Na LEONARD MANG’OHA-ALIYEKUWA KIBAHA
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Tanzania, Charles Mwijage, amesema ukuaji wa uchumi unapaswa kwenda sambamba na kasi ya kukuwa kwa maendeleo nchini.
Ametoa kauli hiyo jana wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza sabuni na vipodozi cha Kampuni ya Keds Tanzania Limited ya nchini China, kinachotarajiwa kuanza ujenzi hivi karibuni.
Waziri Mwijage alisema hatua iliyofikiwa na kampuni hiyo kuelekea ujenzi wa kiwanda hicho ni miongoni mwa kazi nzuri ya kujivunia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
“Kiwanda hiki kikikamilika kitakuwa kinazalisha tani 50,000 kwa mwaka huku mauzo ya kampuni yakiwa ni dola za Marekani milioni 33 kwa mwaka, hii inatoa matumaini kufikia lengo sekta ya viwanda kutoa walau asilimia 40 ya ajira zote.
“Kinachonifurahisha na kuona kuwa wataanza uzalishaji mapema ni kuwa shughuli ya kutayarisha eneo la ujenzi wa kiwanda hiki umechukua siku 28 tu na wameniambia kuwa ndani ya miezi saba wataanza uzalishaji,” alisema Waziri Mwijage.
Alisema Serikali itahakikisha inaendelea na juhudi zake za kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini ili kuhakikisha wanawekeza mikoa yote nchini na kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya nyingine kwenda wilayani Kibaha kujifunza namna ambavyo wilaya hiyo imefanikiwa kuwavutia wamekezaji kuwekeza.
“Niwaeleze tu uongozi wa Kampuni ya Keds, hakuna sababu ya kwenda nchi nyingine, zalisheni hapa mkauze katika nchi hizo ambako mtaona kuna soko la bidhaa zenu,” alisema.
Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika kiwanda hicho kinachotarajiwa kuwekeza kiasi cha dola za Marekani milioni 12, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Cliord Tandari, alisema kuwa utakuwa na faida kuwa kwa wananchi.
“Kwanza kitazalisha ajira za moja kwa moja 2,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 2,000 lakini pia utasaidia kupunguza matumizi ya fedha zetu za kigeni kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi na pengine niwatake kuendelea kuwa mabalozi wazuri na kuendelea kuzitangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini,” alisema Tandari.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Keds Tanzania Limited, Jack Feng, alisema kampuni hiyo itaendelea na shughuli za uwekezaji katika maeneo mengine hasa katika uwekezaji wa viwanda.
“Tutaendelea pia kuwashawishi wenzetu kuja kuwekeza Tanzania kwa kuzingatia kuwa Tanzania ina amani na kuna miundombinu mizuri ya kutuwezesha kwenda mahali popote, hata ukiangalia hapa tunapojenga tuko karibu na barabara kuu ya Morogoro,” alisema Feng.