24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mwenyekiti UWT ahamia Chadema

NA JANETH MUSHI, ARUSHA

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Arusha, Vicky Mollel amekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mollel ambaye aliwahi kuwa Diwani wa Viti Maalum Kata ya Daraja Mbili kupitia CCM anatarajiwa kukabidhiwa kadi ya uanachama Jumatano   wiki  hii  na aliyekuwa mgombea urais wa Ukawa kupitia Chadema, Edward Lowassa.

Mollel aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa ameamua kukihama CCM baada ya kuchoshwa na majungu yanayoendelea ndani ya chama hicho ambako kila kukicha wanatafuta mchawi anayekihujumu.

“CCM imegeuka jamvi la kusutana kila kukicha wanatafuta mchawi ni nani anayehujumu chama, mwenendo wa CCM kujadili watu wanaokihujumu chama ulinikatisha tama,” alisema Vicky na kuongeza:

“Nilipokaa niliona nadhoofisha kipaji changu kwa kumuogopa mwanadamu kwani ninachoamini ni kwamba  chama kinaongozwa na katiba na kanuni.

“Lakini badala yake wachache wanaongoza CCM huku wakidhani kuwa siasa ni kuzua majungu na chuki, ndiyo maana nimeamua kuhama bila kushawishiwa na mtu”.

Alisema   ameamua kuhama CCM ili kuendeleza harakati za ukombozi na kuwa   yeye siyo wa kwanza kukihama chama hicho.

Hakuna aliyekuwa anajua uchungu wa CCM kama Kingunge Ngombale Mwiru na Lowassa, lakini waliamua kuondoka ingawa  wananchi bado wanawahitaji baada ya CCM kuwakataa, alisema.

“Ninamshukuru Lema kwani tulikuwa mahasimu wa muda mrefu ila sasa nimeamini katika  siasa hakuna urafiki wala uadui wa kudumu… nawaomba radhi kina mama wa CCM walionichagua na nawakaribisha huku (Chadema),” alisema Mollel.

Awali mgombea ubunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema  Mollel amechelewa kuhamia upinzani kwa sababu nguvu yake ilihitajika kwa muda mrefu na   kuanzia jana aliingia kwenye timu ya kampeni za ubunge jimboni humo.

“Vicky alikuwa mtu hatari anayetembea usiku kama popo kwa ajili ya CCM Arusha.  Mwanamke aliyekuwa amebaki kufufua CCM ni yeye na ninakuhakikishia kuwa Chadema hutapata shida.

“Tutashirikiana na wewe kwa kila jambo katika kukijenga chama chetu,” alisema Lema

Mollel alipokewa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Arusha Mjini, Derick Magoma ambaye aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura  waweze kumchagua kiongozi wanayemtaka atakayewaletea maendeleo.

Desemba 13 mwaka huu, wananchi wa jimbo hilo wanatarajia kupiga kura za ubunge katika uchaguzi mdogo ambao uchaguzi wa Mbunge uliahirishwa baada ya aliyekuwa Mgombea Ubunge wa Chama cha ACT-Wazalendo, Estomih Mallah kufariki dunia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles