28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mzee wa miaka 73 adaiwa kubaka, kumpa ujauzito mwanafunzi

Na JANETH MUSHI -ARUSHA



Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, linamshikilia mzee mmoja David Nnko(73), mkazi wa Kijiji cha Sakila Juu Kata ya Kikatiti, kwa tuhuma za kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la sita (jina linahifadhiwa), mwenye umri wa miaka 14.

Aidha kutokana na matukio ya ubakaji na mimba kwa wanafunzi wilayani Arumeru, kamati maalum ya wataalamu imeundwa itakayokuwa ikisikiliza mashauri yanayohusiana na matukio hayo ili kukabiliana nayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake,Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, amesema matukio ya ubakaji na mimba kwa wanafunzi yamekithiri ambapo katika kipindi cha miaka miwili takwimu zinaonyesha wanafunzi 84 wa Shule za Msingi na Sekondari, wamekatisha masomo baada ya kupata ujauzito.

Alisema kutokana na vitendo hivyo kukithiri, kamati maalum itakayoanza kazi jumanne wiki ijayo ambayo itaongozwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Mwalimu James Nchembe, kwa kushirikiana na Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya jamii, Jeshi la Polisi pamoja na Mahakama, watashirikiana katika usikilizaji wa mashauri hayo na kuyafikisha katika vyombo vya sheria.

“Tunalaani na kukemea vitendo hivi,kwani kumekuwa na baadhi ya watu wazima wanaojihusisha na vitendo hivyo kwa sababu ya imani za kishirikina au tamaa za kingono, kuanzia wiki ijayo tutaunda kamati ya pamoja na tutapokea malalamiko ya watu wote wakiwemo wanafunzi waliowahi kubakwa au kupewa mimba.

“Kamati itahusika na mashauri ambayo yamekwama katika ngazi za watendaji wa chini,polisi au mahakamani hivyo tutaomba wazazi na walezi kama wana vielelezo waje navyo, serikali haiwezi kuvumilia matukio hayo kila kukicha,” amesema.

Akizungumzia tukio la mzee huyo kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi huyo ambaye ni ndugu yake, alidai kuwa walipata taarifa za mshitakiwa huyo kumrubuni mwanafunzi huyo kwa kumuomba amsaidie kupukuchua mahindi debe moja na na kumpa sadolini moja kama ujira wa kazi hiyo kisha kumvuta ndani na kumbaka kwa nyakati mbili tofauti.

Alisema ili kukomesha wahusika wa vitendo hivyo, watawaweka hadharani watuhumiwa wote watakaobainika ili jamii iwafahamu.

“Tutaendelea kufichua wabakaji kwenye vyombo vya habari ili familia na jamii nzima ijue na tutavalia njuga suala hili hadi liishe,kwani wanafunzi wanakosa haki zao za msingi za kusoma kwa kukatishwa masomo, lengo la haya yote ni jamii ibadilike,” amesema.

Akizungumza mbele ya waandishi hao Mzee huyo alidai kutofahamu lolote juu ya suala la mtoto huyo na kuongeza kuwa huyo ni sawa na mtoto wake.

“Wananisingizia kwani huyu mtoto ni sawa na wa kwangu, hata mara kwa mara mama yake amekuwa akimtuma huku kwangu kuja kuchuma mboga shambani na kwa kuwa sisi ni familia moja tunashirikiana mambo mbalimbali,” alidai na kuongeza

“Baba wa binti huyu ni mdogo wangu katika ukoo wetu wa Nnko, na hili jambo limesukwa na mama wa mtoto kwani nilishangaa nakamatwa tu na polisi na katika familia zetu hakuna ugomvi wowote sielewi kwa nini wamenisingizia,”

“Nilipovuna mahindi ya vuli ya mwaka jana, mwezi wa tisa mwaka huu, nilimpa mtoto kibarua cha kuja kupukuchua mahindi debe mbili na alipomaliza nilimpa ujira wake wa sadolini mbili za mahindi kama tulivyokubaliana na nakumbuka haikuwa siku ya shule,” amesema.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Kikatiti Hamida Mnyenyelwa alisema alipata taarifa shuleni kwa mwanafunzi huyo kuhusu utoro wake na walianza kumfuatilia kwa kushirikiana na walimu shuleni hapo,kabla ya kubaini kuwa ni mjamzito wa wiki nane.

“Mtoto alikuwa mtoro, tukashirikiana na walimu lakini tukawa hatumuelewi ndipo alipoenda kupimwa na kukutwa mjamzito, ambapo alidai mzee huyo amewahi kumuingilia kimwili mara mbili kwa nyakati tofauti,” amesema.

Naye mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Flora Nnko, alidai alikuwa na mazoea ya kumtuma kwenda kuchuma mboga shambani kwa shemeji yake (mtuhumiwa) na wakati mwingine alikuwa akimuomba mtoto akamsaidie kupukuchua mahindi.

“Huyu mzee ni shemeji yangu, mke wake alishafariki hivyo tunashirikiana katika masuala mbalimbali, nakumbuka Jumapili moja aliniomba mtoto akamsaidie kupukuchua mahindi, mimi nikaenda kanisani na niliporudi baadaye jioni mtoto alikuja na mahindi sadolini mbili.

“Mwezi wa tisa mwishoni mtoto alianza kuumwa baba yake akampeleka hospitali na alipopimwa aligundulika ana ujauzito wa wiki nane, tulimbembeleza sana mtoto amtaje aliyempa mimba hakutaka lakini baadaye alimtaja mzee Nnko na ameshafanya naye mapenzi mara mbili,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles