ELIZABETH HOMBO-ALIYEKUWA PWANI
RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, amewataka vijana kuzingatia maadili ili waweze kufanikiwa katika maisha yao ikiwemo masomo.
Alitoa kauli hiyo juzi katika mahafali ya saba ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Ahmes iliyoko Bagamoyo mkoani Pwani.
Mwinyi ambaye pia ni mlezi wa shule hiyo, aliwapongeza walimu na uongozi mzima kwa kulea wanafunzi katika maadili na hatimaye shule hiyo kushika nafasi ya tatu kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka 2019.
“Si jambo rahisi wala kuonekana kila mahali kwa watu kuwalea vijana wetu kwa namna mnavyowalea ninyi walimu wa Ahmes na kuwasogeza mbele kila mwaka na maadili ndiyo jambo kubwa lililowafikisheni hapa,” alisema.
Alisema watu wengi wamekuwa wakidhani kwamba shule hiyo ya Ahmes ni yake na kwamba wengi wamekuwa wakimsumbua ili watoto wao wapate nafasi.
“Jamaa zangu na rafiki zangu na watu kwa ujumla wote wanalilia wapate nafasi katika shule hii, maadamu ina initials za jina langu, kwa hiyo tupate nafasi sasa, mkiona foleni msistaajabu. Kwanini nasema hayo, ni kwa sababu mnavyowasogeza vijana wetu kimasomo na kitabia,” alisema.
Vilevile alisema ana imani kwamba wanafunzi walio chini nao wameambukizwa maadili na kwamba watakuwa vijana wazuri huko waendako.
“Tabia ya shule hii ni kama samaki aina ya nyenga ambaye ni samaki maalumu, watu wa Bagamoyo ni wavuvi, samaki huyu kama kuna kitu chini ya maji yeye anakaa juu kabisa anajenga nyumba yake hapo, hakuna anayekuja akamwondoa, yeye ndio yeye.
“Sasa shule hii iko kama huyo samaki, ninawaombea inshallah Mwenyezi Mungu atawafisha mbali,” alisema.
Aliwataka walimu wengine nao kuiga mfano huo kwa kuwalea vijana katika maadili na kuwaongoza kwa malengo na sio tu kufanya kazi kutimiza wajibu bali kwa malengo maalumu.
“Muwafundishe vijana katika kujenga utu wa mwanadamu hapa. Vijana mliobaki mna kazi kubwa ya kufuata nyayo za wenzenu waliofanya vizuri, nyuma msirudi na hatimaye Mwenyezi Mungu atatupa uhai na mtakuwa wa kwanza kitaifa,” alisema.
Awali meneja wa shule hiyo, Sam Mjema, alisema siri ya kufanya vizuri kitaifa ni kutokana na namna wanavyoshirikiana baina ya wazazi, walimu na wanafunzi.
“Lengo letu si mwanafunzi afanye vizuri kimasomo, lakini pia tunawafundisha nidhamu na mfumo mzima wa maisha, sio kwamba anapata daraja la kwanza, lakini kichwani uelewa wake ni mdogo,” alisema Mjema.