29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mwigulu, January wakana kukacha mdahalo

januaryMWIGULUNCHEMBANa Waandishi Wetu, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, wamekana taarifa za kukimbia kushiriki mdahalo uliokuwa umeandaliwa na CEO Round table (CEOrt), na kudai kuwa mabadiliko ya ratiba ndiyo yaliyosababisha hali hiyo.
Makada hao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walisema hayo kupitia mitandao yao ya kijamii ya Facebook na Tweter, ambapo Mwigulu alisema ratiba ya mdahalo kubadilika ndiyo iliyomfanya ashindwe kuhudhuria.
“Kumradhi wote, hatujakimbia mdahalo ila kubadilika kwa ratiba ndio imefanya hali hiyo itokee, awali tuliambiwa ni leo (juzi) asubuhi, tukajiandaa nikaaga ofisini, ikabadilika tena nikaambiwa Jumamosi wiki ijayo, nikafurahi zaidi kwani ilikuwa nzuri.
“Nikafuta ruhusa na sasa nikiwa Dodoma naambiwa ni leo (juzi) sio Jumamosi tena na nilikuwa tayari nimechelewa kwenda Dar kwa gari ambapo ndege ya mwisho ya Dodoma kwenda Dar es Salaam ni saa tatu asubuhi.
“Kwa sasa nashughulikia kupata nafasi ya mdahalo mwingine, ni fursa nzuri kwa Watanzania kutusikiliza na kufanya uamuzi wa kiongozi yupi ana ajenda zinazowahusu moja kwa moja,” alisema Mwigulu
Kwa upande wake, Makamba aliandika kupitia akaunti yake ya Tweter kwamba awali alikubali kushiriki mdahalo ratiba ikiwa ni asubuhi, lakini ilipobadilika na kuwa usiku alishindwa kufika kutokana na kuingiliana na ratiba nyingine.
“Mdahalo nilikubali kushiriki mwaliko wa awali ambapo ilikuwa ni asubuhi ya leo (juzi), kuhamishiwa usiku kumeingiliana na ratiba yetu, lakini bado kuna round (mzunguko) zijazo,” alisema Makamba.
Kutofika kwa makada hao katika ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam juzi, kulisababisha kuahirishwa kwa mdahalo huo ambapo hadi kufikia saa 1:20 usiku alikuwa amefika mgombea mmoja, Balozi Amina Salum Ali, kati ya wagombea watano walioalikwa na kuthibitisha kushiriki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles