28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mwijage ataja sababu sita uchumi wa viwanda  

MwijageNa RAMADHAN HASSAN, DODOMA

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, ametaja sababu sita za Serikali kuingia katika uchumi wa viwanda.

Alizitaja sababu hizo mjini hapa jana, wakati akifunga kikao cha ushiriki wa mifuko ya hifadhi ya jamii katika uchumi wa viwanda, ambao ulihudhuriwa na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk. Hamisi Kigwangala na Naibu Waziri wa Kilimo, Mfugo na Uvuvi, William ole Nasha.

Waziri Mwijage alizitaja sababu hizo kuwa moja hadi tatu ni ajira, huku nyingine zikiwa ni kuzalisha bidhaa ili kukidhi mahitaji, kuchangamsha uchumi pamoja na kukusanya kodi.

“Nazitaja sababu sita za kuingia katika uchumi wa viwanda, moja ni ajira, mbili ni ajira, tatu ajira, nne ni kuzalisha bidhaa ili kukidhi mahitaji yetu, tano kuchangamsha uchumi wetu na sita tuweze kukusanya kodi ili tuweze kupata mapato yatakayoongeza uchumi wetu,” alisema.

Aliwata Watanzania kuwekeza katika zao la asali ambalo soko lake lipo ndani na nje ya nchi.

“Jamani wekezeni katika asali, soko lake lipo waziwazi, hata ikiwezekana Watanzania wote tuanze kufuga nyuki ili tupate asali, soko lake lipo kila mahali,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania (TSSA), Meshach Bandawe, alisema walikutana na Serikali ili kujua namna watakavyoweza kutekeleza ushiriki wao katika uchumi wa viwanda.

“Kikubwa tunahitaji na kuomba ushirikiano kutoka serikalini, tunaamini kama tutawekeza katika uchumi wa viwanda mpaka ifikapo 2020, asilimia 40 ya Watanzania watakuwa na ajira na sisi tunataka viwanda ambavyo vina tija bila ya kuathiri mfuko,” alisema.

Akifungua mkutano huo, Waziri Jenister alisema mifuko ya jamii inatakiwa kutumia fursa ya kuwekeza katika uchumi wa viwanda ili kutoa ajira kwa mamilioni ya Watanzania.

“Mkusanyiko huu utatusaidia kupiga hatua katika kufikia uchumi wa viwanda, uwekezaji katika viwanda uendane na malighafi za Tanzania, tunaweza kuwekeza katika viwanda vya nguo na ngozi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles