NA KULWA MZEE
-DAR ES SALAAM
UPANDE wa Jamhuri umemfikisha mahakamani msanii wa maigizo, Bulton Mwemba ‘Mwijaku’ (35) kwa tuhuma za kusambaza picha za utupu mtandaoni, na amepelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Mwijaku ambaye pia kwenye uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutafuta wagombea ubunge alishiriki kwenye Jimbo la Kawe na kupata kura 0, alipanda kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Richard Kabate.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon akisaidiana na Wakili Mwanaamina Kombakono, walidai mshtakiwa mkazi wa Mbezi Beach, alitenda kosa hilo katika terehe tofauti kati ya Septemba 17 hadi Oktoba 10 mwaka 2019 jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa katika tarehe hizo alisambaza picha za utupu akitumia kompyuta yake kupitia mtandao wa WhatsApp.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Mwijaku alikana kutenda kosa hilo. Upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo upo hatua za mwisho.
Mahakama ilikubali kumpa ‘summons’ kwa masharti kwamba atakuwa nje kwa dhamana akiwa na wadhamini wawili ambao ni wasanii wenzake kutoka tasnia ya filamu – ‘Bongo movie’ au muziki – ‘Bongo fleva’.
Wasanii hao watatakiwa wawe na barua za utambulisho zitakazothibitishwa na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) watakaosaini dhamana ya Sh 500,000 kila mmoja.
Hata hivyo, Mwijaku alishindwa kutimiza masharti hayo na kupelekwa rumande hadi Agosti 12, mwaka huu kesi itakapotajwa.