Na RAMADHAN HASSAN
-DODOMA
RAIS Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, ametaja sababu za kujiuzulu kwake nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa kulitokana na kulinda heshima ya taifa na ya Rais wa awamu ya kwanza.
Amesema anasikitishwa kuona chanzo cha kujiuzulu kwake bado hadi sasa kipo, ambacho ni mauaji ya vikongwe jambo ambalo ni fedheha kubwa kwa taifa.
Kauli hiyo aliitoa Dodoma jana katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, ambayo kitaifa yamefanyika mkoani hapa.
Alisema hakuna haja kwa sasa kiongozi kujiuzulu kwa sababu ya mauaji bali Serikali inapaswa kupambana na wauaji wote ili kutoruhusu hali hiyo kuendelea.
Alisema mwaka 1976 akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, alilazimika kujiuzulu baada ya kutokea mauaji katika Mkoa wa Shinyanga lakini miaka tisa baadaye akawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka 10.
“Kuongezeka kwa wazee ni jambo jema linaloonyesha taifa linapata maendeleo lakini hili la kuwaua vikongwe ni aibu na fedheha kubwa sana, naomba likomeshwe,” alisema Mwinyi.
Alivitaka vyombo vya habari kutambuwa kuwa vina jukumu la kutoa elimu kwa jamii wakiwamo watu wenye tabia hiyo ya kuwaua vikongwe.
“Mwaka 1976 nilijizulu, kisa ni mauaji ya watu Shinyanga. Nilijiuzulu ili kumwokoa Rais na fedheha (Mwalimu Nyerere)…nikaona aibu inipate mimi.
“… leo bado risala inasema na tumesikia mama Waziri kasikia, viongozi wamesikia, hakutakuwa na haja ya kujiuzulu ila wao ndiyo wanatakiwa kujiuzulu.
“Tunaendelea kukabiliana na mauaji na imani za ushirikina, ni aibu, ila haya yanaendelea kushughulikiwa na sasa mkazo utaongezwa katika utoaji wa elimu kwa jamii,” alisema.
Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema Serikali imetoa kipaumbele kwa wazee na haitasita kuwahudumia kila inapobidi.
Alisema Serikali kila mwezi inapeleka fedha katika kambi 17 za wazee na imekwisha kununua bajaji 10 kwa ajili ya kuwahudumia, yakiwamo majiko matano ya kutumia.
“Kwa sasa Tanzania ni nchi ya pili kwa ubora wa afya za wazee katika nchi 11, hivyo katika hili ni lazima tujipongeze,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Wazee Taifa, Stebastian Mbulegi alisema alimwomba Rais Mstaafu Mwinyi kuwafikishia salamu zao kwa Rais Dk. John Magufuli kuhusina na mambo matano ambayo ni pamoja na kuomba itungwe sheria kuhusiana na Sera ya Taifa ya Wazee ili kuipa nguvu.
Pia alitaka wazee wapate huduma za afya bure na bila malipo kwa vile wamekuwa wakisumbuliwa katika hospitali na vituo vya afya.
“Pia Serikali ikomeshe mauaji ya vikongwe kutokana na imani za ushirikina, itoe malipo ya pensheni kwa wazee wote ikizingatiwa kwa sasa ni asilimia nne tu ya wazee wanaopata na asilimia 96 hawapati,” alisema Mbulegi.
Pia Mwenyekiti huyo alimwomba Rais huyo Mstaafu, wazee washirikishwe katika ngazi mbalimbali za uamuzi kama vile kupatiwa viti maalumu vya ubunge na udiwani.