29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mzee Moyo: Sijutii kufukuzwa CCM

hassan-nassor-moyoNa Is-haka Omar, Zanzibar
WAZIRI wa zamani wa Mambo ya Ndani mstaafu, Mzee Nassor Moyo, amesema hajutii kufukuzwa uanachama ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hatarajii kukata rufaa.
Akizungumza na MTANZANIA mjini hapa jana, Moyo alisema ataendelea kuwa muumini wa Serikali tatu na kudai mamlaka kamili ya Zanzibar hadi mwisho wa maisha yake.
Alisema anaamini kile anachosimamia ndani ya moyo wake, hivyo hakuna chama wala taasisi yoyote yenye uwezo wa kubadilisha kile anachokiamini kusimamia masilahi ya wananchi wa visiwa vya Zanzibar.
“Naamini ninachofanya na kusimamia siyo dhambi wala usaliti kama baadhi ya wanachama wa CCM wanavyoamini, bali napigania uhuru, usawa wa watu na mapambano haya ni endelevu,” alisema.
Moyo ambaye amekuwa mtumishi wa umma ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa muda mrefu, alisema anatambua mambo mengi ambayo yamefanyika, lakini sasa anashangaa kuona vijana wengi wanajifanya wanajua mambo ya CCM kuliko wazee.
Alipoulizwa kuhusu ukweli juu ya tuhuma zinazomkabili, alisema safari ya kupigania haki na usawa katika maisha ya wanadamu haiwezi kukosa vikwazo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi, Yussuf Mohamed Yussuf, alikiri Moyo kuvuliwa uanachama na Halmashauri Kuu ya Mkoa huo juzi.
Alisema CCM imetumia busara na hekima nyingi kufuatilia mwenendo wa mwanachama huyo kwa miaka minne baada ya kupokea tuhuma mbalimbali za kukiuka maadili ya chama.
Yussuf alisema miongozi mwa makosa makubwa aliyofanya Moyo, ni kusimama katika majukwaa ya Chama cha Wananchi (CUF) na kudai yeye ni muumini wa Serikali tatu, mfuasi wa kudai mamlaka kamili ya Zanzibar na kujiita mjumbe wa CCM katika Kamati ya Maridhiano ambayo chama chenyewe hakikuhusishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles