Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Katika jitihada za kuwasaidia watu wenye ulemavu kiafya Serikali imeandaa mwongozo wa utambuzi wa mapema wa watoto wenye ulemavu na kanuni za maadili za afya ya uzazi kwa watu wenye ulemavu kwa watoa huduma za afya.
Akizungumza wakati wa mkutano wa tathmini ya mradi wa kuandika habari za watu wenye ulemavu unaosimamiwa na Shirika la Internews, Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Josephine Lyengi, amesema miongozo hiyo imeshasainiwa na sasa hivi inachapishwa iweze kusambazwa.
Lyengi ambaye aliwasilisha mada kuhusu hatua zinazoendelea serikalini amesema asilimia kubwa ya ulemavu unaweza kuzuiliwa kwa kuboresha mazingira na kuzingatia taratibu za kimsingi za afya.
Amesema pia vyuo vya ufundi stadi kwa ajili ya watu wenye ulemavu ambavyo vilikuwa vimefungwa vinakarabatiwa viweze kufunguliwa.
“Serikali imeandaa vishikwambi (tablets) vya lugha ya alama ambapo kitawezesha wanafunzi wa sekondari kutumia kama kamusi, pia kwa siku zijazo kishikwambi cha vyuo vikuu,” amesema Lyengi.
Hata hivyo amesema bado kuna changamoto ya uelewa wa sera zilizopo, hali duni ya kimaisha, ukosefu wa wataalamu na uchache wa nyenzo za kujimudu.
Naye Mkuu wa Programu wa Taasisi ya Vijana Wenye Ulemavu Tanzania YoWDO, Genarius Geisha, ambaye aliwasilisha mada kuhusu upatikanaji wa habari za watu wenye ulemavu amesema bado kuna changamoto ya kutambua majina sahihi ya kuwaita watu wenye ulemavu na kushauri wahariri na waandishi wa habari wapewe elimu ya kina.
“Mradi umesaidia kupaza sauti kuhusu maisha ya watu wenye ulemavu, waandishi wamejitahidi mno, kazi kubwa imefanyika kwa sababu habari zimegusa kila eneo.
“Kumekuwa na habari za kutoa hamasa kwa jamii namna ya kuishi na watu wenye ulemavu, kuwaheshimu, kuwajali na kuwapenda na kuibua uovu uliojificha katika jamii,” amesema Geisha.
Geisha pia alitoa mfano wa habari zilizochapishwa na Mtanzania Digital ikiwemo ya wanafunzi wasio na ulemavu wanavyowasaidia wenzao kujikinga na corona kwamba inaonyesha jinsi ushirikiano uliopo kwenye shule jumuishi hatua inayosaidia pia kupunguza mtazamo hasi kwenye jamii dhidi ya watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Nipashe, Beatrice Bandawe, aliyewasilisha mada kuhusu uzoefu wake katika habari za watu wenye ulemavu amesema hivi sasa kuna mwamko wa waandishi wengi kuandika habari za watu wenye ulemavu hasa kutoka mikoani tofauti na zamani ambapo ilizoeleka habari nyingi zinatoka Dar es Salaam.
“Vyombo vya habari vimesaidia kutangaza na kuleta mambo chanya ambayo yameboresha ustawi wa watu wenye ulemavu, kazi zinazofanywa na vyombo vya habari zimesaidia kuongeza ufahamu kuhusu umuhimu wa kuwalinda, kuwapa nafasi na kuwainua watu wenye ulemavu,” amesema Bandawe.
Mgeni rasmi katika mkutano huo mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Zainab Kombo Shaib, amewataka waandishi wa habari kuendelea kuibua masuala ya watu wenye ulemavu.
“Nafurahi kuona namna waandishi wa habari wanavyoibua matatizo mbalimbali katika jamii, msichoke kuingia mtaani hadi vijijini mtufikishie habari ili tuweze kuzifuatilia,” amesema.
Mmoja wa waandishi wa habari walioshiriki katika mradi huo kutoka Kituo cha redio cha CG FM Tabora, Vivian Pyuza, amesema baada ya kupata mafunzo kutoka Internews ameweza kufikia malengo aliyoyatarajia kwani habari nyingi alizoandika zimeleta matokeo chanya kwenye jamii.
Naye Mkuu wa Kanda wa Miradi kutoka Internews Kenya, Jackie Lidubwi, amesema mradi huo uliozinduliwa Februari mwaka huu umekuwa na mafanikio makubwa hasa kwa habari zilizoleta matokeo chanya.