23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

MWEKEZAJI ADAIWA KUHUJUMU WACHIMBAJI WADOGO

Na Masyaga Matinyi – Mererani

KAMPUNI ya Tanzanite One Limited, inayochimba madini ya vito aina ya tanzanite katika eneo la Mererani mkoani Manyara, imetajwa kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani na migogoro ya mara kwa mara.

Chanzo kikuu cha migogoro na uvunjifu wa amani ambao umegharimu maisha ya wachimbaji wadogo kadhaa, ni mwingiliano wa njia za uchimbaji chini ya ardhi, maarufu kwa jina la “mitobozano” na matumizi ya nguvu kubwa dhidi ya wachimbaji wadogo, yakiwamo mabomu ya machozi na risasi za moto.

Ukiacha mwekezaji Tanzanite One Limited inayomilikiwa na Kampuni ya Sky Associates Group Limited iliyosajiliwa katika nchi ya British Virgin Islands na kufanya kazi zake Hong Kong, kuna zaidi ya wachimbaji wadogo na wa kati 400 katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa kanuni na taratibu za uchimbaji wa tanzanite, unapotokea mtobozano, unapaswa kutatuliwa na kamati ya pamoja inayoundwa na pande zinazohusika, jambo ambalo limekuwa halifanyiki.

Pia imebainika pasipo shaka kuwa hakuna ramani rasmi kuonyesha nani anapaswa kuwa wapi katika eneo hilo, isipokuwa shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa kufuata eneo lililoombewa leseni.

Katika kuthibitisha hilo, MTANZANIA lilizungumza na Kamishna wa Madini, Wizara ya Nishati na Madini, Benjamin Mchwampaka, ambaye alithibitisha kutokuwapo ramani rasmi ya eneo hilo nyeti kwa uchumi wa Tanzania.

“Ni kweli hakuna ‘official map’ ya Mererani kubainisha maeneo ya uchimbaji, kwa hiyo maeneo ya uchimbaji yanatokana na leseni zilizotolewa,” alisema Kamishna Mchwampaka.

HUJUMA

Mwekezaji Tanzanite One Limited, anadaiwa kutumia ukubwa wa eneo lililobainishwa katika leseni yake namba ML 490/2013 ambalo ni kilometa za mraba 7.6 (tutafafanua baadae) kuwahujumu wachimbaji wadogo, ambao kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 2010, leseni zao zinaruhusu kufanya shughuli za uchimbaji katika eneo lenye ukubwa wa kilometa moja ya mraba.

Sheria ya Madini ya 2010, kifungu cha 5 (1) kifungu kidogo cha (f) inasema (tafsiri isiyo rasmi): “Kwa leseni ya uchimbaji wa malighafi za ujenzi au madini ya vito ukiacha almasi, ukubwa wa eneo utakuwa kilometa ya mraba moja (hekari 100).”

Kwa mujibu wa wachimbaji wadogo, wa kati na viongozi wa vyama vyao ambao walizungumza kwa nyakati tofauti, mifano halisi kuwa mwekezaji huyo amekuwa na utaratibu usio mzuri na wa haki kuingia katika migodi ya wachimbaji wengine chini ya ardhi.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi na Wauzaji Madini Tanzania (TAMIDA) ambaye pia ni mchimbaji wa tanzanite, Sammy Mollel, alisema mchezo huo wa mwekezaji ni tatizo kubwa kwa sasa migodini hapo.

Alisema: “Mitobozano ni jambo ambalo haliepukiki katika mazingira tunayofanya kazi kule migodini, lakini unapotokea mtobozano kuna taratibu ambazo tumejiwekea za kupata suluhu na kazi kuendelea.

“Lakini wanachofanya hawa wenzetu si jambo lenye tija, haiwezekani mtu uchimbe chini mwaka mzima, unapofikia mkanda sasa uanze kupata mawe, wao wanakuja na kudai umeingia kwenye eneo lao.

“Na wakija ni vita, wanaambatana na askari wao wenye silaha na polisi, yatapigwa mabomu ya machozi na wakati mwingine risasi za moto. Na kumbuka hayo yote yanafanyika chini ya ardhi, madhara huwa ni makubwa sana kwa upande wetu, na taarifa zote zikiwamo za majeruhi na vifo zipo polisi.”

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Chama cha Wachimba Madini Manyara (MAREMA), Zephania Mungaya, alisema vimeshafanyika vikao vingi kujaribu kupata suluhu na mwekezaji bila mafanikio.

“Hawa wenzetu wana nguvu kubwa, tumejaribu njia nyingi vikiwamo vikao, lakini wapi, wanachama wetu wengi wameathirika kiuchumi, kibiashara na kwa namna nyinginezo, hata ukienda polisi kesi ni nyingi, lakini mambo ni yale yale.

“Baya zaidi unapokutana na hawa Tanzanite One chini ya ardhi hawakuachi ukiwa kama walivyokukuta, watachukua hadi vitendea kazi vyako, na hata sasa ukienda kule kwenye eneo lao, utakuta vifaa vingi vya wachimbaji wadogo,” alisema.

MTANZANIA ilifanikiwa kufika kwenye mgodi wa mmoja wa wachimbaji walioathirika na vita ya mitobozano, Said Nasoro, maarufu kwa jina la Mwarabu, ambaye alianza shughuli za uchimbaji Oktoba 2012.

Nasoro ambaye tofauti na wachimbaji wengine, alikuwa na mpango ambao alishaanza utekelezaji wake wa kujenga chuo kidogo na kiwanda cha kusanifu madini katika eneo la mgodi wake, jambo ambalo lingesaidia kufundisha Watanzania jinsi ya kusanifu mawe na kutoa ajira.

Lakini kwa sasa mradi huo umesimama baada ya Tanzanite One kumzuia kuendelea kuchimba ilihali alikuwa amekaribia kupata madini baada ya kuufikia mkondo. Alirudishwa nyuma umbali wa mita 600 na baadhi ya vifaa vyake vilitaifishwa.

“Tukio lile lilikuwa baya sana lilitokea Novemba 2015, kwa sababu kabla ya kuukaribia mkondo wa madini, nilishachimba kwa takribani miaka miwili na kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 2, ambazo ni mikopo ya benki na nyingine kutoka kwa wabia wenzangu.

“Baada ya kurudishwa nyuma kwa nguvu, ilibidi nianze kuchimba kuelekea mwelekeo mwingine. Kwa hiyo ndiyo hali halisi ya hapa, wakipata taarifa kwamba unakaribia kupata madini, wanakuvamia na kudai ni eneo lao.

“Niliathirika kabisa kisaikolojia na hata kiafya, lile tukio lilinisababishia shinikizo la damu, ambalo hadi sasa linanisumbua sana.

“Kwa sababu wasingenirudisha nyuma, hii leo tungekuwa na shule ya kukata madini na kiwanda na kwa kufanya hivyo tungekuwa tunaungana na Rais Magufuli kujenga Tanzania ya viwanda, lakini kila kitu kimesimama kama unavyoona,” alisema Nasoro.

Akizungumzia tuhuma dhidi yao, mmoja wa wakurugenzi na wamiliki wa Sky Associates Group Limited, Faisal Shahbhai, alikiri kuwapo kwa mitobozano na kuwatupia lawama wachimbaji wadogo na wa kati kuwa wao ndio huingia katika eneo lao kwa makusudi kwa lengo la kuiba madini.

Alipoulizwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Massawe, alisema taarifa za matukio hayo wanazo na zinashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

UJANJA

Kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010, leseni ya madini ya vito haipaswi kutolewa kwa eneo linalozidi kilometa ya mraba moja.

Lakini leseni ya Tanzanite One yenye namba ML 490/2013 inaonyesha kuwa kampuni hiyo inachimba tanzanite, marble na graphite, jambo ambalo liliiwezesha kupewa eneo la kilometa za mraba 7.6.

Pamoja na leseni hiyo kuonyesha aina ya madini yanayopaswa kuchimbwa, lakini kwa takribani miaka mitatu sasa tangu Sky Associates wanunue Tanzania One Limited, hawajawahi kuchimba marble na graphite.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Sky Associates, Shahbhai, alikiri kampuni hiyo kuchimba madini hayo pekee na kudai wapo mbioni kuanza kuchimba graphite na marble baada ya kupata soko, ingawaje hakutaka kutaja lilipo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles