30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

MWENYEKITI UVCCM ARUSHA AKAMATWA NA POLISI

Na JANETH MUSHI -ARUSHA

JESHI la Polisi mkoa wa Arusha  linamshikilia Diwani wa Kata ya Sambasha, Lengai ole Sabaya (CCM) kwa tuhuma za kujifanya ofisa usalama wa taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema walimkamata ole Sabaya kwa tuhuma hizo ambazo alishawahi kuzitenda siku zilizopita na kufikishwa mahakamani ambako shauri hilo lilifutwa.

Alisema  baada ya kesi hiyo kuondolewa  waliendelea kufanya uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili mtuhumiwa huyo ambaye pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mkoa wa Arusha.

“Ni kweli amekamatwa na yupo kituo cha polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.

“Tunamshikilia kwa kosa ambalo alishawahi kulitenda huko nyuma na liliondoshwa mahakamani kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi na kwa kuwa uchunguzi umekamilika, hati iko tayari.

“Kosa alilokamatwa nalo ni kwamba  alijifanya yeye ni ofisa usalama wa taifa  wakati siyo kweli. Kwa kuwa suala la upelelezi ni la utaalamu na lengo la kupeleleza kesi ni ili iwe na mafanikio, hayo madai ya kusema amekamatwa kwa sababu za siasa sisi siyo wanasiasa na hatuyajui kwa sababu sisi ni watendaji tunaofanya kazi kwa mujibu wa sheria.

“Kwa hiyo mwenye kusema maneno  hatuwezi kumzuia, lakini ukweli ndiyo huo na hili shauri lilishatokea huko nyuma na masuala ya upelelezi ni mapana.

“Yaani kadri unavyokwenda ndivyo unagundua ni kipi sijakiweka sawa. Suala la kusema alishawahi kufikishwa mahakamani au vinginevyo hilo suala liachiwe upande wa upelelezi kwani pia mahakama itatenda haki kila upande utakapokuwa umewasilisha ushahidi wake,”alisema Kamanda Mkumbo.

Awali, Aprili 28 mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ilimwachia huru ole Sabaya baada ya kufuta kesi iliyokuwa ikimkabili kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles