27.4 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

Kura ya maoni, uchaguzi mkuu viko njia panda

Jaji LubuvaNa Fredy Azzah, Dar es Salaam
KUTOKANA na kusuasua kwa uandikishaji wapigakura katika daftari la kudumu, baadhi ya wadau wamekuwa wakisema kuna uwezekano mkubwa Uchaguzi Mkuu ukasogezwa mbele kama ilivyofanyika kwa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, amelieleza gazeti hili jana kuwa Uchaguzi Mkuu hautasogezwa mbele bali utafanyika kwa mujibu wa Katiba Oktoba, mwaka huu.
Alisema kufikia muda huo uandikishaji katika daftari hilo kwa kutumia mashine za kielektroniki ((Biometric Voter Registration – BVR) utakuwa umekamilika nchi nzima.
Moja ya vitu vinavyofanya wadau kupata wasiwasi endapo uandikishaji utakamilika kwa muda, ni ukweli kuwa mashine 8,000 zinazotarajiwa kutumika kuandikisha wapigakura na muda uliobaki ni chache zikilinganishwa na zilizotumika kwenye nchi zilizowahi kutumia teknolojia hiyo.

KENYA
Mathalani Kenya mwaka 2013 ilitumia mashine 15,000 kuandikisha wapigakura 14,352,545.
Tume ya Uchaguzi ya Kenya ilikuwa na vituo 25,000 vya kuandikisha wapigakura, ilikuwa pia na watumishi 30,000 walioajiriwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Kutokana na maandalizi mazuri, nchi hiyo ilikuwa na vifaa pamoja na watumishi wa kutosha ambao walifanya kazi kwa siku 30 baada ya maandalizi ya miezi sita ya elimu ya namna ya kutumia vifaa hivyo vya kisasa.
Kenya pia ilitumia muda mrefu kujiandaa, kwani zoezi hilo lilianza mwaka 2009 kwa vituo vya majaribio vilivyohusisha majimbo 18 nchi nzima ilihali Tanzania majario yalianza mapema mwaka huu kwenye majimbo matatu tu.
Mwaka 2012 nchi hiyo ilifanya majaribio mengine kwenye majimbo 209.
NIGERIA
Uzoefu mwingine ni nchi ya Nigeria, ambayo ilitumia mashine 132,000 kuandikisha wapigakura wake.
Nigeria ambayo ni taifa lenye watu wengi zaidi Afrika, ilitumia idadi hiyo ya mashine kusajili wapigakura milioni 76 ndani ya wiki tatu.
Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo pia iliajiri watu 300,000 kwa ajili ya kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa wakati na kupata matokeo mazuri.
Nigeria ambayo ilitumia uzoefu wa Kenya kufanya shughuli hiyo, iliingiza teknolojia rahisi kwenye mfumo huo ili uweze kuendana na hali za taifa hilo.
Muda ambao mataifa hayo yalitumia kuanzia kwenye majaribio ni zaidi ya miaka mitatu.

JAJI LUBUVA
Akizungumzia changamoto hiyo jana, Jaji Lubuva alisema uandikishaji wapigakura kwenye dafatari la kudumu, ungepaswa kuanza muda mrefu, lakini ilishindikana kutokana na ukosefu wa fedha.
Hadi sasa NEC haina idadi kamili ya watumishi inaotarajia kuwatumia katika kazi hiyo zaidi ya kutegemea wakurugenzi wa halmashauri wawapatie watu wanaojua mambo ya Tehama (IT), walimu ambao watapewa mafunzo ya muda mfupi ili kuweza kufanya kazi hiyo.
“Siwezi kusema watu wangapi tunao, kwa sababu tukienda sehemu nyingine tunaongeza mashine na watu wa kuzifanyia kazi wanaongezeka.
“Lakini ni watu wengi wanahitajika kwa sababu wakati mwingine wanatakiwa kupokezana, siyo mtu mmoja tangu asubuhi hadi jioni,” alisema Jaji Lubuva.
Alipotakiwa kueleza kama muda uliobaki uandikishaji utamalizika mapema na kufanya Uchaguzi Mkuu Oktoba, alisema hilo ndilo lengo la tume.
“Huu uboreshaji ingetakiwa uwe umeanza muda mrefu huko nyuma, kwa sababu mbalimbali labda ya ukosefu wa fedha tulichelewa. Lakini kati ya sasa na Oktoba tutakuwa tumemaliza, hilo ndilo lengo letu, hiyo ndiyo target (lengo) yetu na jinsi ilivyo uchaguzi hatutaahirisha.
“Ni kweli kwamba sisi ingebidi tuwe na muda mrefu ili tuende polepole kuliko kukimbizana, lakini ‘as its now’ (kama ilivyo sasa) ndiyo (mashine za BVR) tumezipata na mimi na wenzangu kwenye tume tuna matumaini kabisa kuwa hadi Oktoba tutafanya kila liwezekanalo tuboreshe daftari na watu wapige kura, hilo ndiyo la kwangu, ukinibana kwenye hesabu ya kujipima sisi na hao wengine, siyo langu,” alisema.
Alipoulizwa hadi sasa NEC ina mashine ngapi, alisema: “Baada ya zile 250, Aprili 17 tulipokea 1,600 na tarehe 25 mwezi huu tutapokea 1,600 hadi mwisho mwa Mei tutakuwa tumepokea zote 8,000. Kwahiyo tunapata uwezo zaidi.
“Ndiyo maana tunasema hadi Oktoba mapema tutakuwa tumemaliza, kama mambo yanaenda kama tunavyoyaona, tutakuwa tumetoa hadi majina watu wayaone.
“Hizi 1,600 zinatuwezesha kufanya mikoa minne kwa pamoja, ndiyo maana Mei tunaanza kuandikisha kwenye mikoa ya Mbeya, Dodoma, Katavi na Rukwa.
“Kadiri zinavyokuja (BVR) na huku tunaendelea, kwahiyo hadi mwisho wa Mei tutaendelea na tutafika mikoa yote, ndiyo maana tulianza Njombe na zile 250.”
Swali: Hapa tatizo ni muda uliobaki na idadi ya mashine, Njombe ilitumika takribani miezi miwili na kuna mikoa mingine ina changamoto za miundombinu kuliko hata Njombe, huoni kwamba hiyo itakuwa kikwazo?
Jibu: Hata huko Makete kuna visiwa tulikuwa tunatumia boti, kuna vituo hatukupata watu kabisa, ila mimi bado nategemea sasa hivi hadi unakuja uchaguzi tutafanya kila liwezekanalo watu waandikishwe na wapige kura.
Ukinishikia kwenye hesabu za Nigeria kwamba zilikuwa ngapi BVR, sitasema kwa sababu sisi hizo 8,000 ndiyo Serikali imeweza kununua, kwahiyo lazima tufanye kazi na hizo.
Ndiyo nakubali tungehitaji muda, lakini hapa ndipo tulipo na uchaguzi ni lazima ufanyike.
Kwahiyo tutakimbia, tutajitahidi kadiri tutakavyoweza, na kadhalika kuna watu wengine wanatengeneza mazingira kwamba inawezekana watu wasiandikishwe.
Swali: Nani mwenye jukumu la kuhamasisha watu wajiandikishe?
Jibu: Chini ya sheria ya kura ya maoni, tumepewa hiyo kazi, lakini ilikuwa iwe ya watu wengine, hasa ile Tume ya Jaji Warioba (aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba).
Wale ndio wanaojua historia na walivyoenda huko, sisi ingekuwa tu mchakato wa jinsi ya kupiga kura. Lakini bahati nzuri ile sheria ikasema tunaweza kuruhusu vyama vya kiraia, ambavyo hadi sasa tumesharuhusu zaidi ya vyama 300 kufanya hiyo kazi.
Tanzania bara zaidi ya 300 na Zanzibar vipo zaidi ya 70, sisi kazi kama za kutengeneza vijarida tunaendelea nazo.
Kwahiyo kuahirishwa kwa kura ya maoni mbali na sababu ya kuboresha daftari tuliyotoa, wananchi wanapata fursa ya kujielimisha zaidi juu ya Katiba Inayopendekezwa watakayoipigia kura. Kwahiyo kisheria jukumu ni letu.
Swali: Mmepanga kutumia wafanyakazi wangapi kwenye zoezi la uandikishaji na mnatarajia kuwa na vituo vingapi?
Jibu: Wakurugenzi kwa sasa wanatuletea idadi ya watu kwenye maeneo yao kwa sababu ile ya sensa ya kitaifa wakati mwingine kama Makambako idadi ya watu ni kubwa kuliko namba iliyo kwenye sensa.
Kwahiyo sasa hivi wakurugenzi ndo wanatuambia, sasa hivi ‘as we talk’ hiyo idadi sina, kwahiyo kujua idadi ya vituo na mashine ngapi tutaziweka huko ni tatizo.

MAJARIBIO TANZANIA KWA MAJIMBO MATATU
Wakati Kenya ikitumia takribani miaka mitano tangu majaribio yaliyohusisha majimbo 209, Tanzania imeanza majaribo mwaka huu kwa kuhusisha majimbo matatu tu.
Kwa Dar es Salaam, majaribio yalifanyika kwenye kata za Bunju ambako wapigakura 15,123 waliandikishwa kati ya 27,148 na Kata ya Mbweni wapigakura 6,200 waliandikishwa kati ya 8,278.
Takwimu hizi za waliondikishwa zinatokana na makisio ya watu yaliyowekwa kutokana na matokeo ya sensa mwaka 2012.
Mkoa wa Morogoro Kata za Ifakara, Kakingiuka, Ipangala, Mlabani na Viwanja Sitini wapigakura walioandikishwa ni 19,188 wakati makisio yalikuwa watu 17,790 na Mkoa wa Katavi, Halmashauri ya Mlele kata za Ikuba, Usevya na Kibaoni wapigakura 11,210 waliandikishwa wakati makisio yalikuwa watu 11,394.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles