Na CHRISTIAN BWAYA
HAKUNA mwanadamu anayependa hofu. Hofu inaumiza, inaondoa amani na inanyonya nguvu za kufanya vitu unavyovipenda.
Kuna nyakati maisha hukutanisha watu mazingira yanayojaza hofu. Matukio mabaya yaliyowahi kukukuta, kutotimiza matarajio uliyonayo katika maisha. Simulizi unazozisikia kwa watu wanaokuzunguka, vyote hivyo kwa pamoja vinaweza kuwa chanzo cha hofu.
Kama nilivyoahidi, makala haya yanaangazia mbinu unazoweza kutumia kukabiliana na hofu maishani.
Jambo la kwanza la kuelewa ni ukweli kwamba mzizi mkubwa wa hofu ni fikra. Hofu, kama zilivyo hisia nyingine, ni zao la kile unachokifikiri. Hisia ulizonazo, iwe furaha au huzuni, upendo au chuki, zimevutwa na sumaku tunayoiita fikra. Kile unachofikiri kinatengeneza hisia unazokuwa nazo. Ni sawa na simu yako ya kiganjani inavyofanya kazi. Kile unachoingiza kwenye simu yako ndicho utakachokipata ukikihitaji baadae.
Huwezi kutafuta jina la mtu ambaye hukuwahi kumhifadhi kwenye simu yako. Lazima uwe umeingiza namba zake na kuzitunza kwa jina unalolifahamu ili baadae ukimtafuta au yeye akikupigia, simu yako imtambue. Ikitokea umepigiwa simu na mtu ambaye namba zake hukuwa umezitunza awali, tunafahamu kuwa simu yako haitamtambua. Simu hukupa kile ulichokiweka. Ndivyo ufahamu wetu unavyofanya kazi. Ukiingiza wazo hasi, lazima upate hisia hasi. Ukiingiza wazo chanya utapata hisia chanya.
Kwa uelewa huo, maana yake ni kwamba unapokuwa na hofu fulani, kuna mambo ambayo wewe bila kujua umeyaruhusu kutengenezea mazingira hasi. Kwa sababu, kile unachokifikiri ndicho utakachojisikia. Haijalishi unawaza mawazo chanya au hasi, kile unachokiingiza kwenye ufahamu wako ndicho utakachokipata. Maana yake ni kwamba unaweza kubadili maisha yako kwa kubadili fikra zako. Ukitaka kuwa na hisia njema, unahitaji kubadili mawazo yako.
Jambo la pili la kuzingatia ni kwamba fikra zako ni mkusanyiko wa maneno unayoyasikia kichwani mwako na yale unayoyatamka kwa sauti. Unapomwambia mtu: “Siku yangu imekuwa mbaya.” Maana yake hicho ndicho ulichokifikiria awali na ndicho ulichokisema. Mawazo yako yamezalisha matamshi. Na kwa kawaida, kitendo chochote unachokifanya, kinategemea kile unachokifikiria. Kila unachokifanya kimeanzia kwenye fikra zako. Mawazo yako ndiyo yanayoamua ikiwa maneno utakayotamka na vitu utakavyovifanya vitakuwa chanya au hasi. Swali linaweza kuwa utajuaje basi ikiwa mawazo yako ni chanya au hasi? Mawazo yako yanakuwa chanya ikiwa unachokifikiria ni kile unachokipenda. Kwa upande mwingine, mawazo yako yatakuwa hasi ikiwa unafikiri kile usichokipenda.
Nitakupa mfano rahisi. Unapofikiria kuhusu ugumu wa jambo, maana yake hapo unafikiri kitu usichokipenda kwa sababu, kwa kawaida, hatupendi mambo yawe magumu. Katika mazingira kama haya, tunaweza kusema, umejawa mawazo hasi. Chukulia unasema: “Nitashindwa mtihani.” Hapo ina maana unafikiri kitu usichokipenda na hivyo tunaweza kusema umejaza ufahamu wako mawazo hasi. Unaposema: “Sitapona nikisafiri.” Hapo unakuwa na fikra hasi kwa sababu tunajua ungependa kupona.
Hebu fikiria unawaza mambo unayotaka yakutokee katika maisha. Unajisikiaje? Chukulia kwa mfano unawaza, “Nitafanikiwa maishani,” “Nitafanya vizuri mtihani wangu,” “Wanangu watafanikiwa masomoni.” “Mwaka huu utakuwa mzuri.” Mawazo kama haya ni chanya kwa sababu hayo unayoyafikiri ndiyo unayotamani yatokee.
Lakini katika hali ya kawaida, watu wengi wanapenda kufikiri na kuzungumzia mambo wasiyoyapenda. Unakuta watu wanazungumzia namna mwaka utakavyokuwa mbaya, namna ‘vyuma vilivyokaza’, namna biashara zinavyofungwa, soko la ajira lilivyo gumu, vile ajali zilivyoongezeka, na bado watu hawa wanashangaa inakuwaje mioyo yao imejawa hofu kila wakati. Kanuni hapa ni rahisi: Kile unachokipa nafasi kwenye ufahamu wako, kile unachokipa nafasi kwenye mazungumzo yako, ndicho kitakachozalisha hisia hasi au chanya.
Maana yangu ni kwamba, unapokuwa mtu wa kufikiri na kuzungumzia mambo usiyoyapenda, mambo yanayokutisha, mambo yanayokuumiza, mambo yanayokuondolea furaha, hapo unakuwa unashiriki kazi ya kukaribisha hofu yako mwenyewe. Ukitaka kuanza safari ya kushughulikia hofu inayokusumbua, hatua ya kwanza kabisa ya kuchukua ni kudhibiti fikra zako. Anza kuzungumzia mambo mazuri hata kwa kujilazimisha. Zungumza kama mtu mwenye ujasiri hata kama ni kweli umejawa hofu. Usikubali kunyong’onyea kwa sababu tu unajua una wasiwasi.
Maana yake ni kwamba badala ya kuzungumzia namna gani una wasiwasi na maisha, anza kuzungumza kama mtu mwenye uhakika na maisha. Badala ya kuzungumzia uwezekano wa kufukuzwa kazi, anza kuongea kama mtu unayejiamini na kazi. Badala ya kuongelea matukio ya vifo, magonjwa, ajali, maadui, anza kuongelea mambo chanya hata kama huyaoni kwenye maisha yako. Ongelea afya njema hata kama unaumwa. Zungumzia watu unaowapenda badala ya watu usiowapenda. Ukifanya hivi mara kwa mara, uwezekano wa kuondokana na hofu inayokusumbua itaanza kukuacha.
ITAENDELEA
Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Kwa unasihi wasiliana naye kwa 0754 870 815.