23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

152 mbaroni kwa kujiandikisha mara mbili BVR

NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, limewatia mbaroni watu 152 wa Mkoa wa Njombe kwa tuhuma za kujiandikisha mara mbili katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa elektroniki (BVR).
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi wa NEC, Dk. Sisti Cariah, alisema watuhumiwa hao walinaswa kupitia vifaa maalumu na watashtakiwa kwa kosa la jinai ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema mfumo mpya wa BVR utasaidia kupunguza au kuondoa matatizo yaliyomo kwenye daftari lililopo ikiwamo kuzuia mtu kujiandikisha zaidi ya mara moja.
Dk. Cariah, pamoja na hali hiyo alisema lakini NEC inakabiliwa na changamoto ikiwamo ongezeko la kata mpya 130 ambazo zimeongezwa na TAMISEMI, hali inayowafanya warudi tena kuendelea na kazi hiyo ikiwamo kwenda kuhakiki mipaka.
“Tumelazimika kusogeza mbele zoezi la uboreshaji kwa mikoa minne kutokana na mabadiliko yanayoendelea kufanywa ya mipaka ya kiutawala ya kata, vijiji, vitongoji na mitaa ambapo mabadiliko hayo yanatakiwa kufanyiwa kazi katika mfumo wa uboreshaji daftari la wapigakura,” alisema Dk. Cariah.
Alitaja mikoa iliyosogezwa mbele uboreshaji wa daftari hilo kuwa ni Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Mara ambapo awali ilitangazwa kazi hiyo ingeanza jana na badala yake itaanza Juni 16.
Dk. Cariah alisema wamepata mafanikio makubwa katika uboreshaji daftari hilo ambapo hadi sasa wamefanikiwa kukamilisha kazi hiyo katika mikoa ya Lindi, Njombe, Mtwara, Ruvuma, Geita, Iringa na Shinyanga.
Akifafanua baadhi ya mafanikio hayo, alisema kwa Lindi wamefanikiwa kuandikisha wananchi 529,224 ambapo takwimu zilizopo zinasema watakaokuwa na sifa za kupiga kura wenye umri wa miaka 18 katika mkoa huo ni 518,230.
Alisema kazi hiyo inaendelea pia katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Mbeya, Tabora, Kagera na Dodoma ambapo Mkoa wa Dar es Salaam itafanyika Julai 2, na itakuwa ya haraka zaidi kutokana na wingi wa vifaa vitakavyokuwapo.
Dk. Cariah alisema kwa upande wa visiwani Zanzibar, watakaoandikishwa ni wale waliokosa sifa za ukazi ambazo kigezo chake kilikuwa ni lazima raia huyo awe ameishi visiwani humo zaidi ya miezi 36.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles