia amewaomba kuendelea kuelimisha jamii ya Watanzania katikia kutoa elimu sahihi kiuhusu VVU na UKIMWI pamoja na mengine yote yanayohusiana na hayo.
“Leo nisiku njema kabisa ambayo tunabadilisha uzoefu na viongozi wa dini katika kupambana na virusi vya UKIMWI hapa nchini, kwani tunatambua uwepo wao katika kupambana jambo hili.
“Tunawaomba sana viongozi wetu wa dini muendelee kuelimisha jamii ya Watanzania katika kutoa elimu sahihi kuhusu VVU na UKIMWI pamoja na mengine yote yanayohusiana na hayo. Muendelee pia kututia nguvu na kutuombea ili dawa hizi tunazozitumia zitufae vyema na si vinginevyo,” amesema Leticia.
Mdahalo huo ulioandaliwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) ukihusisha Viongozi wa Dini na Vijana ambao ni sehemu ya Maadhimisho ya UKIMWI duniani ambayo Kitaifa yatafanyika jijini Mbeya Desemba Mosi yakiwa na Kauli mbiu ya “Zingatia Usawa, Tokomeza UKIMWI, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko”.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, yatakayiifanyika katika viwanja vya Ruandanzovwe.