24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Maelfu wamzika Mkapa

Na MWANDISHI WETU – MASASI

MAELFU ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, wameungana na wenzao wa mikoa ya kusini, viongozi wa Serikali na wa dini katika safari ya mwisho ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye amezikwa jana kijijini kwake Lupaso, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Mazishi ya Mkapa aliyefariki dunia usiku wa Julai 23, yaliongozwa na Rais Dk. John Magufuli ambaye aliambatana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya tatu, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Shughuli za mazishi zilianza saa 1 asubuhi na ilipofika saa tisa alasiri, mwili wa Mkapa uliingizwa kaburini.

ASKOFU NYAISOMBA

Katika ibada ya mwisho iliyofanyika nyumbani kwake katika Kijiji cha Lupaso, Askofu Gerasi Nyaisomba alimwelezea Mkapa kama mtu mwenye karama ya pekee, aliyejinyenyekeza kwa Mungu hadi hatua ya mwisho.

Alisema akiwa katika mafunzo yake katika nchi mbalimbali alizopitia, alijifunza na kuishi kile anachokiamini katika mazingira yake yote.

Askofu Nyaisomba alisema Mkapa katika utawala wake alihakikisha anatawala kwa haki na pale alipokosea alitambua makosa yake na kukiri.

“Kila alipoishi alijifunza kuishi kulingana na mazingira. Lakini alijali na kuheshimu toba. Alifanya toba muhimu kwa kuandika kitabu chake, ‘My Life My Purpose’, hiyo ni toba ya uungwana na usikivu,” alisema Askofu Nyaisomba.

Alisema Kanisa halitarajii kuona mtu yeyote anafika akiwa na hatimiliki ya kuwaongezea wafiwa machungu kwa njia yoyote, ikiwemo kupitia mitandao ya kijamii.

Askofu Nyaisomba alisema anatoa pole kwa familia ya marehemu Mkapa, kwa Rais Magufuli, makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri Mkuu Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Ali Idd, Rais wa Zanzibar, Dk. Shein,  Serikali zote mbili na Watanzania wote.

Aliomba kila mmoja katika tukio hilo amuone mwenzake amefanya vizuri kuliko yeye kwa kuwa ndiyo iliyokuwa hulka ya ndani ya Mkapa.

“Kwa Mkapa, katika watu aliowapatia shughuli aliamini kwamba watafanya vizuri kuliko yeye. Kwa hiyo hilo ni jambo alilojivunia, kuwapa watu majukumu huku akiamini kuwa watafanya vizuri zaidi ya namna ambavyo angefanya yeye. Hili ni suala la kulienzi,” alisema Askofu Nyaisomba.

Alisema kifo chake kiwe ndiyo mwanzo wa kuiunganisha familia ambayo sasa ataendelea kuiombea ili iwe imara zaidi ya ilivyokuwa awali.

BALOZI WA MSUMBIJI

Balozi wa Msumbiji nchini, Monica Musa, aliwasilisha salamu za rambirambi kutoka kwa Rais Philippe Nyusi wa nchi hiyo.

Alisema katika ujumbe wa Rais Nyusi, alitoa salamu za rambirambi kwa Rais Magufuli kwa kifo cha rais huyo mstaafu pamoja na familia yake, akiwaombea wapate ahueni ya mapema kutokana na kumpoteza mpendwa wao.

“Rais Nyusi anawatakia familia mshikamano na matumaini, wawe na nguvu ya kushinda wakati huu wakimpoteza mpendwa wao Mkapa,” alisema Balozi Monica.

Alisema Rais Nyusi ameshindwa kufika mwenyewe msibani baada ya kupata dharura, lakini ametuma ujumbe, unaoambatana na ujumbe wa Rais wa zamani nchini humo, Joachim Chisano.

DK. SHEIN

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisema kusanyiko la jana lilikuwa na dhumuni kuu la kumsindikiza marehemu Mkapa katika safari yake ya mwisho.

Alisema wananchi wa Zanzibar wanaungana na Watanzania wote, wananchi wa Mtwara hususan Masasi katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza kifo cha mtu muhimu aliyeacha alama katika taifa.

“Takribani siku sita zilizopita taifa liliingia katika machozi, ila ni vyema kwenda mbele za Mungu na kumwombea amsitiri mahali pema,” alisema Dk. Shein.

Alisema Mkapa aliyahifadhi na kuyatunza Mapinduzi ya Zanzibar, aliuhifadhi na kuulinda Muungano kwa vitendo, hivyo ni sahihi kumuunga mkono kwa vitendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles