23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

RC Gama amjibu Halima Mdee

Halima-MdeeNA RODRICK MUSHI, MOSHI
SIKU moja baada ya Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee (Chadema), kumlipua Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, akidai kuwa amekuwa dalali wa viwanja, hatimaye amejibu mapigo na kusema kusakamwa kwake kunatokana na msimamo wake dhidi ya wa wanywaji pombe wilayani Rombo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, alisema kauli ya Mdee imejaa siasa, hasa kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, lakini hatorudi nyuma.
Alisema pamoja na kusakamwa kwake ndani ya Bunge na wapinzani, alishangazwa na hatua ya kuhusishwa na kufunguliwa kwa Soko la Kati mjini Moshi, ambalo awali lilikuwa limefungwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), akisema huenda itakuwa imeongeza hasira, hasa baada ya upinzani kushindwa kuwatetea wanyonge.
“Ninapenda kusema kuwa sitoruhusu upikaji wa gongo uendelee kwenye mkoa wangu, na nitaendelea kupambana na hilo, sasa naona msimamo wangu na jitihada ambazo nimekuwa nikifanya imekuwa nongwa, mimi najiamini ni msafi, sina wasiwasi katika hilo,” alisema Gama.
Alisema anashangazwa na kauli ya Mdee kudai kuwa ameshirikiana na Kampuni ya Jun Yu Investment International ya nchini China, kutaka kumiliki ardhi iliyokwishalipiwa fidia na Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ya Sh milion 168 kinyume cha sheria.
Gama alisema alifanya juhudi kiwanda cha saruji kujengwa Kilimanjaro kwa ajili ya kuinua uchumi pamoja na nafasi ya ajira, ambapo aliwaomba wawekezaji hao kujenga katika Wilaya ya Rombo katika eneo la halmashauri na sio la mwekezaji.
“Walipojenga kiwanda siyo mali yangu na wala sikuhusika kudalalia, ni mali ya halmashauri ambayo ilihusika pia kuwalipa fidia wananchi ambao walikuwa na eneo hilo,” alisema Gama.
Alisema hana hisa kwenye kampuni hiyo huku akikiri mtoto wake Muyanga Gama, kuwa ni mmoja wa wanahisa katika kampuni hiyo ambapo ni haki yake kisheria kutokana na makubaliano waliyofikia na wenzake.
“Kama kweli nilikuwa nimehongwa shilingi milioni 500 ungekuta nimebaki kwenye ukuu wa mkoa? Na kama hizo fedha zipo naomba wazilete, na pia suala la hisa ni haki yangu, lakini katika hiki kiwanda cha saruji sina hisa hata moja,” alisema.
Kwa upande wa eneo la Lokolova alisema tayari limeshabadilishwa kutoka eneo la kilimo na ufugaji kwenda viwanda na biashara na kinachosubiriwa ni mkopo kutoka Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), ambapo kila hatua inasimamiwa na mkoa.
“Kitu kikishasemwa bungeni hata kama siyo kweli unayetajwa huna sehemu ya kuzungumzia, ila ukweli wawekezaji wa Rombo walikuwa wanataka kwenda kuwekeza Bagamoyo, ndiyo nikamwambia mwanangu pamoja na wenzake ambao walikubali kuwekeza hapa,” alisema.
Kuhusu kutajwa kuhusika katika kiwanja cha Mawenzi chenye hati namba C.T 056035 kilichopo chini ya Mawenzi Sport Club, alisema kilichofanyika ni suala la kisheria.
Alisema sheria za ardhi, mmiliki akishajenga na kuwa na hati, hata asipolipia miaka 100 bado eneo litaendelea kuwa ni mali yake na ndiyo kilichotokea eneo la Mawenzi.
“Manispaa hawakutaka kutekeleza sheria ya ardhi, na wamiliki walitaka kwenda mahakamani kushitaki manispaa na mimi sikuwa tayari kwa hilo, na kama madiwani walitaka kutetea haki wangetoa mapendekezo kwa rais afute hiyo.
“Madiwani wamepeleka kesi mahakamani,wakachangishana fedha kudai eneo kuwa ni lao, lakini wameshindwa mahakamani, mbona hawasemi kama walishindwa na mimi sitoi haki kwa upendeleo kwa kuwa manispaa ni Serikali, hapana,” alisema.
Juzi Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mdee, alidai kuwa Gama anahusika na ufisadi wa kutaka kumiliki ardhi katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Wilaya ya Rombo mkoani humo.
Kutokana na hali hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuzuia mchakato wowote haramu utakaofanywa na Gama kuhusu ardhi.
Mdee alimtaja Gama wakati akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2015/16 mjini Dodoma juzi.
Alisema Gama akishirikiana na kampuni binafsi ya Jun Yu Investment International, anataka kumiliki ardhi iliyokwishalipiwa fidia ya Sh milioni 168 na Halmashauri ya Wilaya ya Rombo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles