31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Maofisa 63 wa usalama, jeshi watiwa mbaroni Ethiopia

MOGADISHU, SOMALI



MAMLAKA za hapa zimesema zimewakamata jumla ya maofisa 63 kutoka idara zake za upelelezi na jeshi, pamoja na wafanyabiashara kadhaa kwa madai ya rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Taarifa zilizopatikana mjini hapa zinaeleza miongoni mwa waliokamatwa ni mkuu wa zamani wa kampuni kubwa ya kijeshi ya uhandisi na utengenezaji chuma ya  Metec.

Kukamatwa kwa maofisa hao wa ngazi ya juu ni matokeo ya uchunguzi wa miezi mitano ulioagizwa na kiongozi wa taifa hilo la Mashariki mwa Afrika anayelenga kuleta mageuzi, Abiy Ahmed.

Mwanasheria Mkuu, Berhanu Tsegaye aliwaambia waandishi wa habari juzi kwamba jumla ya watu 36 walikamatwa kutokana na kushiriki kwenye ukiukwaji wa haki za binadamu, huku wengine 27 wakikamatwa kwa madai ya rushwa.

Madai hayo ya ukiukwaji wa haki za binadamu yalisababisha uonevu dhidi ya wafungwa wa kisiasa, ikiwemo kukamatwa isivyo halali, kupigwa, ubakaji na hata mauaji.

Mwanasheria huyo aliyaelezea matukio ya uhalifu, upendeleo na rushwa, ikiwemo uporaji katika kampuni kubwa ya kijeshi ya utengenezaji chuma na uhandisi ya Metec, inayozalisha vifaa vya kijeshi na bidhaa nyingine za kiraia.

“Mikataba ilifanyika kupitia mitandao ya familia na washirika. Matokeo yake nchi imepata hasara kubwa,” alisema Tsegaye.

Mapema wiki hii Mwanasheria Mkuu wa zamani wa kampuni hiyo ya kijeshi, Kinfe Dagnew ambaye ni meja jenerali katika jeshi la hapa,  alikamatwa karibu na mji wa kaskazini magharibi wa Humera, ambao upo karibu na mpaka wa Sudan na Eritrea.

Kwa mujibu wa mwanasheria mkuu, uchunguzi uliofanywa umebaini kampuni hiyo ilifanya manunuzi ya kimataifa yanayofikia Dola za Marekani bilioni 2 bila kufuata michakato ya zabuni.

Kwa miongo kadhaa kampuni hiyo ya Metec imekuwa kiungo muhimu katika uchumi uliodhibitiwa na taifa na jeshi.

Maofisa wa juu wa kampuni hiyo inayotengeneza vifaa vya kijeshi na kujihusisha na sekta nyinginezo kama vile kilimo na ujenzi wengi ni maofisa jeshi.

Kukamatwa huko kwa maofisa ni hatua mojawapo ya waziri mkuu mpya, Abiy aliyeingia madarakani baada ya mtangulizi wake kun’gatuka katikati mwa maandamano makubwa ya kuipinga Serikali.

Abiy anaonekana kuwa na dhamira ya kuleta mageuzi na demokrasia nchini hapa.

Hadi sasa amewaachia huru wafungwa wengi wa kisiasa na kuyaondolea marufuku makundi ya upinzani ambayo wakati mmoja yalitangazwa kuwa mashirika ya kigaidi.

Pia ameweza kurejesha upya mahusiano ya kidiplomasia na hasimu wake wa muda mrefu Eritrea mapema mwaka huu na kukomesha rasmi vita ya mpaka ambayo iliwaua makumi kwa maelfu ya raia kati ya mwaka 1998 na 2000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles