WASHINGTON DC, Marekani
BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema linatatizwa na ghasia zilizotokea hivi karibuni kati ya Israel na Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Mapigano makali kuwahi kutokea katika miaka mine yaliibuka Jumapili iliyopita baada wa wapiganaji wa Hamas kuingilia kati operesheni za siri zilizokuwa zikifanywa na Israel katika ukanda huo wa Gaza.
Chama cha Wapalestina cha Hamas kimesema kinachunguza kama Israel imezingatia makubaliano ya Misri ya kusimamisha mapigano.
Israel nayo inasema itaendelea na mashambulio yake ya anga katika ukanda wa Gaza ikiwa ni lazima kufanya hivyo.
Balozi wa Israel Umoja wa Mataifa, Danny Danon amesema nchi yake kila siku inafanya kila iliwezalo kuhakikisha usalama wa watu wake.
”Tunachukua hatua kuwalinda watu wetu. Na wakati unapojua kwamba kuna mtu anachimba njia ya chini ya ardhi ama kuna mtu anapanga mashambulio ama tukio la utekaji, utachukua hatua za kujilinda,”alisema balozi huyo.
Katika mapigano hayo Wapalestina sita waliuawa na mashambulio yaliyofanywa na Israel, huku roketi zilizorushwa na wapiganaji wa Hamas zikiua muisrael mmoja.